Watiania urais waendelea kusaka wadhamini, waeleza matumaini yao
Muktasari:
- Ratiba iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), shughuli ya kurejesha fomu za kuomba uteuzi itakamilika Agosti 27, 2025 saa 10:00 jioni na siku hiyohiyo Tume itafanya uteuzi, kabla ya kuanza kampeni Agosti 28, 2025.
Dar es Salaam. Watiania wa urais wanaowakilisha vyama vyao wameendelea kuchanja mbuga katika mikoa mbalimbali kutafuta wadhamini, huku wakieleza matumaini yao ya kukamilisha mchakato huo kwa mafanikio.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024, watiania wa nafasi ya urais wanatakiwa kuwa na wadhamini 200 kutoka kwenye kila mkoa kwa jumla ya mikoa 10 ambapo kati ya hiyo, miwili iwe ya Zanzibar.
Ratiba iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), shughuli ya kurejesha fomu za kuomba uteuzi itakamilika Agosti 27, 2025 saa 10:00 jioni na siku hiyohiyo Tume itafanya uteuzi, kabla ya kuanza kampeni Agosti 28, 2025.
Akizungumzia upande wa chama chake, Mwenyekiti wa DP, Philip Fumbo amesema mwaka 2020, kilipata wadhamini mikoa yote bila changamoto yoyote, na mwaka 2025 mambo yanakwenda kama walivyopanga.
“Hatuna shaka, DP ni tumaini la Watanzania hatujawahi kuanguka, tayari tumepata wadhamini kwenye mikoa ya Iringa, Morogoro, Dar es Salaam, Pwani, Kigoma, Tabora na Zanzibar, tutakamilisha ratiba yetu ya kusaka wadhamini kwa wakati,” amesema.
Chama hicho kinawakilishwa na Abdul Mluya na mgombea mwenza wake, Abrahman Khatib kuipeperusha bendera yake kwenye kinyanganyiro cha kugombea nafasi za urais.
Kwa upande wake, mtiania wa urais kupitia UDP, Saum Rashid amesema bado anazunguka mikoani kusaka wadhamini na matarajio yake ni kwamba hadi Agosti 22, 2025, yeye na mgombea mwenza, Juma Faki watakuwa wamekamilisha, kwani wameweka utaratibu wa kuwapatia viongozi wao mikoani fomu hizo ili kufanikisha mchakato huo.
Mgombea urais kupitia NLD, Doyo Hassan Doyo amesema hadi sasa wamekamilisha kupata wadhamini katika mikoa minane.
“Mikoa tuliyokamilisha kupata wadhamini ni Dodoma, Singida, Manyara, Arusha, Tanga, Pwani, Morogoro na Dar es Salaam na tunataraji kukamilisha mchakato huu Agosti 20, 2025,” amesema Doyo.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa amesema kabla ya Agosti 23, 2025 watakuwa wamekamilisha utaratibu huo.
“Tayari tumepata wadhamini kwenye mikoa sita na tunaendelea na mikoa iliyobaki. Mikoa ambayo tayari ni Dar es Salaam, Lindi, Pwani, Dodoma, Unguja na Pemba,” amesema.
Mtiania wa urais kupitia CUF, Gombo Samandito Gombo ambaye baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa INEC aliahidi endapo atachaguliwa kuwa rais, atasimamia haki na kuhakikisha rasilimali za Taifa zinawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.
Kwa upande wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasini ambaye ni mgombea mwenza wa kiti cha urais wa chama hicho, amesema licha ya kuwa miongoni mwa waliochukua fomu mwishoni, tayari wamepata wadhamini katika mikoa sita.
“Tunatarajia Agosti 22, 2025 tuwe tumekamilisha, kwa sasa tunaendelea na ziara kwenye mikoa iliyosalia na tutakamilisha kwa muda husika,” amesema.
NCCR Mageuzi ilimteua Haji Ambari Khamisi kuwa mwakilishi wake wa urais, akishirikiana na Joseph Selasini kama mgombea mwenza.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa ADC, Shaban Itutu amesema ndani ya wiki moja watakuwa wamekamilisha kupata wadhamini.
“Kwa sasa tunaendelea kutafuta wadhamini, ndani ya wiki moja tutaita waandishi wa habari na kutoa taarifa yetu kama chama,” amesema.
Katibu Mkuu wa AAFP, Rashid Rai amesema bado wanaendelea kutafuta wadhamini mikoani na watakamilisha Agosti 20, 2025.
“Tumeshakamilisha mikoa saba tumebakiza mitatu, baadhi ya mikoa tuliyokamilisha ni Mtwara, Ruvuma, Lindi, Pwani, visiwa vya Unguja na Pemba. Mikoa hii iliyobaki tutaifikia kwa wakati,” amesema Rai.
Kwingineko mkoani Njombe, mtiania wa nafasi ya urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu anaendelea na ziara yake ya kusaka wadhamini huku akizungumza na makundi mbalimbali ya wanachama wa chama hicho.
Mwalimu amesisitiza umuhimu wa makaa ya mawe na miti katika kujenga uchumi wa Mkoa wa Njombe.
“Makaa ya mawe yanasafirishwa asubuhi hadi jioni, Njombe inaendelea kuwa maskini, Njombe mmekosa viongozi makini wa kusimamia rasilimali hizi ziweze kuwanufaisha,” amesema mtiania huyo.
Amesema akishinda nafasi hiyo atahakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kwa masilahi ya wakazi wa eneo hilo badala ya kusafirishwa huku wenyeji wakibaki maskini.