AY afunguka namna ya kugeuza nyimbo za zamani kuwa ‘hit songs’

Ubunifu zaidi na ubora wa hali ya juu unahitajika Ili kuzifanya nyimbo za zamani ziweze kusikilizwa tena zikiwa na ladha mpya ikiwamo kufanya remix na ubora wa hali ya juu, sio kitu rahisi kufanya wimbo wa zamani uka-vibe tena masikioni mwa watu hasa kwa wakati huu ambapo muziki umeenda mbali kila aina ya midundo na ala za muziki zinazidi kuongezeka na kukua kila kukicha.

Katika kulizungumzia hilo Mwananchi imezungumza na mwanamuziki mkongwe wa Bongo Fleva, Ambwene Yessayah maarufu kama A.Y ambaye amehudumia vyema kiwanda cha Hip Hop ambapo mpaka sasa bado anakimbiza kwenye muziki, amefunguka kuhusu kufanya remix ya nyimbo za zamani kuzileta katika usasa, akidai kuwa remix inahitaji ubunifu sana na ndiyo maana wasanii wengi wakongwe wanaogopa kufanya.

“Tabia ya remix wasanii wengi wanaogopa sana kwa sababu ya kuhofika kuharibu classic zao, remix ni kujitofautisha kati ya ule ubora uliyokuwa nao na kuweka katika upande mwingine,” amesema.

Hata hivyo, ameelezea kuwa msanii akitaka kufanya remix kuna vitu vya kuvizingatia na kuviangalia ikiwemo aina ya mwanamuziki unayetaka kuimba naye.

“Msanii akitaka kufanya remix kuna vitu anatakiwa aangalie kama aina ya mwanamuziki anayetaka kuimba naye, Producer gani anaweza kutengeneza remix yako, na nani anaweza kuweka ‘base’  je unaimba naye sauti ikoje, Melody zake, uandishi wake unaenda n akitu ambacho unataka kufanya naye na sema hivyo kwa sababu nimeshaona watu wengi wanafanya remix alafu zinakuja ku-slop,” amesema A.Y.


Mambo anayozingatia anapofanya kazi na wasanii wadogo?

A.Y. amefunguka vitu ambavyo anavizingatia katika kufanya kazi na wasanii wa kizazi kipya ambapo amedai kuwa si kila msanii anaweza kufanya kazi naye.

“Wasanii wengi wanaona kila kitu wanaweza kufanya wakati haiwezekani na si kila msanii anaweza kufanya naye kazi awe mdogo au mkubwa kwa sababu muziki sio kwenda na beats au kuweka melody juu ya wimbo, je tone yako inaendana na beats unayotaka kufanya,” amesema.

Aliamini ‘Kombinesheni’ yake na Marioo watafanya kitu kizuri

Ni kama mafahari wawili walikutana katika zizi moja kuwapa burudani mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva hayo anayathibitisha A.Y. baada ya kufanya remix ya wimbo wa ‘Yule’ uliotoka wiki mbili zilizopita ambapo amedai kuwa aliamini kuwa akifanya kazi na Marioo itakuwa nzuri.

“Bhana dude la Remix ya ‘Yule’ linafanya vizuri na tuko mbioni kutoa video yake  kwa sababu niliamini nikifanya combination na Marioo itakuwa nzuri na ndiyo ilivyokuwa, pia mimi napenda kufanya kazi na mtu anayeichukulia kazi yangu kama yake na mimi nachukulia yake kama yangu.”


Afunguka mipango mengine ya kufanya kazi na Marioo

Mbali na hayo mwanamuziki huyo amefunguka mipango yake ya kupiga kazi zaidi na Marioo ameeleza yuko tayari kufanya naye kazi siku za usoni kwa sababu huwa anasikiliza kazi zake nyingi.

“Ikitokea kufanya kazi na Marioo huko siku za mbele hakuna shida nitafanya kwa sababu kuna kazi zake nyingi huwa nazisikiliza na siyo yeye tu hata wasanii wengine pia nasikiliza kazi zao kwa hiyo nikisikiliza kitu naenda nacho basi tunaweza tukafanya,” amesema.


Nafasi yake kwa mashabiki wa sasa katika Bongo Fleva

Kama inavyofahamika muziki wa sasa ni kujichanganya na kuangalia mashabiki nini wanachopenda kwa sasa kwa A.Y, licha ya kuwa mkongwe katika muziki ameeleza kuwa yeye ataendana na mdundo kwa sababu anaimba na anafanya Hip-Hop hivyo anaweza kuingia katika aina yoyote ya muziki.

“Mimi sina shida kwa sababu naimba na kurap hivyo naweza kuwa ‘flexible’ kwenye aina yoyote ya muziki wa kisasa na ndiyo kitu ambacho Mungu amenijaalia kwa hiyo naweza kufanya vyote kwenye muziki na ndiyo maana kila rika inapenda muziki wa tofauti.

Pia ameelezea kuwa kuna watu wanapenda nyimbo zake za international na ndiyo maana anapopanda jukwaani ni kawaida kuchukua hata masaa mawili ili kila mtu afurahie ladha yake ya muziki anaoutaka kwa muda huo kwa sababu kila kitu yeye anafanya.

Utakumbuka A.Y. amewahi kufanya Remix na Diamond Platnumz wimbo wa ‘Zigo’,  remix ya ‘Leo’ na Avril kutoka Kenya, remix ya Distance aliyomshirikisha mwanamziki kutoka Zambia Jay Rox, na Rayvanny.