Wajumbe mguu sawa Mkutano Mkuu wa CUF
Muktasari:
- Jumla ya majina matano yanatarajiwa kuwasilishwa mbele ya wajumbe hao baada ya kupitishwa na Kamati ya Uongozi, kisha Baraza Kuu la chama hicho na kujiridhisha wamekidhi vigezo, hivyo ni kazi ya wajumbe wa mkutano mkuu kumchagua anayefaa.
Dar es Salaam. Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) wameanza kujongea ukumbini, tayari kwa kutekeleza shughuli yao ya kuwachagua watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar Oktoba 29, 2025.
Jumla ya majina matano yanatarajiwa kuwasilishwa mbele ya wajumbe hao, baada ya kupitishwa na kufanyiwa mchujo na Kamati ya Uongozi, kisha Baraza Kuu la chama hicho na kujiridhisha wamekidhi vigezo, hivyo ni kazi ya wajumbe kumchagua anayefaa.
Kati yao, watiania wawili wanawania nafasi ya Rais, ambao ni Mkunyutila Siwale na Samandito Gombo huku Rose Kuhoji ambaye pia alitia nia, jina lake limeondolewa na Baraza Kuu la chama hicho kwa kosa la kuunga mkono walioleta vurugu zilizofanyika Agosti 6, 2025 katika kikao cha Baraza Kuu la chama hicho.
Kwa upande wa Zanzibar, makada watatu waliotia nia wote wamepenya, ambao ni Habib Mohammed, Masoud Hamad na Mohamed Khatib. Wote watafikishwa mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu ili wamchague mmoja wao atakayepeperusha bendera ya chama hicho upande wa Zanzibar.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) wameshawasili ukumbini, tayari kwa kutekeleza shughuli yao ya kuwachagua watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar Oktoba 29, 2025.
Shughuli inayoendelea kwa sasa ni usajili wa wajumbe ili waingine kwenye ukumbi wa Lekham Social Hall. Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wanalalamikia urasimu katika utaratibu huo unaoonekana kuwachosha kwa kusimama muda mrefu.
Viongozi mbalimbali wa chama hicho wameshaanza kuwasili akiwemo Katibu Mkuu, Husna Abdallah, Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya na wengineo.
Mohamed Pazi, mmoja wa wajumbe wanaotakiwa kuingia ndani ya ukumbi huo, analalamikia utaratibu uliowekwa, jambo linalowafanya kusimama kwa muda mrefu.
“Utaratibu ulipaswa kuwa mzuri ili tusipoteze muda mrefu, kwa kuwa jambo tunalokwenda kulifanya ni kubwa,” amesema.
Akiwa na mtazamo kama huo, Hamad Hamad amedai chama hicho hakijawahi kuboresha utaratibu wa wajumbe kuingia kwenye ukumbi kwani kila ifikapo nyakati kama hizo, mambo yatakuwa hivyo hivyo.
“Ustaharabu ni jambo nzuri, ni sababu ya kila mkutano kutokea vurugu sababu kubwa viongozi hawataki kuweka utaratibu rafiki wa kuingia,” amesema Hamad.