Prime
Hiki hapa ‘kichinjio’ kwa watia nia CCM

Moshi. Ni kama vile wana kiburi na jeuri fulani, kwamba viongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wameonya juu ya kampeni za mapema zinazofanywa na wale wanaowania ubunge na udiwani 2025, lakini ni kama sikio la kufa.
Huko kwenye majimbo na kata katika mikoa mbalimbali nchini, kuna moto unawaka ama chini kwa chini au waziwazi kutokana na wingi wa makada walioanza kampeni mapema, licha ya maonyo ya viongozi wa juu wa CCM.
Unaweza kuwafananisha baadhi ya makada wanaowania ubunge na udiwani kama mnyama wa mwituni anayefahamika kama nyumbu, kwamba anaona kabisa mwenzake aliyeingia mtoni analiwa na mamba, lakini na yeye anaingia.

Wafuasi wa CCM wakiwa katika mkutano mkuu jijini Dodoma .Picha Maktaba
Lakini wasichokifahamu ni kuwa kanuni ya 25 ya Kanuni za Uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya Dola toleo la 2021 inayopatikana katika kijitabu cha Kanuni kuanzia ukurasa wa 57 hadi 59, inakwenda kuwa kitanzi kwao.
Hii ni kwa sababu matendo yanayoendelea katika baadhi ya kata na majimbo ya uchaguzi nchini yanakiuka kanuni hiyo na inasema wazi mwanachama anayeomba kugombea nafasi hizo na akakiuka miiko hiyo, hatateuliwa kugombea nafasi hiyo.
Lakini haikuishia hapo, Kanuni hiyo inawabana pia viongozi wa chama hicho tawala, kwamba kiongozi yeyote, ambaye baada ya kuchaguliwa, atathibitika kuvunja miiko hiyo naye rungu ni lilelile, atavuliwa uongozi wake ndani ya chama.
Huko majimboni sasa hivi kuna pilikapilika nyingi, zinazoonekana na zisizoonekana, huku baadhi walioonyesha nia lakini hawajajitangaza, wamekuwa wakijipitisha pitisha na kugawa zawadi na rushwa kwa baadhi ya wajumbe na viongozi.
Wengine wanatumia udini na kuwa safari hii ni zamu ya muumini wa dini fulani kuwa mbunge au diwani, lakini wengine wameenda mbali na kuanza kupakana matope na kuchafuana kwa kuanzisha makundi ya Whatsapp kwa lengo hilo.
Lakini wengine wanajipitisha huku wakidai kuwa ama wametumwa na Rais Samia au Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa au kiongozi mwingine wa juu ndani ya Serikali na CCM, kugombea wakati hakuna kitu kama hicho, bali kuwaghilibu wajumbe.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais Samia Suluhu Hassan akiongoza kikao cha Kamati Kuu ya CCM leo Machi 10, 2025 jijini Dodoma.
Kuna baadhi ya viongozi wa kata, wilaya na hata mkoa wa CCM ambao wameonyesha dhahiri kuwa na wagombea mifukoni au kuwabeba baadhi ya watiania ama kutokana na uswahiba, rushwa au upendeleo na kujuana.
Kuna vikao visivyo rasmi huko kwenye majimbo na kata vikihusisha baadhi ya viongozi wa CCM, watia nia na idadi kubwa ya wapigakura katika kura za maoni, lengo likiwa moja tu, kutengeneza mtandao wa ushindi kwa mtia nia.
Licha ya maonyo na makaripio ya viongozi wakuu wa chama hicho, akiwamo mwenyekiti, Rais Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu, Balozi Emmanuel Nchimbi na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala, hali ni kama jana na juzi.
Baadhi ya watia nia wameshupaza shingo, hawataki kusikia la mkuu na mwisho kanuni ya 25 inakwenda kuwavunja miguu, kwa sababu kinachofanyika hivi sasa majimboni ni vurugu na kuwanyima usingizi wabunge na madiwani waliopo.
Kanuni ya 25 inasemaje
Kanuni ya 25 ambayo inakwenda kuwa kitanzi cha makada wengi walioonyesha nia na kuleta vurugu kwenye kata na majimbo, ndiyo inasimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya Dola.
Kwa mujibu wa Kanuni ndogo ya (1), ni mwiko kwa kiongozo yeyote, kwa maneno au vitendo, kumpendelea au kumsaidia mwombaji mmoja, kupata kura nyingi dhidi ya mwingine miongoni mwa wale waliorudisha fomu.
Kanuni ndogo ya (2) inasema ni mwiko kabisa kwa mgombea kutumia au kuhusisha ukabila, dini, rushwa, rangi au eneo analoishi au analotoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi kupigia kura za maoni ndani ya CCM
“Ni mwiko kwa mgombea yeyote kufanya kampeni za kupakana matope, au ya aina nyingine yoyote ile dhidi ya mgombea mwingine,” zinasema kanuni hizo.
Ukisoma kanuni ndogo ya (4) inasema: “Ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mwombaji yeyote wa nafasi ya uongozi au mwanachama aliyekabidhiwa dhamana ya kusimamia kura za maoni, uchujaji na uteuzi kukiuka kanuni, Katiba na sheria.”

Kanuni ndogo ya (5) inasema ni marufuku kwa mwanachama anayetarajia kugombea au wakala wake kufanya vitendo vyovyote vinavyoonekana dhahiri ni sehemu ya kampeni za kuwania nafasi anayoitafuta kabla ya muda rasmi.
“Ni marufuku kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake, kutoa misaada mbalimbali wakati uchaguzi unapokaribia, ambayo dhahiri ina lengo la kuvutia kura,” inasema Kanuni ndogo ya (6) ya kanuni hizo.
Hata hivyo, kanuni hiyo inasema hao wanakatazwa isipokuwa kanuni hiyo haitamhusu Rais, mbunge au diwani ambaye yuko madarakani wakati huo, kwa kuwa bado anao wajibu wa kuhudumia wananchi katika eneo lake la uongozi.
Kwa hiyo, kuna adhabu ya kuvunja kanuni hii ambapo inapatikana kwenye Kanuni ndogo ya (7) (a) na (b) ambapo kwa atakayethibitika kuzikiuka atavuliwa uongozi na mgombea atakayethibitika kuzivunja hatateuliwa kugombea nafasi anayowania.
Msimamo wa Rais Samia
Januari 18, 2025 akiwa Jijini Dodoma akiongoza mkutano mkuu Maalumu wa CCM, Rais Samia alisema wapo makada wa CCM ambao wameanza kampeni mapema na kusisitiza kuwa masuala ya kampeni za mapema chama kinazikemea vikali.
“Masuala ya kampeni za mapema na hapa ni kuwaasa wale wanaojipanga kugombea. Masuala ya kampeni za mapema tumeshapata malalamiko na ushahidi wa picha,” alisema Rais Samia, akiwalenga waonyesha nia ubunge na udiwani.
“Nina ushahidi wa picha za watu wanaofanya misafara kwenda majimboni, watu wanaoitisha mikutano mikuu ya majimbo kwa kisingizio cha ufugaji au mambo mengine, lakini dhamira yao ni kujitambulisha kwa wanachama,” alisema Rais.
“Tuna ushahidi wa picha nyingi sana. Sasa tunaona tutoe onyo mapema,” alisisitiza mwenyekiti huyo wa CCM na kusema chama kinafahamu katika uchaguzi wa ndani wa chama kunakuwa na makundi, akataka baada ya mgombea kupatikana yavunjwe.
Kauli kali ya Nchimbi, Makala
Si Rais Samia pekee ambaye amekemea kile kinachoendelea kwenye majimbo na kata, bali hata Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Nchimbi naye akiwa Jijini Dodoma Februari 19, 2025 aliwaonya walioanza kampeni mapema kuwa wataenguliwa.

Nchimbi alitoa karipio hilo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makatibu wa Matawi na Kata kutoka Wilaya ya Dodoma, ambapo alisema wapo makada wa CCM walioanza kampeni majimboni na kwenye kata wakitumia mbinu mbalimbali.
Katibu mkuu huyo alisema wapo walioanzisha mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO) zinazozunguka majimboni, kufadhili matukio ya kijamii kama harusi, sherehe za ndoa na kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa, lakini malengo ni uchaguzi 2025.
“Baadhi ya wabunge wanapitisha fomu ili wanachama wajiorodheshe ili waunge mkono wao kupita bila kupingwa. Hicho kitu hakipo. Wanachofanya ni kutulazimisha kuwaengua mapema. Waache mara moja,” alisema Balozi Nchimbi.
Balozi Nchimbi alifichua kuwa wapo baadhi ya wabunge na watia nia wanaandaa kumbukumbu ya kifo cha mama yake anaalika watu 3,000 au kumbukumbu ya kuzaliwa anaalika watu 900, wote wamevaa sare na wanalipwa posho.
“CCM ina mfumo makini wa kufuatilia kila kinachotokea huko (majimboni na kwenye kata) na tunachukua kumbukumbu ambazo ndizo tutazitumia kuwaengua. Kwa hiyo wakienguliwa wasijiulize hii imetokea wapi,” alisisitiza Balozi Nchimbi.
“Natuma salamu kwa makatibu wa matawi, natuma salamu kwa makatibu wa Kata, natuma salamu kwa makatibu wa wilaya na mikoa na nawakumbusha kuwa wao ni wakurugenzi wa uchaguzi katika maeneo yao,” alisema Balozi Nchimbi.
“Sifa kuu ya mkurugenzi wa uchaguzi ni kutokuwa na upande, ni kutopendelea upande wowote na kusimamia Kanuni na Katiba. Tunapoelekea kwenye uchaguzi, kupuuza Kanuni na Katiba ya CCM ni kosa kubwa,” alisisitiza Balozi Nchimbi.
Katibu wa Itikadi, Mafunzo na Uenezi, Amos Makala naye hakuwa mbali na kile ambacho Rais Samia na Balozi Nchimbi walikionya, kwani naye alisema chama hicho kinafuatilia kwa ukaribu wale wanaotajwa kuanza kampeni mapema.

“Tuwape nafasi waliochaguliwa wafanye kazi zao hadi muda sahihi utakapofika. Msidhani chama kipo kimya, nyendo zako zinaratibiwa, kumbukumbu zako zitawekwa kwamba wewe umeanza kampeni mapema,” alisema Makala.
Kauli za wabunge
Jimbo la Moshi Mjini linaloongozwa na mbunge wake, Priscus Tarimo ni moja ya majimbo nchini yenye pukurushani nyingi za makada wanaosaka ubunge na baadhi yao walishaitwa na kuhojiwa katika vikao vya maadili vya CCM.
Alipotafutwa na Mwananchi, Tarimo, anayemaliza kipindi chake cha ubunge 2020-2025, alisema hali ya kisiasa katika jimbo lake ni shwari isipokuwa wapo makada (hakuwataja) wanavunja kanuni na kufanya kampeni kabla ya muda.
“Hali ya kisiasa kama hali ya kisiasa ni shwari isipokuwa wapo watu (makada) wanaovunja kanuni wazi wazi, lakini mamlaka zinashindwa kuchukua hatua stahiki. Wengine wanaenda mbali na kudai wametumwa na viongozi wa juu,” alisema.

Tarimo alitolea mfano wa kada mmoja ambaye katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwamo misiba, amekuwa akijitangaza ndiye mbunge wa Moshi mjini 2025 na wakati mwingine akionyesha mawasiliano ya simu na watu aliodai ni wazito.
Hali hiyo ya Jimbo la Moshi mjini, pengine ndiyo inatokea katika majimbo mengi nchini na wabunge kadhaa wameshasikika wakijitokeza hadharani kulalamikia kuwa harakati hizo zinawafanya washindwe kujikita kutimiza majukumu yao.
Machi 14 2025, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Temeke ilitoa taarifa kwa wanahabari kuwa ilikuwa imemkamata mmoja wa makada wa CCM kwa tuhuma za kuandaa mkutano ili kutoa rushwa.
Kwa hiyo, kwa kuwa Rais Samia ameonya, Balozi Nchimbi ameonya, Makala ameonya na Takukuru imeonya, huu si wakati tena wa maneno maneno, CCM na vyombo vya Dola vishirikiane kudhibiti kinachoendelea majimboni na kata.