Prime
Dk Nchimbi akerwa na kauli za chuki kwa upinzani

Muktasari:
- Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, amepiga marufuku kauli na nyimbo zinazojenga chuki badala ya mshikamano wa kitaifa.
Dar es Salaam. Kauli na nyimbo mbaya kwa upinzani, za kibaguzi na matendo yenye taswira yanayoweza kutafsiriwa kuwa ni kushabikia ukandamizaji wa haki za wananchi zimeendelea kumkera Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi.
Ikiwa ni kwa mara ya tatu, jana Dk Nchimbi akiwa Shirati wilayani Rorya akiendelea na ziara ya siku sita, alilazimika kutoa onyo akikerwa na nyimbo na kauli mbaya kutoka ndani ya chama hicho dhidi ya upinzani, akisema CCM inapaswa kuwa mfano wa lugha zinazowaunganisha Watanzania.
Akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji na viongozi wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) ngazi za mikoa na wilaya zote, Ihemi mkoani Iringa Julai 11, 2024, Dk Nchimbi aliwataka viongozi na wanachama wa CCM kuepuka kutoa kauli au kufanya vitendo vyenye taswira inayoweza kutafsiriwa kuwa baadhi yao wanashabikia ukandamizaji wa haki za wananchi.
Kama haitoshi, Dk Nchimbi alikemea kauli iliyotolewa Aprili 2024 na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera, Faris Buruhan, ya kulitaka Jeshi la Polisi kutowatafuta vijana wanaotukana viongozi pindi wanapopotezwa.
Kuhusu nyimbo
Akizungumza leo Ijumaa Aprili 25, 2025 na wananchi wa Shirati wilayani Tarime akiendelea na ziara ya siku sita, Dk Nchimbi ameonyesha kukerwa na nyimbo na kauli mbaya kutoka ndani ya chama hicho dhidi ya upinzani, akisema CCM inapaswa kuwa mfano wa lugha zinazowaunganisha Watanzania.
Kwa sababu chama hicho ndicho kilicholiasisi Taifa, amesema wanachama wake hawapaswi kuwa chanzo cha uchochezi, vurugu na namna yoyote itakayochochea umwagaji damu nchini.
Kauli ya Dk Nchimbi inatokana na hivi karibuni kusambaa video kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha wafuasi wa CCM wakiimba wimbo dhidi ya vyama vya upinzani.
Baadhi ya maneno katika wimbo huo yanasikika: "Upinzani ukifa... mimi siwezi kulia... nitawatupa mtoni, wawe chakula cha mamba."
Dk Nchimbi baada ya kuwasikilizisha kipande hicho cha video wananchi wa Shirati mkoani Mara aliko kwa ziara ya kikazi, alipiga marufuku kisitumike popote dhidi ya vyama vya upinzani.
Mbali na hilo, amewaomba viongozi wa dini waendeleze jukumu lao la kujenga mshikamano wa kitaifa na wajiepushe na kauli zinazoigawa nchi.
Alisema chama hicho kiwe cha mfano, akieleza wimbo wa namna hiyo una maneno yanayojenga chuki katika Taifa.
"Hayajengi upendo miongoni mwa Watanzania, lazima zitafutwe nyimbo zinazohamasisha upendo bila kusababisha chuki kwa wengine. Wimbo wa namna hii, mimi kama Katibu Mkuu wa CCM napiga marufuku kutumika dhidi ya upinzani," amesema.
Amesema CCM lazima iwe mfano bora wa kutoa kauli zinazounganisha watu na isiwe chanzo cha uchochezi, vurugu na namna yoyote itakayochochea umwagaji damu.
Dk Nchimbi, ambaye ni mgombea mwenza mteule wa Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, amesema chama hicho kinapaswa kuwa mstari wa mbele kusimamia iliyoyaasisi.
Katika hilo, ametaka iwe rahisi kwa wanachama wa chama hicho kukumbushana kila wakati, hasa pale inapotokea mmoja ametoa kauli inayovunja mshikamano wa kitaifa.
"Iwe rahisi kuwakumbusha wote wanaofanya hivyo ndani ya CCM ili kujenga nchi yenye mshikamano, umoja na si ile inayotafuta damu za watu," amesema.
Dk Nchimbi pia aliwaonya wanasiasa, wakiwamo wa upinzani, akisema wanapaswa kupima maneno yao yasiwe chanzo cha kupandikiza chuki.
Alitaka kuwapo utaratibu wa yeyote anayetoa lugha hatari kwa mshikamano, wafuatwe hata wazazi wake ili wasaidie kumweleza.
Kama inavyopaswa kuwa kwa wanasiasa, Dk Nchimbi ametaka hata viongozi wa dini wajiepushe na mambo yanayoweza kuligawa Taifa.
Amewashukuru viongozi wa dini na kamati za amani kwa kuendelea kutoa mchango katika kuendeleza umoja wa Taifa, akiwasihi waiendeleze kazi hiyo.
Dk Nchimbi amesema katika Mkoa wa Mara chama hicho kina zaidi ya wanachama 450,000 na kwamba, wingi wao hautakuwa na maana iwapo hawataonyesha upendo kwa Taifa.
Katika mkutano huo, alimpigia simu Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, akimtaka aeleze mpango wa Serikali kuhusu ujenzi wa barabara ya Utegi–Shirati.
Hatua hiyo imetokana na ombi la Mbunge wa Rorya, Jaffari Chege, aliyesema ingawa zabuni kwa barabara hiyo imeshatangazwa, muhimu ni kuharakishwa ujenzi wake hapo mkandarasi atakapopatikana.
Dk Nchimbi amepiga simu ya moja kwa moja kwa Ulega kujibu hilo, ambaye amesema tayari kilomita 27 za barabara hiyo zimeshatangazwa, na hadi Aprili 29 atajulikana mkandarasi.
Baada ya hatua hiyo, amesema mkataba utasainiwa na mkandarasi husika tayari kuanza shughuli za ujenzi mara moja kwa kiwango cha lami.
"Baada ya kufungua zabuni kitakachofuata ni kuhakikisha mkandarasi anaanza kazi mara moja," alisema Ulega na kuibua shangwe kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo. Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari, amesema kilichofanywa na Dk Nchimbi ni ithibati ya hekima ya kiuongozi.
Hata hivyo, amesema iwapo wimbo huo na kauli nyingine zingeachwa ziendelee kutolewa na makada wa CCM dhidi ya upinzani, zingekuwa na athari zaidi ya zile mbaya zinazotolewa na upinzani dhidi ya chama tawala.
Hilo linatokana na kile alichoeleza, CCM ndicho chama chenye dola na kinamiliki kila kilichomo nchini, hivyo kina vingi vya kupoteza kwa kujihusisha na siasa za maneno yanayoleta uhasama.
“Marumbano yanaweza kuongeza hasira na chuki, hasa kwa upande wa Serikali. Wapinzani wakiongea kwa hasira, wakati mwingine unaweza kuwaelewa, lakini siyo CCM ambayo inamiliki kila kitu,” ameeleza.
Kilichofanywa na Dk Nchimbi, amesema, kinafanana na ilivyowahi kutokea enzi za utawala wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Alisema katika kipindi hicho, wapinzani walikuwa wakiwafanyia fujo viongozi wa CCM, lakini chama hicho tawala kiliwakataza makada wake kujibu mapigo.
“Wangejibu mapigo, maana yake wanatoa mwanya wa majibizano, hatimaye ingeleta vurugu na mwisho wa siku amani pengine ingevunjika,” amesema.
Alieleza kitendo cha chama tawala kufanya siasa zinazojibu kauli kwa ukali na kuhatarisha mshikamano kama upinzani, ni hatari zaidi, hivyo hatua iliyofanywa na Dk Nchimbi ni muhimu.
Alisema lugha za kuvunja mshikamano na umoja wa kitaifa huzaa chuki, ambayo nayo huzaa vurugu, hatimaye amani kutoweka.
Makaripio ya awali
Akizungumza na viongozi wa UVCCM, Ihemi mkoani Iringa Julai 11, 2024, Dk Nchimbi aliwataka viongozi na wanachama wa CCM kuepuka kutoa kauli za kibaguzi au kufanya vitendo vyenye taswira inayoweza kutafsiriwa kuwa baadhi yao wanashabikia ukandamizaji wa haki za wananchi.
Kauli hiyo ilitokana na video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ikimuonyesha mmoja wa makada wa CCM akitoa kauli zinazoashiria ubaguzi katika kupata haki.
Katika video iliyorushwa mitandaoni Julai 10 na 11, 2024, alionekana kada wa CCM ambaye hakufahamika jina wala eneo, akisema mtu wa CCM akiwa na kesi ni rahisi kupata msamaha, tofauti na Chadema.
"Ukipata tatizo, kesi ya mwana CCM au mwana Chadema ni vitu viwili tofauti, hata iwe polisi au kwa mwenyekiti wa kijiji. Huyu (CCM) anaweza, hebu pisha usirudie moja, mbili na tatu, wewe usirudie kufanya. Lakini tukikujua wewe ni wa… (anaonyesha alama ya vema inayotumiwa na Chadema), tutahangaika na wewe. Eeeh, tukubali hii nchi kwa sasa hivi," alisema kada huyo.
Hata hivyo, Dk Nchimbi alisema: "Niwasisitizie UVCCM, ni muhimu kwa watendaji wetu, viongozi wetu na wanachama wetu kutambua kuwa mnabeba taswira ya chama chetu kila wakati, katika mnayosema au kutenda.
“Kama kuna jambo tunapaswa kulilinda kwa wivu mkubwa ni taswira chanya ya CCM, hasa jambo linalohusu dhamana ya kuongoza nchi yetu na kuwatumikia wananchi kwa haki na usawa, kwa kupinga kauli na vitendo vya ubaguzi na dhuluma kwa Watanzania.”
Aliwataka UVCCM kuwa mstari wa mbele kulinda taswira hiyo muda wote na kujiepusha na kauli au matendo yanayoharibu taswira ya chama hicho tawala.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.