Benki ya NCBA yakoleza mapambano mabadiliko ya tabianchi

Muktasari:
- Mto Mpiji ni mojawapo ya vyanzo muhimu vya maji katika Wilaya ya Kinondoni ambavyo kwa miaka ya hivi karibuni vimeathiriwa na uharibifu wa mazingira, ujenzi holela, uchafuzi wa maji na ukataji miti.
Dar es Salaam. Wakati dunia inapambana na mabadiliko ya tabia nchi, Benki ya NCBA Tanzania imeamua kurudisha shukurani kwa jamii kwa kupanda ili kusaidia mapambano hayo.
Katika jitihada hizo imepanda miti zaidi 8,000 nchini nzima ikiwa ni utekelezaji wa kampeni maalumu ya kusaidia mapambano ya mabadiliko ya tabianchi.
Katika kampeni hiyo, miongoni mwa maeneo waliyolenga kuyanusuru ni kwenye vyanzo vya maji, ambapo benki hiyo ilipanda miti 5,000 kandokando ya Mto Mpiji, eneo la Bunju B jijini Dar es Salaam.
Kulingana na dhamira ya dhati ya benki hiyo kuhakikisha mazingira ya kuishi yanakuwa salama pamoja na vyanzo vya maji, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA, Alex Mziray ameongoza mamia ya washiriki kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, viongozi wa kijamii, wafanyakazi wa benki na wakazi wa Bunju, kurejesha uhai wa Mto Mpiji kwa kupanda miti.

Mto Mpiji ni mojawapo ya vyanzo muhimu vya maji katika Wilaya ya Kinondoni ambavyo kwa miaka ya hivi karibuni vimeathiriwa na uharibifu wa mazingira, ujenzi holela, uchafuzi wa maji na ukataji miti.
“Kupanda miti hii 5,000 ni hatua ya matumaini, ya mabadiliko na ya uwekezaji kwa maisha ya sasa na ya vizazi vijavyo. NCBA tunataka kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto kubwa zinazoikabili dunia yetu, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mziray.
Miti iliyopandwa ni mchanganyiko wa aina za asili na zile zinazokua haraka ambazo zinasaidia kuimarisha kingo za mito, kupunguza mmomonyoko wa udongo na kuwezesha mazingira ya asili kurejea kama ilivyokuwa awali.
Mbali ya kupanda miti, wananchi wa eneo hilo walipewa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira, faida za kuulinda mtu huo na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunapanda miti, lakini tunapanda pia maarifa, mshikamano na uwajibikaji wa pamoja,” amesema Mziray.
Amefafanua kuwa kampeni hiyo ni mwendelezo wa shughuli mbalimbali ambazo NCBA ilianza kuzifanya tangu mwaka uliopita ikiwemo upandaji miti Zanzibar kwa ajili ya kuhifadhi ukanda wa pwani, Arusha katika hospitali za jijini Mwanza.
Hadi sasa zaidi ya miti 8,000 imekwishapandwa nchini kote.
Kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, NCBA benki inaamini kuwa mafanikio ya utunzaji mazingira yanahitaji hatua za pamoja kutoka sekta binafsi, Serikali jamii na washirika wa maendeleo.