Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afrika yaazimia mambo sita kukabili mabadiliko ya tabianchi

Wajumbe wa Mkutano wa Kundi la Majadiliano ya Mabadiliko ya Tabianchi Afrika (AGN) kutoka mataifa 54 wakiwa kwenye majadiliano katika mkutano uliofanyika Zanzibar ikiwa ni maandalizi ya kuelekea mkutano wa COP30 unaotarajiwa kufanyika Novemba nchini Brazil. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Afrika inahitaji Dola 1.3 trilioni za Marekani kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Unguja. Mambo sita yameazimiwa katika mkutano wa kundi la wataalamu wa majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi Afrika (AGN) ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo wezeshi ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya tabianchi na kutumia maliasili zilizopo kuyanufaisha mataifa hayo.

Mkutano huo uliohudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa 54 ya Afrika, pia umeamua kuunda kikosi kazi kitakachoshughulikia masuala ya Afrika na kuwa na msimamo wa pamoja wanapozungumzia masuala ya Afrika.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo Mei 2, 2025, Mwenyekiti wa AGN, Dk Richard Muyungi amesema ajenda kubwa ni kutengeneza mshikamano katika mikutano ya kimataifa namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tumeamua tutumie njia za kisayansi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pia tumekubaliana misimamo yetu ya pamoja ndiyo itatuongoza kupigania kitu kimoja tunachokitaka kama Bara la Afrika,” amesema.

Dk Muyungi amesema wamekubaliana mtaji wa maliasili zilizopo Afrika uwe uti wa mgongo wa majadiliano wanayofanya. “Kuna msitu wa Congo ambao unanyonya hewa ukaa kwa kiasi kikubwa, huku asilimia 40 ya madini yanatoka Afrika, lazima tutumie maliasili hizi kama mtaji,” amesema.

Mkutano huo umeazimia kuongeza ushiriki wa vijana na usawa wa jinsia katika masuala ya tabianchi.

Akifunga mkutano huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Cyprian Luhemeja amesema Afrika inaendelea katika mazingira magumu kwa sababu ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

“Sisi hatuchafui, lakini tunaathiriwa sana. Zaidi ya watu bilioni moja wapo nyuma yetu wanataka tupambane kwa niaba yao,” amesema.

Amesema wanapaswa kupeleka ajenda kwa mshikamano na kuwaeleza waziwazi kwamba fedha wanazotoa hazitoshi na msisitizo uwe upatikanaji wa fedha na kuwa na mikopo isiyokuwa mzigo kwa mataifa hayo.

“Vigezo vya kupata fedha hizi lazima viwe wazi ili kuepuka masharti magumu ya ukopeshaji, ushirikishaji wa vijana na kuwajengea uwezo maana mustakabali wa Afrika upo mikononi mwa vijana, amesema.

Amesema lazima wajenge kwenye fikra zao kwamba Afrika si Bara maskini.

“Ni wakati wa kusimama na kusema sisi si maskini kwa hiyo tusimame kuwa na sera na mifumo ya kulinda rasilimali zetu,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa kukabiliana  na upotevu na madhara (FRLD), Dk Ibrahim Diong amesema mikutano ya aina hiyo inawafanya kuwa wamoja na kutengeneza ajenda za pamoja kwa ajili ya masilahi ya Bara hilo.

Amesema ni wakati sasa wa kushikamana na kutekeleza ajenda kwa umoja badala ya kuparaganyika.

Akizungumza kuhusu mfuko wa FRLD, Dk Diong amesema wameupigania kwa zaidi ya miongo mitatu, hivyo baada ya kuanzishwa lazima wajizatiti kuhakikisha fedha za kutosha na zenye usawa zinapatikana.

Licha ya Afrika kuchangia asilimia nne ya mabadiliko ya tabianchi, amesema ndiyo inayoathiriwa zaidi.

“Ndiyo maana mfuko huu ni muhimu, lakini unapaswa uwasaidie walengwa na jamii inayoathirika na mabadiliko ya tabianchi kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Katika mipango hiyo amesema ni kuhakikisha hakuna mtu hata mmoja anabaki nyuma, hivyo lazima kuyabana mataifa yaliyoendelea kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia changamoto hizo.

Kati ya fedha zinazopatikana amesema Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zitakazopewa kipaumbele kwa ajili ya kukabiliana na athari hizo.

Mkutano huo ulilenga kujadiliana kuhusu vipaumbele na mipango mikakati ya Bara la Afrika kuelekea mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa (COP30) kuhusu mabadiliko ya tabianchi unaotarajia kufanyika Novemba, mwaka huu nchini Brazil.