Wadau, Serikali kujadili makali ya mabadiliko ya tabianchi

Muktasari:
- Lengo kuu la warsha ni kuimarisha uelewa wa wadau kuhusu njia za upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, sambamba na mikakati madhubuti inayoendana na hali halisi ya maeneo nchini.
Dar es Salaam. Siku tatu za kujadili athari za mabadiliko ya tabianchi kuwakutanisha wadau pamoja na Serikali jijini Dar es Salaam lengo ikiwa ni kuimarisha uelewa wa njia za kukabiliana na athari hizo, ikiwemo upatikanaji wa fedha pamoja na mikakati.
Wadau hao Shirika la Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) pamoja na taasisi za Serikali katika siku ya kwanza ya warsha, watajadili athari na udhaifu wa mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya Pwani na ukanda wa kati hapa Tanzania, kupitia mazoezi ya vikundi, masomo ya mifano na mijadala mbalimbali.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano, Aprili 23, 2025 katika taarifa ya UNCDF walioandaa warsha hiyo ya Kitaifa kwa lengo la kuimarisha uelewa na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uhimilivu kwa maendeleo endelevu nchini Tanzania itakayofanyika.

Mfuko wa UNCDF, kupitia Mfumo wa Maisha ya Uhimilivu wa Tabianchi kwa Ngazi ya Serikali za Mitaa (LoCAL), umekuja na warsha hiyo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa wadau na kuongeza uelewa na uwezo wa jinsi ya kuainisha vipaumbele vya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, katika awamu ya pili ya utekelezaji wa programu ya LoCAL nchini Tanzania.
Mratibu wa LoCAL, Aine Mushi amesema kipaumbele kitawekwa kwenye kuongeza uelewa, uwezo wa kupanga vipaumbele na kuingiza vifungu kwenye bajeti ya mamlaka za serikali za mitaa na kujenga uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi kwa wananchi, kwa kutumia mbinu shirikishi na zinazozingatia usawa wa kijinsia.
Aine amesema malengo ya warsha mfuko umesema unataka kuongeza uelewa wa wadau kuhusu mpango wa LoCAL kama jukwaa la kuendeleza harakati za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhamasisha upatikanaji wa fedha za kujenga uwezo wa kukabiliana na athari hizo nchini Tanzania.
“Kujenga uwezo wa kufanya tathmini za athari na uhimilivu wa mabadiliko tabianchi ili kusaidia upangaji wa mikakati ya kukabiliana na hali hiyo katika ngazi ya halmashauri, kusaidia halmashauri kuingiza mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo ni vipaumbele vya jamii husika kwenye mipango na bajeti za halmashauri,” amesema Aine.

Mratibu huyo amesema siku ya pili itajikita katika kuingiza mikakati ya mabadiliko ya tabianchi kwenye mipango na bajeti za halmashauri. Mada zitahusisha matumizi ya zana za uandaaji na upangaji wa bajeti, mifumo ya ufuatiliaji na tathmini. Mafunzo yataendeshwa na wataalamu kutoka Chuo cha Mafunzo ya Serikali za mtaa cha Hombolo na Chuo cha Mipango Dodoma.