Prime
MAMBO MATANO MEI MOSI 2025: Mishahara yaendelea kugonga vichwa vya wafanyakazi

Muktasari:
- Mwaka huu maadhimisho ya Mei mosi kitaifa yatanyika mkoani Singida yakiwa na kaulimbiu, Uchaguzi Mkuu 2025, Utuletee Viongozi Wanaojali Haki na Masilahi ya Wafanyakazi, Sote Tushiriki.
Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya kuadhimishwa Siku ya Wafanyakazi Duniani, maarufu Mei mosi, watumishi wa umma na wa sekta binafsi wanatamani kusikia mambo matano kuhusu kuboresha masilahi.
Mambo hayo ni kuongezwa kima cha chini cha mshahara hasa kwa sekta binafsi, kupandishwa kwa viwango vya mishahara, masilahi kwa watumishi wa kazi za ndani, mikataba ya kazi na bima ya afya kwa wanahabari.
Hata hivyo, Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya amesema hawana kitu cha kumwambia Rais isipokuwa wanasubiri aseme jambo kwa kuwa, mengi waliyokuwa wakiyataka yamefanyiwa kazi.
Kwa mwaka huu, maadhimisho ya Mei mosi kitaifa yatanyika mkoani Singida, yakiongozwa na kaulimbiu, Uchaguzi Mkuu 2025, Utuletee Viongozi Wanaojali Haki na Masilahi ya Wafanyakazi, Sote Tushiriki.
Kumekuwa na utamaduni wa muda mrefu kuwa, sherehe za maadhimisho ya Mei mosi kutathmini hali ya haki na usalama wa mahali pa kazi kwa wafanyakazi na kuibua changamoto zinazowakabili.
Kwa miaka kadhaa ya nyuma, maadhimisho hayo yalikuwa yakitumika kutangaza kima kipya cha mshahara au nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma na sekta binafsi, lakini utamaduni huo umeanza kupotea miaka ya hivi karibuni.
Maadhimisho hayo yanafanyika huku kukiwa na kilio kikubwa kutoka kwa wafanyakazi za sekta ya umma na binafsi kuwa kiwango cha mshahara wanachopokea hakilingani na kupanda kwa gharama za maisha kwa sasa.
Kauli ya rais wa Tucta
Nyamhokya ambaye ni rais wa Tucta amesema:“Niseme kuwa, mwaka huu hatuna kilio cha kumfikishia Rais, ila tunajua kuwa yeye ni mama na kiongozi anaweza kuwa na kitu cha kutuambia hivyo tunategemea yeye mwenyewe atuambie.”
Akizungumzia suala la masilahi, amesema bado kuna shida kwa sekta binafsi ambako wanatamani nako kuwe na maboresho, lakini wanashindwa kulazimisha kutokana na kutokuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Kauli ya Tadwu
Katika mahojiano na gazeti hili, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Madereva (Tadwu), Ally Kimaro amesema licha ya mchango mkubwa wa madereva katika maendeleo ya uchumi wa Taifa, bado hawajatambuliwa ipasavyo.
Mwenyekiti huyo amelalamikia kutoshirikishwa kwa karibu katika maandalizi ya maadhimisho ya Mei mosi mwaka huu, licha ya kuwa sekta yao ni miongoni mwa zinazoliingizia Taifa pato kubwa nchini.
“Madereva bado hatuthaminiwi licha ya umuhimu wetu. Tumeendelea kusahaulika hata katika maadhimisho haya ya Mei mosi,” amedai Kimaro.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, amelalamikia kutokuwepo kwa mikataba ya ajira ya kudumu kwa madereva wengi, pamoja na waajiri kutolipa mishahara kwa mujibu wa kiwango cha chini kilichowekwa na Serikali.
“Kiwango cha chini cha mshahara kilichotangazwa ni Sh300,000, lakini wapo madereva wanaolipwa Sh200, 000 tu. Ni waajiri wachache sana ndio hulipa zaidi ya hapo,” amesema mwenyekiti huyo katika mahojiano hayo maalumu.
Hata hivyo, ameishauri Serikali kuingilia kati kwa kuondoa kipengele kinachoruhusu mwajiri na mwajiriwa kupatana kuhusu masilahi yao bila kufuata sheria na badala yake kuwe na mfumo wa kisheria unaowalinda madereva.
Chodawu walia na mkataba
Chama cha Wafanyakazi wa Nyumbani, Hifadhini, Hotelini, Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu), kimeeleza kuwa, kingependa kusikia Serikali ikitamka kupitishwa kwa mkataba namba 189 wa wafanyakazi wa nyumbani.
Mkuu wa Idara ya Sheria wa chama hicho, Asteria Mathias amesema ahadi ya mkataba huo ungepitishwa na Bunge, lakini matumaini ya kufanya hivyo yanafifia hasa ikizingatiwa Bunge linafikia ukomo wake Juni 28, mwaka huu.
Asteria amesema endapo mkataba huo utaridhiwa, utaenda kuwapa hadhi wafanyakazi wa nyumbani na kuweza kufanya kazi za staha tofauti na ilivyo sasa ambako wengi wao hawathaminiki na wengine hupitia manyanyaso.
“Katika haki hizo ni pamoja na kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, haki ya kupata faragha, likizo yenye posho, malipo ya saa za ziada na mapumziko ya wiki na kupandishwa mshahara ili uendane na hali halisi ya maisha,”amesema.
Kulingana na kima cha chini cha mshahara kilichopitishwa mwaka 2022 na kuanza kutumika mwaka 2023, mfanyakazi wa nyumbani anayelala kwa mwajiriwa anapaswa kulipwa Sh60,000 kwa mwezi na anayekwenda na kurudi Sh120,000.
Anayefanya kazi kwa mbunge au mtumishi wa Serikali ambaye malipo yake hujumuishwa na ya mlinzi na mfanyakazi wa ndani, anapaswa kulipwa Sh200,000 na wanaofanya kwa mabalozi na wafanyabiashara wakubwa ni Sh250,000.
CWT na kilio cha malipo ya ziada
Kwa upande wake, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wamesema moja ya jambo zuri wanalotarajia kulisikia siku hiyo ya Mei mosi kutoka serikalini ni kurejeshwa kwa malipo ya ziada kwa walimu yanayofahamika kama Teaching Allowance.
Akizungunza na gazeti hili katika mahojiano maalumu, Rais wa chama hicho, Leah Ulaya amesema fedha za malipo hayo ya ziada zilifutwa kipindi cha uongozi wa Rais Jakaya Kikwete kwa kile ilichodai inataka kuwawekea utaratibu mzuri.
Akifafanua kuhusu kazi zinazopaswa kulipwa kwa ajili ya malipo hayo, Rais huyo amesema ni pamoja na kufanya kazi zaidi muda uliowekwa wa kazi akitolea mfano kuna walimu wanafika shule saa 12:00 asubuhi na kutoka 12:00 jioni.
Pia, fedha hizo ni kwa ajili ya kuwalipa walimu ambao wamekuwa wakifanya kazi ambazo sio majukumu yao ikiwamo kusimamia miradi mbalimbali na ujenzi kwenye shule na wanaoshiriki kutoa mafunzo ya ziada kwa wanafunzi.
Kuhusu suala la masilahi ya walimu, amesema wanashukuru, Serikali ya awamu ya sita imejitahidi kushughulikia kwa kiasi fulani ikiwamo upandishaji madaraja kwa walimu, nauli mambo ambayo huku nyuma ilikuwa kilio chao kikubwa.
Jowuta nao walia na masilahi
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi kwenye Vyombo vya Habari (Jowuta), Musa Juma amesema anachotaka kuona katika maadhimisho hayo ni mailahi ya waandishi wa habari na mazingira bora mahali pa kazi kutazamwa.
Juma amesema waandishi wengi hawana mikataba wala bima, hivyo siku hiyo wanatarajia mamlaka zizungumzie masilahi ya waandishi wa habari.
“Japo Waziri wa Habari (Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo) alishaahidi kukutana na waandishi wa habari kuzungumzia suala hili la masilahi, lakini tunataka liwe kisheria na kwenye maadhimisho pia lizungumziwe,”amesema Juma.
Mwenyekiti huyo amesema anaamini suala la masilahi ya waandishi wa habari kama Serikali itasimamia ipasavyo.
Hata hivyo, amesema changamoto anayoona katika tasnia hiyo ni kwamba hakuna jitihada zinachukuliwa katika kuvisaidia vyombo vya habari na kueleza kuna nchi wamefika hatua hadi ya kuvipa ruzuku kutokana na kutambua umuhimu wake.
Changamoto nyingine amesema ni masharti magumu yaliyopo katika kuviendesha vyombo hivyo ikiwamo mwekezaji kutoka nje kutoruhusiwa kumilika hisa zaidi ya asilimia 49 jambo linawafanya wanaotaka kuja nchini kusita kufanya hivyo.
“Kama Serikali ina nia ya dhati, basi vikwazo kama hivi viondolewe kwa wawekezaji, kwani kwa kufanya hivyo waandishi wengi watapata ajira na serikali itapata kodi,”amesema mwenyekiti huyo.
Kauli ya Cotwu
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (Cotwu), Juliana Mpanduji, amesema wanaamini yanayohusu haki, mazingira ya kazi, masilahi na ustawi Rais Samia Suluhu Hassan atayatolea majibu siku hiyo.
Juliana amesema tamko la Rais huwa ni maelekezo kamili, hivyo wanatarajia kusikia akitoa majibu kuhusu masilahi na haki za wafanyakazi.
“Pia, tunatarajia kusikia kutoka kwa Rais akielekeza anataka nini kwetu kama watoto na wafanyakazi wake, lakini pia masharti mbalimbali ya kisera na kisheria, anaweza kuelekeza vizuri kwa waajiri ambao wanaishi kila siku na wafanyakazi na sisi pia kupata muda wa kujitathimi,”amesema.