Prime
Katibu wa Chadema Kilimanjaro asimamishwa, mwenyewe aeleza mwanzo mwisho

Moshi. Mambo yanazidi kuchemka, ndivyo unaweza kuelezea kile kinachoendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya chama hicho kumsimamisha Katibu wake wa mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema.
Alipotafutwa usiku huu saa 2:39 Mei 7, 2025 ili kuthibitisha kama barua inayosambaa mitandaoni imetoka katika ofisi yake, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Ndonde Totinan, amesema ni ya kweli na anaifahamu vizuri.
“Ni kweli. Ofisi yangu imepokea tuhuma kuhusiana na makosa mbalimbali ya kimaadili lakini sasa ili kutendea haki pande zote, tumeona tumsimamishe kwa nafasi yake ili kuleta uhuru wa uchunguzi wa hilo jambo”amesema Totinan.
“Kwa hiyo ina maana uchunguzi ukikamilika basi kama atakutwa na hatia hatua za kinidhamu zitachukuliwa, ikionekana hana hatia basi atarudi kwenye nafasi yake kwa sababu aliteuliwa hiyo nafasi kwa kipindi cha miaka mitano”
“Imefanyika tu kwa lengo la kupisha uchunguzi dhidi ya madai hayo,”amesisitiza.
Lema anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi waliohudumu kwa muda mrefu katika wadhifa huo, akihudumu kuanzia mwaka 2009 na chini ya uongozi wake, chama hicho kilifanya vizuri mkoani humo uchaguzi mkuu 2010 na 2015.
Katika uchaguzi mkuu mwaka 2010 wakati Philemon Ndesamburo (marehemu) akiwa mwenyekiti na Lema Katibu wake, Chadema ilifanikiwa kunyakua majimbo matatu ya Moshi mjini, Rombo, Hai na kuongoza Halmashauri za wilaya mbili.
Uchaguzi mkuu wa 2015, Lema na Ndesamburo chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliwezesha umoja huo kunyakua majimbo saba kati ya tisa na kuongoza halmashauri tano kati ya saba za Mkoa wa Kilimanjaro.
Taarifa ya kusimamishwa kwake ilianza kusambaa katika makundi ya WhatsApp, mengi yakiwa yana wanachama wengi wa Chadema saa 2:40 usiku, ingawa taarifa hiyo kwa umma haikuwa imemtaja katibu huyo kwa jina bali cheo chake.
Lema alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia suala hilo, amesema na yeye ameiona tu kwenye mitandao, hajatafutwa na kiongozi yoyote wala kuitwa kuhojiwa.
“Mamlaka ya nidhamu ya Katibu wa mkoa ni kwenye kamati ya maadili ya Kanda, ambayo ndio ilistahili kukaa na kusikiliza shauri hilo kwa mujibu wa kanuni za chama. Hiki kilichofanyika ni kinyume kabisa na Katiba na maadili ya chama”
“Haya ni matokeo ya kujengwa kwa chuki kubwa ndani ya chama badala ya kuwaleta wanachama pamoja na kuhimiza upendo, umoja na mshikamano. Kwa kweli haya mambo hayana afya, kabla ya kutoa uamuzi niite kwanza unisikilize,”amesema Lema.
Taarifa ya kusimamishwa
Taarifa ya kusimamishwa kwake iliyotiwa saini na Ndonde Totinan ambaye ni Katibu wa Kanda ya Kaskazini wa Chadema, imedai kusimamishwa kwake ni kutokana na mwenendo usioridhisha wa kimaadili na kinidhamu.
“Hii imetokana na mwenendo usioridhisha wa kimaadili na nidhamu kwa kushawishi viongozi wa majimbo kujiondoa Chadema na kuhudhuria kikao siku ya Alhamisi Moshi mjini kujiunga na chama kingine,”imeeleza taarifa hiyo.
“Aidha shauri lake limepelekwa katika kamati ya maadili ya Kanda kwa mujibu wa Mwongozo wa Maadili ya Chama Kanuni ya 8(b)(ii) wa mwaka 2019,”inasema.
“Kwa kuwa nafasi ya ukatibu wa mkoa ni ngazi ya uteuzi wa kamati tendaji ya Kanda, na kwa mujibu wa Ibara ya 6.3.5(b) nafasi ya uteuzi itakayokuwa wazi itazibwa na mamlaka husika, nafasi hiyo itazibwa kamati itakapotoa maelekezo”
Kusimamishwa kwa Lema kumekuja saa chache tangu waliokuwa manaibu makatibu wakuu wawili wakati wa uongozi wa Freeman Mbowe, Benson Kigaila na Salum Mwalimu kutangaza kujivua uanachama wa Chadema leo Mei 7, 2025.
Wengine waliojiondoa ni Catherine Ruge aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na aliyekuwa mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano ya Mambo ya Nje, John Mrema wanaounda kundi la G55.