Diamond afanya maajabu tena

Muktasari:
- Diamond amefikisha subscribers hao huku akiwa na zaidi ya watazamaji zaidi ya bilioni mbili kutoka kwenye video 1,075 alizopandisha katika mtandao huo.
Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz ameweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza na wapekee ukanda wa Jangwa la Sahara kufikisha subscribers milioni 10 kwenye mtandao wa YouTube.
Diamond amefikisha subscribers hao huku akiwa na zaidi ya watazamaji zaidi ya bilioni mbili kutoka kwenye video 1,075 alizopandisha katika mtandao huo.

Diamond alifungua rasmi ukurasa huo wa YouTube Juni 12, 2011. Na kuanza kuutumia mtandao huo kibiashara ikiwa kama moja ya sehemu zake kubwa za kupatia kipato na umaarufu kutokana na nyimbo, shoo, na mtindo wake wa maisha.
Aidha mwaka 2020, Diamond alitajwa kama msanii ambaye anaongoza kuwa na watazamaji wengi Afrika kupitia mtandao huo. Ambapo aliweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kufikisha watazamaji bilioni 1 huku akiwazidi wasanii wengine kama Burna Boy, Davido, Wizkidayo Tekno Nairamarley na wengine.
Diamond anakuwa mbele yao tena kwa wafuasi wengi wa YouTube akiwapiku wasanii kama Rema, Davido, Asake, Harmonize, Rayvanny, Wizkid na wengine wengi.
Utakumbuka Diamond alitoka na wimbo, Kamwambie (2009) uliomfanya kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2010 kama Msanii Bora Chipukizi na hadi sasa ameshashinda tuzo hizo 22 akiwa ndiye msanii aliyeshinda mara nyingi zaidi.

Na huyu ndiye msanii Bongo aliyefanya vizuri zaidi YouTube 2024 ambapo ametazamwa (views) zaidi ya mara milioni 440 akifuatiwa na Rayvanny mwenye milioni 182 ambaye namba zake hata ukizizidisha mara mbili bado hamfikii Diamond.
Diamond, mshindi wa tuzo nane za AEAUSA Marekani, ndiye msanii pekee Afrika Mashariki mwenye video nyingi zilizotazamwa YouTube zaidi mara milioni 100, anazo tano ambazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Jeje (2020) na Nana (2015).