Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Albam mpya ya Marioo 'The God Son' na tumaini jipya

Muktasari:

  • Hili ni jaribio jingine la Marioo baada ya albamu yake ya kwanza, The Kid You Know (2022) kushindwa kunyakua TMA 2022 kitu kilichomfanya kulalamika kuwa amehujumiwa maana alistahili ushindi kwa asilimia 100.

Mwimbaji  wa Bongofleva, Marioo ameachia albamu yake ya pili, The God Son (2024) ikiwa na nyimbo 17, ahadi yake aliyoitoa katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 ni kwamba mradi huo utashinda tuzo msimu ujao wa 2024.

Hili ni jaribio jingine la Marioo baada ya albamu yake ya kwanza, The Kid You Know (2022) kushindwa kunyakua TMA 2022 kitu kilichomfanya kulalamika kuwa amehujumiwa maana alistahili ushindi kwa asilimia 100.

Albamu hii mpya ya Marioo imeshirikisha wasanii kama Alikiba, Harmonize, Stans na Aslay, wengine wa kimataifa ni Bien na Kenny Sol wa Kenya, Joshua Baraka wa Uganda, Patoranking wa Nigeria na King Promise wa Ghana.

Ikiwa imepita katika mikono ya watayarishaji muziki wanane akiwamo S2kizzy na Abbah, tayari nyimbo mbili kutoka katika The God Son (2024) zimeshaachiwa ambazo ni Hakuna Matata, 2025, Unanichekesha.

Kwa mujibu wa cover ya albamu hiyo, mtayarishaji mkuu ni mtoto wa kwanza wa Marioo na Paula, Princesss Amarah ambaye ana umri wa miezi saba sasa, wakati ile ya kwanza mtayarishaji mkuu alikuwa ni Abbah ambaye ndiye kamtoa msanii huyo kimuziki.

Utakumbuka Marioo alianza kung’aa kimuziki baada ya kuurudia wimbo wa Lameck Ditto, Moyo Sukuma Damu (2016) ambao ulimvutia Prodyuza Emma The Boy na kumuomba Ruge Mutahaba ampe nafasi pale Tanzania House of Talent (THT).

Mwaka mmoja baadaye alikuja kutoka na ngoma yake, Dar Kugumu (2018) iliyotayarishwa na Abbah, na kwa sasa ana utitiri wa nyimbo zilizofanya vizuri hadi kushinda tuzo tano za TMA huku akishirikiana na wasanii wengi wakubwa.

Akizungumza katika TMA 2023 hafla iliyofanyika Oktoba 19 mwaka huu, Marioo alidai msimu ujao atabeba tuzo nyingi zaidi ikiwemo ile ya Albamu Bora ya Mwaka ambayo tangu msimu wa 2021 walioichukua ni Alikiba, Barnaba na Harmonize.

Kauli ya Marioo ilikuja kufuatia kushinda tuzo mbili za TMA 2023 kama Mwimbaji Bora wa Kiume Bongofleva na Mwandishi Bora, akiungana na mastaa wengine waliobeba tuzo mbili mbili usiku huo ambao ni Zuchu, Harmonize na Young Lunya.

Ikumbukwe katika TMA 2022 ushindi wa Albamu Bora ulienda kwa Barnaba (Love Sounds Different) akiwabwaga washi-ndani wake ambao ni Harmonize (Made For Us), Conboi (Street Ties), Kusah (Conboi) na Marioo (The Kid You Know).

Hilo lilimfanya Marioo kuibuka na kudai kuwa albamu yake ilikuwa kali kuizidi ile Barnaba ambayo mtayarishaji wake mkuu alikuwa ni Diamond Platnumz, akijibu hilo Barnaba alisema kama Marioo anaona kadhulumiwa basi akachukue tuzo hiyo.

Albamu hiyo ya Barnaba iliyotoka na nyimbo 19 ilishirikisha mastaa kama Alikiba, Diamond, Jux, Nandy, Rayvanny, Phina, Jay Melody, Kusah, Young Lunya, Mbosso, Khaligraph Jones, Joel Lwaga, Khadija Kopa, Lady Jaydee n.k.

Hadi sasa albamu hiyo imesikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 66.2 katika mtandao wa Boomplay Music, wakati ile ya Marioo imefikisha milioni 113.6, hiki ndio Marioo alikuwa analalamikia kuwa albamu yake imezidi namba hiyo ya Barnaba vipi akose tuzo?.

Sasa Marioo kutokea Bad Nation Label ameachia albamu mpya, The God Son (2024) ngoja tuone kipi ataambulia msimu ujao ukizingatia kuna wasanii wengine wametoa albamu pamoja na EP ambazo nazo huwekwa katika kipengele hicho.

Waliotoa albamu hadi sasa ni Roma (Nipeni Maua Yangu), Jay Melody (Therapy), Young Lunya (Mbuzi), Stamina (Msanii Bora wa Hip Hop) n.k, huku EP wakiwa ni Anjella (The Black Queen), Rayvanny (ZiiBeats Vol.2), Bwana Misosi (Mbona Kimya), Alikiba (Starter) n.k.

Katika TMA msimu huu iliyoshinda Albamu Bora ya Mwaka ni ‘Visit Bongo’ ya Harmonize ikizibwaga albamu nyingine nne, ‘5’ ya Abigail Chams, ‘Swahili Kid’ ya D Voice, ‘Most People Want This’ ya Navy Kenzo na ‘Flowers III’ ya Rayvanny.

Hata hivyo, ushindi huo ulikuja baada ya Harmonize kuwania kipengele hicho misimu miwili mfululizo bila ushindi, aliwania kupitia albamu zake High School (2021) na Made For Us (2022), hivyo Marioo anaweza kukosa pia.

Tuzo za TMA ambazo zilianzishwa mwaka 1999 na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ziliporejea msimu wa 2021 baada ya kusimama tangu 2015, Alikiba ndiye alishinda Albamu Bora ya Mwaka.

Ni kupitia albamu yake ya tatu, Only One King (2021) iliyotoka kwa ushirikiano wa Ziiki Media na Kings Music, washindani wake walikuwa ni Harmonize (High School), Marco Chali (Ona), Wakazi (Live At Sauti za Busara) na Weusi (Air Weusi).

Na huenda msimu ujao ambao Marioo anasema atashinda naye Alikiba akawania kupitia EP yake ya kwanza, Starter (2024) yenye nyimbo saba huku akiwashirikisha Jay Melody, Marioo na Nandy, Msanii Bora wa Kike TMA 2023 ikiwa ni tuzo yake ya nne.