Vuta-nikuvute AAFP Soud kujitangaza mgombea urais Zanzibar
Mtia nia kuomba nafasi ya Urais Zanzibar kupitia chama cha Wakulima AAFP, Said Soud Said akieleza dhamira yake na kutangaza sera za chama chake kwa waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Mwera Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Wakati Soud akijinasibu kutangaza msimamo huo, chama chake cha AAFP na Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa, wamesema hawamtambui kama mtiania wa nafasi hiyo, kwa sababu amekiuka utaratibu.
Dar es Salaam. Mwanasiasa Said Soud Said, ameingia na mguu wa kushoto, kwenye kinyang’anyiro cha uraia katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu baada ya kujitangaza ndiye mgombea wa nafasi hiyo.
Ni mguu wa kushoto kwa sababu si Chama chake cha Wakulima (AAFP), wala Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, inayomtambua kama mtiania wa urais wa Zanzibar. Taasisi hizo zote mbili zimemkana Soud kwa nyakati tofauti.
Dalili za Soud kukataliwa zilianza kuonyeshwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa AAFP uliofanyika Aprili 30, mwaka huu Dar es Salaam, baada ya mwanasiasa huyo, kupigiwa kura nyingi za hapana na kushindwa kupewa ridhaa ya kuwania urais wa Zanzibar.
Inadaiwa baada ya Soud, aliyekuwa mtiania pekee, kushindwa kuteuliwa kuwania urais, alisababisha vurugu katika mkutano huo kwa kuwakimbiza baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar, waliompinga.
Mkutano mkuu wa chama hicho, ulitamatika pasipo kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya AAFP.
Kutokana na hilo, Ofisi ya Msajili ilikiagiza chama hicho kuitisha upya mkutano mkuu kwa siku zijazo na ikiwa hakina fedha, kiitishe halmashauri kuu ili kumpata mgombea wa nafasi hiyo.
Lakini, katika hali ya kushangaza jana Alhamisi Agosti 14, 2025 mbele ya kamera za wanahabari mjini Unguja, Soud alijitokeza na kujitangaza ndiye mgombea wa urais wa Zanzibar, akitaja sababu mbalimbali.
Hatua hiyo imeibua mtafaruku na kuacha maswali mengi kuhusu mwelekeo wa AAFP wa kumpata mgombea huku waliojipanga kuwania nafasi hiyo wakibaki njiapanda.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa AAFP, Rashid Rai amesema hawamtambui Soud kama mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia chama hicho.
Hata Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa, imesema kitendo hicho hakina msingi wa kisheria, ni kinyume na taratibu rasmi.
Maelezo ya Soud
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Agosti 15, 2025, Soud amesema licha ya sintofahamu iliyopo kwa baadhi ya makada, dhamira yake ya kuwania urais Zanzibar iko palepale, akieleza hababaishwi na wanaopiga kelele.
“Nimejidhatiti kushiriki kikamilifu katika kinyang’anyiro hicho ili kuwatumikia Wazanzibari, ninazo sababu za uamuzi wangu wa kutangaza nia.
“Sihitaji kuwajibu watu kwa sasa, mkutano mkuu wanaodai kuwa ulipiga kura ya kunikataa ulikumbwa na changamoto nyingi na haukuwa na uwazi wa kutosha,” amedai Soud.
Amesema wakati ukifika wa Tume ya Taifa ya Zanzibar (ZEC) kuweka taratibu rasmi za kuchukua fomu za kugombea urais, atatoa maelezo ya kina kuhusu uamuzi wake kuwania nafasi hiyo.
“Nikichukua fomu ndipo nitakapowaeleza sababu zangu za kugombea urais, kwa sasa nawaomba wananchi waendelee kuwa watulivu na kuvuta subira,”ameeleza.
Soud amesema shabaha yake ni kuleta mabadiliko ya kweli, kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua kimaendeleo kwa kusimamia haki, usawa na ustawi wa wananchi wote.
Mchakato bado
Licha ya Soud kueleza hayo, Rai amesisitiza kwa sasa AAFP inaendelea na mchakato rasmi wa kumpata mgombea urais wa Zanzibar, huku akimtupia kijembe Soud.
“Nafasi hiyo bado iko wazi, tupo hatua za mwisho za kuitisha Halmashauri Kuu ya chama ili kukamilisha mchakato huo.
“Katiba na kanuni zetu ziko wazi, mtu akikataliwa na wajumbe, mchakato uanza upya. Soud alikataliwa hatakiwi kuwania tena, bali anapaswa kutafutwa kada mwingine,” amesisitiza Rai.
Kwa mujibu wa Rai, baada ya Soud kushindwa, chama kilifungua dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu ili kutoa fursa kwa makada wapya kuwania nafasi hiyo.
“Hatuwezi kukubali vitendo vya mtu kutumia nafasi yake vibaya, chama hakimtambui Soud kama mtiania. Kwa mujibu wa Katiba yetu, taarifa rasmi za uteuzi hutolewa na katibu mkuu,” amesema Rai.
Maelezo ya Rai yanaungwa mkono na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, akisema, “hatua ya Soud ni kufurahisha umma, haina uhalali wowote kikatiba wala kikanuni.”
Nyahoza amefafanua kuwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo, mtiania halali wa chama lazima apitie michakato rasmi iliyoainishwa katika katiba ya chama husika na kuzingatia masharti ya Ofisi ya Msajili.
“Nikwambie, ofisi yetu haimtambui. Kwa sababu ili uwe mtiania lazima upitie michakato yote inayotambulika na kuhisisha uwakilishi ofisi ya msajili,” amesema.
Nyahoza amesisitiza kuwa Soud amekiuka taratibu za AAFP na hatambuliwi na kama mtiania rasmi. Amesema waliwaelekeza AAFP kuitisha kikao cha Halmashauri Kuu ili kumpata mtiania wa nafasi hiyo, hata hivyo bado mchakato haujakamilika.
“Haijatekelezwa, sasa inakuaje ajitangaze? Hicho ni kitendo batili, hatumtambui. Tunachojua mchakato bado unaendelea,” amesisitiza.
Ahadi za Soud
Soud ambaye kila msimu wa uchaguzi amekuwa akitoa ahadi mbalimbali zenye mbwembwe, amesema iwapo atapata ridhaa ya kuongoza Zanzibar, vijana wote wa kisiwa hicho wataoa bure na mahari zao zitalipwa na Serikali.
Pia, Soud amesema atapiga marufuku kutengeneza vitanda vyenye ukubwa wa futi sita kwa sita, badala yake mafundi watapaswa kutengeneza vyenye ukubwa wa futi tatu kwa nne ili kuongeza kizazi.
“Vijana wote wataoa kwa pesa za Serikali, hakuna kijana atakayetoa mahari yake. Serikali ina fedha nyingi mpaka inafikia hatua ya zinaibwa, mimi kwa nini nisichukue fedha zile nikawapa vijana kwamba Sh1 bilioni hii, kila mfungo saba, au mfungo mosi, au mwezi wa Shaaban chukua mkaoe ili kuepuka ubakaji,” amesema.
Kuhusu hoja ya kuongeza uzazi, Soud ambaye amegombea urais zaidi ya mara moja, amesema: “Nitakapopata nafasi ya urais, nchi hii haitakuwa na vitanda vya sita kwa sita, havitazidi futi nne.”
Kama hiyo, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Soud baada ya kuchukua fomu ya kuwania urais aliwaahidi wanahabari wa Zanzibar kuwanunulia bajaji mpya, ili kurahisisha usafiri akisema kundi hilo ni wapiganaji sawa na wanajeshi.
“Kila mwandishi wa habari wa Zanzibar mwenye cheti cha uandishi, nitampatia bajaji mpya kutoka India,”alisema Soud ambaye aliwahi kuwa waziri asiyekuwa na wizara maalumu chini ya utawala wa Dk Ali Mohamed Shein.