Jose Chameleone asimulia magumu aliyopitia, amtaja Professor Jay

Muktasari:
- Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ,Chameleone amesema alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya Kongosho kutokana na matumizi ya pombe kali na uvutaji wa Sigara kupindukia.
Dar es Salaam. Mwanamuziki kutokea nchini Uganda, Jose Chameleone amewasili Tanzania jioni ya leo Mei 8, 2025 na kuzungumza kuhusu maendeleo ya afya yake ambayo ilitetereka tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ,Chameleone amesema alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya Kongosho kutokana na matumizi ya pombe kali na uvutaji wa Sigara kupindukia.

"Nilikuwa nasumbuliwa na Kongosho iliyosababishwa na kunywa pombe sana, kuvuta sana Sigara, na mawazo kwa hiyo wamefanya upasuaji na mpaka sasa natumia dawa baada ya mwaka mmoja ndiyo naweza kumaliza," amesema Jose.
Amesema mwanaye wa kwanza Marcus Abba alichozungumza kuhusu msanii huyo kuwa na marafiki wengi wanaompotosha ni utoto na hawezi kuisha bila marafiki.
"Yule ni mtoto na watoto mara nyingi hawajui nini wazazi wao wanapitia lakini baada ya kuongea hivyo nilikutana naye na akanielewa, mimi sikuchagua kuumwa, kuwa mgonjwa, yule alikuwa akiongea kitoto anamlalamikia baba yake.
"Ndio maisha yalivyo na mimi siwezi kuishi bila marafiki nina marafiki matajiri, masikini, wenye faida na wasio na faida kwa hiyo sina uchaguzi lakini kiukweli alisema anacho jua na anachojifikiria na niliposikia nilimwambia ajirekebishe ili tuwe pamoja," amesema Chameleone.
Aidha, msanii huyo ameelezea sababu iliyopelekea kufika nchini akisema kuwa ni kutoa shukrani kwa Watanzania kwa kumuombea alipokuwa na matatizo ya kiafya lakini pia kuwathibitishia bado yupo hai.

"Kwanza kuwatembelea Watanzania lakini pili Watanzania waliniombea sana wakati nilipokuwa na matatizo ya kiafya, lakini kuna watu walikuwa wanadhani nimekufa sasa nimewatembelea ili wajue kama bado nipo hai, lakini kikubwa nikuwapa shukrani kwa kuniombea," amesema Jose.
Amesema kuwa lazima afike kumjulia hali mkongwe wa Bongo Fleva, Professor Jay ambaye naye bado hali yake kiafya haijaimarika vizuri kwani alimuombea wakati anaumwa.
"Professor Jay ni mwanangu kabisa hata nilivyokuwa Kampala ameniombea niweze kupona lakini na mshukuru Mungu nimeshatoka hospitali, ni ndugu yangu sasa nataka nimtembelee nimechoka kumuona mitandaoni nataka nimuone mwenyewe tuzungumze zaidi na mimi nimpe nguvu" amesema Jose.

Utakumbuka Jose Chameleone alikuwa akisumbuliwa na Kongosho hali iliyosababisha kusafirishwa kutoka hospitali ya Nakasero, Kampala nchini Uganda hadi Marekani kwa ajili ya matibabu, ambapo Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni aligharamia matibabu na Aprili 12, 2025 alirejea nchini kwao huku afya yake ikiwa imeimarika zaidi.