Wafanyakazi watakiwa kupaza sauti Mei Mosi

Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar (Zatuc), Khamis Mwinyi Moh'd akizungumza na waandishi wa habari Ofisi kwake, Maisara kuelekea Sherehe za Wafanyakazi. Picha na Zuleikha Fatawi
Muktasari:
- Maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu kwa Zanzibar yanatarajiwa kufanyika Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Dk Hussein Mwinyi.
Unguja. Ikiwa zimebaki siku nne kuadhimishwa siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (Zatuc), limewataka kujitokeza kwa wingi ili kuwa na sauti ya pamoja wakati wakiwasilisha changamoto zao kwa mamlaka.
Katibu mkuu wa shirikisho hilo, Khamis Mwinyi Moh'd ametoa kauli hiyo leo Aprili 26, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari kuelekea siku hiyo.
Bila kuingia kwa ndani mambo wanayotaka kuyawasilisha siku hiyo, Khamis amesema ikiwa wafanyakazi hawatashiriki kikamilifu katika sherehe hizo mamlaka zitaona ni ya wachache.
“Tunaomba wafanyakazi wajitokeze kwa wingi katika sherehe hizi ili yatakayosemwa iwe ni sauti ya wengi, tuonyeshe mshikamano wetu,” amesema.
Katibu huyo amewakumbusha wafanyakazi kudai haki zao kupitia mifumo rasmi iliyowekwa kisheria, kwani baadhi yao hupeleka malalamiko katika maeneo ambayo hayawezi kupatiwa ufumbuzi.
Kutokana na hilo, amesema wanaweza kukosa haki zao au kucheleweshewa, akitoa mfano wa mfanyakazi kupeleka malalamiko yake kwa sheha wa shehia au diwani.
“Kuna muda maalumu umewekwa unapodai kufika katika vyombo vya sheria sasa mtu akianza kupitia kwa sheha muda unakwenda na haki yake inaweza kupotea,” amesema
Mwenyekiti wa Kamati ya Uenezi na Uhamasishaji, Rihi Haji Ali amesema wanaposhiriki kwa wingi katika sherehe hizo ni wazi wanasherehekea upatikanaji wa haki zao.
Katika hatua nyingine, Khamis amewataka wafanyakazi kushiriki katika uchaguzi na kuchagua viongozi ambao watakuwa wanajali masilahi yao.
Amesema wapo baadhi ya viongozi ambao hawajali wafanyakazi lakini wanasahau kuwa bila ya wafanyakazi hakuna maendeleo katika nchi.
"Huwezi kuwa kiongozi bila ya kuwa na mfanyakazi, hivyo viongozi ambao wanapenda wafanyakazi ndio tunaowahitaji,” amesema.