Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu, Jamhuri kuchuana tena leo kesi yake kuendeshwa mtandaoni

Muktasari:

  • Tundu Lissu anakabiliwa na kesi mbili, ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni na ya uhaini. Kesi ya kuchapisha taarifa za uongo imepangwa leo kwa ajili ya Jamhuri kujibu hoja zake za kupinga kesi kuendeshwa kwa njia ya mtandao.

Dar es Salaam. Kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu leo Jumatatu, Aprili 28, 2025 itaendelea kuunguruma, ambapo mawakili wa pande zote wanatarajiwa kuchuana  vikali kwa hoja, kuhusu kuendeshwa kwa njia ya mtandao.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam inayoketi Kisutu, imepangwa leo kwa ajili ya Jamhuri (upande wa mashitaka) kujibu hoja za Lissu na mawakili wake kupinga kesi hiyo kuendeshwa kwa njia ya mtandao.

Lissu alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka yanayomkabili katika kesi hiyo pamoja na kesi nyingine ya uhaini kwa mahakimu wawili tofauti, Aprili 10, 2025.

Upande wa mashitaka uliieleza Mahakama upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na ukaomba Mahakama ipange tarehe kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

Katika hatua hiyo mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali yanayohusiana na mashitaka na kisha hutakiwa kubainisha taarifa zisizobishaniwa (anazokubaliana nazo) na zinazobishaniwa (asizokubaliana nazo), kabla Mahakama kuanza kupokea ushahidi.

Hivyo Mahakama hiyo ilipanga kuendelea na hatua hiyo Aprili 24, 2025.

Hata hivyo siku hiyo haikuendelea katika hatua hiyo baada ya Lissu kugomea utaratibu uliowekwa na Mahakama, kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya mtandao, huku Lissu akiwa mahabusu katika Gereza la Ukonga.

Hii ni aina ya mawasiliano baina ya mtu na mtu au watu na watu walioko maeneo mawili au zaidi tofauti, ambapo  wanaweza kuonana na kuzungumza moja kwa moja kupitia kamera na kompyuta au runinga zilizounganishwa na mtandao wa intaneti, badala ya kukutana uso kwa uso.

Lissu aligoma kwenda katika chumba kinachowezesha mawasiliano hayo katika gereza hilo na badala yake alitaka afikishwe mahakamani kesi yake isikilizwe katika Mahakama ya wazi, na kutoa fursa kwa umma kuifuatilia.

Jopo la mawakili wanaomwakilisha Lissu zaidi ya 31, likiongozwa na Wakili Mpale Mpoki na wengine wakiwemo Dk Rugemeleza Nshala, Peter Kibatala na kaka  yake Lissu, Alute Mughwai, Jeremiah Mtobesya liliunga mkono msimamo huo wa mteja wao.

Mawakili hao pamoja na mambo mengine walidai  utaratibu huo ni kinyume na matakwa ya sheria, kwani katika hatua hiyo ya usikilizwaji wa awali mshtakiwa anapaswa kufikishwa mahakamani.

"Hata kama mshtakiwa angekuwepo mtandaoni, leo tusingeweza kuendelea kwa sababu ingekuwa ni kinyume na sheria, kwani sheria inataka maelezo ya awali yasomwe mshtakiwa mwenyewe akiwepo", alidai Wakili Mpoki.

Wakili Mpoki alifafanua baada ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali anapaswa yeye mwenyewe kusaini nakala ya hoja zinazobishaniwa na zisizobishaniwa.

Kwa mujibu wa Wakili Kibatala, ingawa kuna Kanuni za uendeshaji wa mashauri kielektroniki zinazoruhusu mashauri kuendeshwa kwa njia hiyo, lakini kuna taratibu zake ambazo zinapaswa kuzingatiwa, akidai kwenye kesi hiyo hazikufuatwa.

"Kwa mfano, kanuni zinaelekeza kuwa taarifa inabidi itolewe siku saba kabla ya siku ya shauri, lakini katika hili sisi tulipewa taarifa jana (Jumatano) saa 3 kasoro usiku," alisema wakili Kibatala alipokuwa akizungumza na Mwananchi nje ya Mahakama, baada ya kesi hiyo kuahirishwa.

Baada ya hoja za mawakili wa utetezi, upande wa utetezi, kupitia kiongozi wa jopo la waendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga uliomba upewe muda wa kujibu hoja hizo za upande wa utetezi.

Hakimu Mhini alikubaliana na hoja na maombi ya upande wa mashitaka na akaelekeza  uwasilishe majibu ya hoja za utetezi leo Jumatatu Aprili 28, 2025

Kwa hiyo leo baada ya upande wa mashitaka kujibu hoja hizo, mawakili wa utetezi pia watakuwa na nafasi ya kujibu hoja hizo za majibu ya upande wa mashitaka.


Mashitaka

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashitaka matatu ya kuchapisha mitandaoni taarifa za uongo, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.

Mashitaka hayo yote matatu ni ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube, akidaiwa kuyatenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaa, kwa nia ya kulaghai umma.

Katika shitaka la kwanza maneno aliyoyachapisha Lissu kuwa:

"Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 wagombea wa Chadema walienguliwa' kwa maelekezo ya Rais," wakati akijua maneno hayo ni ya uongo na ya apotosha umma.

Shitaka la pili anadaiwa siku hiyo alichapisha taarifa za uongo na za kupotosha umma kuwa:

"Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibeg."

Katika shitaka la tatu anadaiwa siku hiyohiyo alichapisha taarifa kuwa:

"Majaji ni MA-CCM, hawawezi kutenda haki, wanapenda wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.

Katika mashitaka hayo alipoulizwa na hakimu iwapo ni kweli au si kweli, Lissu hakukana bali alisema maneno hayo si kosa hivyo sio kweli (kwamba ametenda makosa hayo).

Katika kesi hiyo Lissu aliachiwa kwa dhamana baada ya kutekeleza masharti ya dhamana.

Hata hivyo, alilazimika kupelekwa mahabusu anakohifadhiwa mpaka sasa  kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine ya shitaka la uhaini, ambalo halina dhamana.