Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sakata la Makonda, Gambo lachukua sura mpya

Muktasari:

  • Makonda amtaka Gambo aombe radhi watu wengine aliodai aliwafitini, kuwachonganisha na kuharibu maisha yao.

Arusha. Sakata la madai ya ubadhirifu wa fedha lililoibuliwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo (CCM), limechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kumtaka awaombe radhi aliodai amewafitini, kuwachonganisha na kuharibu maisha yao.

Aprili 23, 2025, Gambo aliliomba radhi Bunge na kufuta maneno aliyotoa dhidi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa.

Gambo alimtuhumu bungeni Waziri Mchengerwa kwamba amesema uongo wakati akitoa maelezo ya Serikali dhidi ya tuhuma ambazo mbunge huyo aliziibua kuhusu ubadhirifu wa fedha katika ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Tuhuma hizo zilimlazimu Spika, Dk Tulia Ackson kuagiza zichunguzwe na Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Kabla ya utekelezaji wa agizo hilo la Spika, Gambo aliomba radhi bungeni na kuondoa kauli yake.

Katika viwanja vya Kilombero leo Jumamosi, Aprili 26, 2025, wakati wa maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mbele ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, mkuu huyo wa mkoa amesema anampongeza Gambo kwa kuomba msamaha bungeni, ila anamtaka aombe radhi watu wengine aliowafitini, kuwachonganisha na kuharibu maisha yao.

"Amechonganisha chonganisha sana watu hapa na leo ameanza kwa kumsifia mkuu wangu wa wilaya kwa sifa zilezile ambazo alinisifia nilipoteuliwa kuwa RC. Lakini sasa hivi kulitamka jina la Makonda hawezi. Namsifu aliomba radhi kwani alikuwa anakwenda kuharibu maisha ya watu kwa kudanganya.

Kwa kuwa Bunge limemsamehe, mimi moyoni sina shaka naye, lakini sharti langu ni moja: aliowaumiza na kuharibu maisha yao akawaombe radhi ili mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu tupate kibali cha kuifanya kazi hii," amesema Makonda.

Gambo aliibua tuhuma hizo Aprili 16, 2025, akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2025/26 alipohoji gharama za jengo la utawala zisizopungua Sh9 bilioni.

Alidai kuwapo tofauti kubwa kati ya vipimo vya mradi na makadirio ya matumizi ya vifaa (BOQ), akieleza kuna dalili ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Hiyo ilikuwa tofauti na maelezo ya Waziri Mchengerwa aliyekanusha madai hayo akieleza miradi ya maendeleo hupitishwa na vikao maalumu vya mabaraza ya madiwani na alipotoa taarifa kamili ya uchunguzi wa suala hilo alieleza hakuna ubadhirifu wowote.

Tuhuma nyingine ilikuwa ni madai kuwa mapato ya stendi ni Sh800 milioni kwa mwezi, huku Waziri Mchengerwa akijibu ni kwa mwaka.


Gambo mkutanoni

Gambo aliposimama kutoa salamu katika mkutano huo wa hadhara, alimtaja Dk Biteko na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, akiwasifia kwa utendaji kazi na uchapakazi wao.

Pia aliipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (Auwsa) kwa kusimamia miradi ya maji na kutaja changamoto kubwa kuwa ni ankara, changamoto aliyosema ni kubwa na suluhu yake ni mita za kulipa maji kabla ya huduma.

Makonda alivyomvaa Gambo mbele ya waziri

Amesema kutokana na wenye nyumba kutokuwapo wakati wa kusoma mita, ililazimu Auwsa kuweka mita nje ya nyumba na baadhi huibwa na kusababisha hasara kwa wananchi.

Ameipongeza Tarura akisema licha ya kuwa na bajeti ndogo wamejitahidi kufanya maboresho katika baadhi ya barabara ambazo zimekuwa kero kwa wananchi.

Awali, Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Iranghe, amesema katika mkoa huo kulikuwa na migogoro mbalimbali ambayo mingine ilisababisha kukwama kwa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.

"Mzigo mzito mpe Mnyamwezi, Makonda ni Mnyamwezi wetu, amebeba mizigo ya kutosha sana. Alikuja tulikuwa na migogoro ya hapa na pale; kuna miradi ilikuwa inakwama, kulikuwa na tabia ambazo hazieleweki; ushirikina siyo ushirikina, roho mbaya siyo roho mbaya, ilimradi vitu haviendi.

Tunavyoongea hapa shughuli inakimbia. Jengo la utawala ambapo tangu aje lilikuwa kwenye msingi tangu mwaka 2019 kwa sababu ya migogoro ya kisiasa ambayo haina kichwa wala miguu, tunavyoongea jengo liko ghorofa ya tano," amesema.