Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ni huzuni Diamond katoswa tena!

Muktasari:

  • Hii ni mara ya tano mfululizo Diamond anakosekana katika tuzo za BET baada ya hapo awali kupata nafasi ya kuwania mara tatu akiwa ndiye msanii pekee kutoka Tanzania mwenye rekodi hiyo.

Dar es Salaam. Majina ya watakaowania tuzo za BET Awards 2026 yametangazwa ambapo wanamuziki watano kutoka Afrika wamepata nafasi, huku staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz, akiachwa kwa mara nyingine.

Hii ni mara ya tano mfululizo Diamond anakosekana katika tuzo za BET baada ya hapo awali kupata nafasi ya kuwania mara tatu akiwa ndiye msanii pekee kutoka Tanzania mwenye rekodi hiyo.

Diamond, mkali wa kibao cha Komasava (2024), amefanikiwa kuwania mara tatu mwaka ya 2014, 2016 na 2021, lakini mara zote hizo aliondoka mikono mitupu.

Katika tuzo za BET 2026 ambazo zinatarajiwa kutolewa Juni 28 nchini Marekani, Cardi B ndiye ameongoza kwa kuchaguliwa kuwania vipengele vingi, ambavyo ni sita, baada ya kufanya vizuri na albamu yake ya pili, Am I the Drama? (2025).

Kendrick Lamar pamoja na Mariah the Scientist wanafuatia wakipata vipengele vitano kila mmoja, huku Doechii, Doja Cat, Clipse, Teyana Taylor, Olivia Dean na Latto wakipata vinne kwa kila mmoja. Kwa upande wa Afrika, kwa mara nyingine tena wanamuziki kutoka Nigeria na Afrika Kusini wameendelea kupata nafasi katika BET, na hawa ndio wenye rekodi nzuri ya kushinda mara nyingi zaidi kwa muda wote.

Wakati baadhi ya mashabiki nchini wakijiuliza kwanini Diamond hapati tena nafasi hiyo, kuna ukweli mchungu wanapaswa kukubaliana nao kwa wakati huu. Ukweli huo ni kwamba huenda wasifu wake kimuziki umeshuka au hana ushawishi mkubwa katika meza ya uamuzi kimataifa, na hilo linaweza kuwa na athari za moja kwa moja katika kinyang’anyiro cha kupata uteuzi.

Ukitazama wasanii kutoka Afrika waliopata nafasi katika BET 2026, kwa sasa wengi wao wana wasifu mkubwa kimuziki kuliko Diamond. Mathalani, wengi wao wamewahi kushinda tuzo za Grammy Awards!.

Tems kutoka Nigeria ambaye ni mshindi wa Grammy 2024, ametajwa kuwania vipengele vitatu vya BET 2026 ambavyo ni Chaguo la Watazamaji, Msanii Bora wa Kike wa R&B/Pop, na BET Her kupitia wimbo wake First (2025).

Ikumbukwe kipengele cha BET Her hutoa tuzo maalumu kwa nyimbo zinazotia moyo na kuwawezesha wanawake. Kilianza kutolewa mwaka 2006 kikitambulika kama BET J Cool Like That.

Naye mshindi wa Grammy mara mbili kutoka Afrika Kusini, Tyla, katika BET 2026 ametajwa katika vipengele viwili. Video Bora ya Mwaka kupitia wimbo wake Chanel (2025), pamoja na kile cha Chaguo la Watazamaji.

Katika BET Awards 2024 ambapo Tyla aliwania kwa mara ya kwanza, alishinda vipengele viwili ambavyo ni Msanii Bora wa Kimataifa na Msanii Bora Chipukizi kupitia wimbo wake maarufu Water (2023).

Mastaa wa Nigeria, Asake na Wizkid ambaye ni mshindi wa Grammy 2021, wamewekwa kwenye kipengele cha Kundi Bora kutokana na ushirikiano wao wa hivi karibuni.

Mwanamuziki mwingine wa Nigeria, Burna Boy ambaye ni mshindi wa Grammy 2021, anawania kipengele cha Wimbo Bora wa Kushirikiana kupitia kolabo yake na Gunna, wgft (2025).

Utauliza kwani Asake amewahi kushinda Grammy? Ni kweli hajawahi, ila amewahi kuwania. Pia kumbuka katika kipengele alichotajwa katika BET 2026 ni cha Kundi Bora ambapo yupo na Wizkid.

Ikumbukwe Wizkid na Burna Boy ndio wasanii vinara Afrika kushinda tuzo nyingi za BET, wote wakiwa na tuzo nne, ingawa Wizkid kuna moja aliishinda kupitia kolabo na Beyonce, Brown Skin Girl (2019).

Mwaka 2010, ndipo BET walipoanza kujumuisha wasanii kutoka Afrika katika tuzo zao kupitia kipengele cha Best International Act; Africa.

Hata hivyo, mwaka 2018 kipengele hicho kilifanyiwa mabadiliko na kuwa Best International Act kikihusisha wasanii wote kutoka nje ya Marekani, lakini kwa msimu huu kipengele hicho hakipo na badala yake wametambulisha vipya viwili.

Msimu uliopita aliyeshinda kipe ngele hicho ni Ayra Starr baada ya kuwabwaga washi ndani wake kama Any Gabrielly, Bas hy, Black Sherif, Joe Dwet File, Rema, Tyla na wengine.

Kwa upande mwingine, hadi sasa mwanachama wa zamani wa Destiny’s Child, Beyonce ndiye msanii aliyeshinda tuzo nyingi zaidi za BET kwa muda wote akiwa na 36. Ikumbukwe tuzo hizo zinazoandaliwa na BET nchini Marekani tangu Juni 2001, zinalenga kusherehekea mafanikio ya wasanii weusi katika muziki, uigizaji, michezo na kadhalika.