Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

AY kuanzia kwa Lady Jaydee, Mis. Triniti hadi Mimi Mars

Muktasari:

  • Akiwa ametoa albamu tatu, Raha Kamili (2003), Hisia Zangu (2005) na Habari Ndio Hiyo (2008), umaarufu wa kazi zake umempa AY majina mengine kama Mzee wa Commercial, Zee, The Butcher n.k.

Dar es Salaam. Hadi sasa AY ni kati ya wasanii walioacha alama katika Bongofleva, muziki alioutumikia kwa miaka zaidi ya 20 na kufungua milango ya kuupeleka kimataifa kwa kushirikiana na wasanii wakubwa.

Akiwa ametoa albamu tatu, Raha Kamili (2003), Hisia Zangu (2005) na Habari Ndio Hiyo (2008), umaarufu wa kazi zake umempa AY majina mengine kama Mzee wa Commercial, Zee, The Butcher n.k.

Rapa huyu aliyeshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) na zile za kimataifa kama Pearl of Africa Music (Uganda), Kisima (Kenya) na Channel O (Afrika Kusini), ameshirikiana na wasanii wengi ila kuna la kujifunza kwake katika eneo hilo, nalo ni jinsi alivyowapa wasanii wa kike nafasi kubwa katika muziki wake, kuanzia Lady Jaydee, Amani, Vanessa Mdee, Mis. Triniti hadi Mimi Mars.


1. Lady Jaydee & AY - 2003

Miongoni mwa nyimbo za mwanzo kabisa za AY kurekodiwa Bongo Records kwa P-Funk Majani ni pamoja na ‘Machoni Kama Watu’ akimshirikisha Lady Jayde, wimbo huo ulikuja baada ya kuamua kufanya kazi kama solo akitokea kundi la S.O.G.

Ni wimbo uliojumuishwa katika albamu ya kwanza ya AY, Raha Kamili (2003), unaambiwa aliurekodi bure kutokana na urafiki wake na Majani. Baadaye AY na Lady Jaydee walikutana tena katika wimbo wa TID, Sifai (2011) uliotengenezwa na Lamar wa Fish Crab.

2. Ray C & AY - 2003

Katika albamu ya Raha Kamili (2003), kulikuwa na wimbo unaoitwa ‘Safi Hiyo’ uliotengenezwa na Xosa kutoka Backyard Records, huu AY aliwashirikisha Mwana FA, Banana Zorro na Ray C. Mwaka huo ndipo Ray C alitoa albamu yake ya kwanza, Mapenzi Yangu (2003), na mwaka uliofuata akashinda tuzo yake ya kwanza ya TMA kama Msanii Bora wa Kike, hivyo AY, mwanachama wa zamani wa East Coast Team hakukosea kumpa kolabo hiyo.


3. Amani, Jokate & AY - 2010

Ukiachilia mbali mambo mengine yaliyokuwa yanazungumzwa baina ya AY na Amani kutokea Kenya walikuwa na muunganiko mzuri wa kikazi, Amani ndiye alianza kufanya kazi na AY katika wimbo wake ‘Usiwe Mbali’ chini ya Ogopa Deejays. Baadaye AY naye akampa shavu Amani na Jokate katika ngoma yake, Kings & Queens (2010) iliyotengenezwa B’Hits na Hermy B na video yake walifanya Ogopa Deejays kutoka Kenya, vilevile Jokate alikuja kusikika katika ngoma nyingine ya AY, El Chapo.


4. Avril, Wahu & AY - 2010

Je, unamkumbuka Avril wa Kenya aliyetamba katika wimbo ‘Chokoza’ na baadaye kuonekana kwenye video ya wimbo wa Diamond Platnumz, Kesho?, basi huyu alishirikishwa na AY katika wimbo wake, Leo Remix (2010). Ni wimbo ulioshinda tuzo ya TMA 2010 kama Wimbo Bora wa Reggae, huku remix nyingine ya wimbo huo AY akimpa shavu Wahu, mke wa mwanamuziki wa Kenya, Nameless ambaye walifunga ndoa Septemba 2005 na hadi sasa wapo pamoja.


5. La’Myia & AY - 2011

Mwimbaji wa Marekani, La’Myia kutoka kundi la R&B la Isyss, alishirikishwa na AY katika wimbo wake, Speak With Ya Body (2011) pamoja na Romeo, La’Myia akaja kusikika tena katika ngoma nyingine ya AY, It’s Going Down. Ikumbukwe La’Myia ndiye ameingiza sauti katika mchezo wa PlayStation 3 wa Killzone 3 kama Jammer, huku akionekana katika vipindi vingi vya televisheni.


6. Vanessa Mdee & AY - 2012

Wakati huo akiwa bado mtangazaji wa Choice FM, ndipo Vanessa Mdee alikutana na AY aliyemshirikisha katika wimbo wake, Money (2012) na huo ukawa mwanzo wa kufanya vizuri kisha kuja kuvuma zaidi kupitia kolabo ya Ommy Dimpoz, Me N You (2013).
Baadaye Vanessa akaja kusainiwa Bxtra Records, zamani B’Hits, ndipo akatoka na wimbo wake, Closer (2013) ulioshinda TMA kama Wimbo Bora wa RnB 2014. Hadi anaacha muziki alikuwa ametoa albamu moja, Money Mondays (2018) chini ya Mdee Music.


7. Mis. Triniti & AY -  2014

Mwimbaji Mis. Triniti wa Uingereza na Marekani pengine ndiye msanii wa kike wa kimataifa aliyeshirikishwa zaidi na AY, amesikika katika nyimbo zake tatu, Good Look (2011) na It’s Going Down (2014) akiwa pamoja na La’Myia. Pia Mis. Triniti amesikika katika wimbo wa AY, Touch Me Touch Me (2014) pamoja na Sean Kingston wa Jamaica, wimbo huu na ule wa ‘It’s Going Down’, zote zimetengenezwa na Riley aliyefanya kazi na Meek Mill, Lady Ganga, Tyga, Kanye West, Beyonce n.k.  


8. Victoria Kimani & AY - 2019

Staa wa Kenya, Victoria Kimani amepewa nafasi katika ngoma ya AY, Love You More (2019) chini ya 02 Beatz, na ikumbukwe kipindi AY anamsimamia Stereo chini ya Unity Entertainment, Victoria pia alisikika katika wimbo wa Stereo, Never Let You Down (2014).  Utakumbuka Victoria Kimani alikuwa msanii wa kwanza wa kike kusainiwa na lebo kubwa Nigeria, Chocolate City mnamo 2012, huku akishirikiana na wasanii wengine wa Afrika kama Tekno, Arielle T, Yemi Alade, Sarkodie, Ice Prince, Phyno, Vanessa, Diamond n.k.


9. Mimi Mars & AY - 2021

Baada ya kuzunguka sana huko nje, AY akaamua kurudi nyumbani na kutua kwa Staa wa Bongofleva kutokea Mdee Music, Mimi Mars ambaye kapewa shavu katika wimbo, Stakaba (2021), uliotengenezwa na Daxo Chali wa MJ Records.
Mimi Mars alitoka kimuziki na wimbo wake, Sugar (2017) uliotengenezwa studio kwa Barnaba, High Table Sound, na tayari ametoa EP mbili, The Road (2018) na Christmas with Mimi Mars (2021).