Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

AAFP yaweka msimamo Uchaguzi Mkuu 2025

Muktasari:

  • Chama cha AAFP kimetangaza rasmi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 kikisema kimejipanga kikamilifu kwa ajili ya kinyang’anyiro hicho na kushinda uchaguzi.

Dar es Salaam. Katika kile kinachoweza kutazamwa kama mwanzo wa sura mpya katika siasa za Tanzania, Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP) kimesema kimekamilisha maandalizi ya kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kikisema kiko tayari kuongoza taifa kwa misingi ya mabadiliko ya kweli.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika Julai 7, 2025 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho, Rashidi Rai amesema AAFP hakipo kwenye medani ya siasa kwa ajili ya kushiriki maigizo ya kisiasa, bali kwa lengo la kusimika uongozi mpya unaosimamia masilahi ya Watanzania wa kawaida.

Rai amesema siasa ya Tanzania imejaa kelele, chuki na vitisho kutoka kwa wanasiasa aliowaita ambao wanachochea vurugu na kugawa taifa kwa misingi ya itikadi badala ya hoja. Amesema AAFP haipo tayari kushiriki siasa hizo na badala yake imejipanga kuwa sauti ya matumaini.

“Tumechoka na siasa za matusi. Tumeshuhudia miaka mingi ya porojo na ahadi zisizotekelezwa. Sisi tunakuja na ajenda ya mabadiliko yanayoonekana, yanayogusa maisha ya kila Mtanzania,” amesema Rai.


Uteuzi wa wagombea

Katika hatua iliyodhihirisha kwamba chama hicho hakipo kwa ajili ya kushabikia siasa za jukwaani pekee, AAFP kimeweka wazi kuwa tayari kimemteua Kunje Ngombare Mwiru kuwa mgombea wake wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kunje, ambaye ametajwa kuwa ni mtu wa maono, amekulia katika mazingira ya kawaida na ana historia ya kupambana na changamoto za maisha akiwa karibu na jamii. Chama hicho kimemuona kama mtu sahihi wa kusimamia ajenda ya mageuzi.

Mgombea mwenza wake, Chumu Abdallah Juma, ni mwanamama mwenye rekodi ya utumishi katika jamii na uelewa wa kina kuhusu masuala ya kijamii na kiuchumi, hasa katika maeneo ya pembezoni.

“Tunaamini hawa si wagombea wa majina makubwa, bali ni watu wa kazi. Ni viongozi watakaoweka mbele masilahi ya taifa, si matumbo yao wala kundi dogo la waliobarikiwa,” aliongeza Katibu Mkuu huyo.


Msimamo wa kushiriki uchaguzi

AAFP imesisitiza kuwa haitashiriki siasa za kujivuta au kulalamika pembeni huku taifa likihitaji uongozi. Chama hicho kimesema kinatambua changamoto katika mfumo wa uchaguzi, lakini hakiwezi kuacha nafasi hiyo ya kihistoria kupita.

“Hatutaikimbia nafasi hii ya kihistoria kwa sababu wengine wameamua kususia. Hatuogopi uchaguzi, tunachotaka ni haki na usawa. Tunaamini kuwa Watanzania wana akili ya kutosha kufanya maamuzi ya maana,” amesema Rai.

Amesisitiza kuwa AAFP hakitakubali uchaguzi wa kuviziana, wa vurugu wala wa kutumia vyombo vya dola kuzima sauti za upinzani. Hata hivyo, alisema wana imani kuwa njia ya mabadiliko ni kushiriki na si kujitoa.


Ilani na kaulimbiu

AAFP tayari imeandaa ilani ya uchaguzi yenye kaulimbiu ya mabadiliko iliyojaa mikakati ya kubadilisha sura ya nchi katika maeneo muhimu kama elimu, afya, maji, miundombinu, ajira kwa vijana, kilimo na ustawi wa jamii.

Rai amesema kuwa mabadiliko hayo si kauli tu ya kisiasa, bali ni ahadi inayotokana na maumivu halisi ya wananchi. Aliongeza kuwa miaka nenda rudi Watanzania wamekuwa wakihangaika kupata huduma za msingi, huku wakipewa ahadi zisizokoma kila uchaguzi unapokuja.

“Tunataka shule zenye walimu wanaofundisha kwa moyo, hospitali zenye dawa, barabara zinazofikika hata wakati wa mvua, na vijiji vyenye maji safi bila wananchi kutembea kilomita tano kuteka ndoo moja,” amesema kwa msisitizo.


Wito wa chama

Katibu mkuu huyo aliwataka Watanzania wote, hususani vijana na wanawake, kuchukua nafasi yao katika mapinduzi ya kisiasa kwa kushiriki uchaguzi wa mwaka huu kwa akili na umakini.

Amesema AAFP haitatoa rushwa wala kuahidi chakula jukwaani, bali itaweka mbele sera na mipango halisi ya maendeleo.

“Wakati umefika kwa Watanzania kukataa siasa za ushabiki. Hii ni fursa ya kizazi kipya kuandika historia yake. Kama tukiendelea kuchagua watu wale wale kwa sababu ya sura au ahadi za juzi, basi tusitarajie maisha mapya kesho,” amesema.


Hali ya kisiasa kwa sasa

AAFP inaingia katika mbio hizi wakati vyama vikuu vya siasa nchini vikijipanga kwa uchaguzi huo. Chama tawala CCM kimeingia katika mchakato wa ndani wa kuchuja majina ya wagombea wake, huku ACT Wazalendo na Chaumma, pia, wakihaha kuhakikisha wanapata wagombea watakaovutia umma.

Wakati huo huo, Chadema bado inashikilia msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi hadi mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi yafanyike, wakisisitiza kauli yao ya “No Reforms, No Election” ambayo imeibua mjadala mpana kitaifa kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini.

Kwa hatua hiyo ya AAFP kuingia rasmi kwenye kinyang’anyiro, mazingira ya kisiasa yanazidi kuwa na mvuto wa aina yake huku Watanzania wakisubiri kuona kama chama hiki kipya kitaweza kutikisa mizizi ya mfumo wa muda mrefu wa kisiasa au kitapita kama upepo wa kisiasa uliojaa maneno na matarajio.