Salum Mwalimu: Ni zamu ya masela kutinga Ikulu
Muktasari:
- Salum Mwalimu asema ni wakati wa kijana kuwa rais wa nchi akiwaomba vijana kumuunga mkono apiganie mahitaji yao.
Tunduru. Wakati watiania wa nafasi ya urais wa Tanzania kutoka vyama mbalimbali wakiendelea kusaka udhamini wa wananchi katika mikoa mbalimbali nchini, mtiania kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ameligeukia kundi la vijana akilihimiza kutimiza ndoto yake.
Mwalimu ambaye alianza ziara yake jana mkoani Lindi, leo ameendelea na ziara hiyo katika Mkoa wa Ruvuma ambako amewataka vijana kumuunga mkono ili akapiganie masilahi ya kundi hilo, katika serikali yake atakayoiunda akishinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano uliohudhuriwa na wananchi wa Mji wa Tunduru mkoani Ruvuma leo Jumapili Agosti 17, 2025, mtiania huyo amesema sasa ni wakati wa kumpata rais kijana atakayetatua kero za vijana.
"Siku zote tumewaamini wazee pekee katika nafasi ya urais huku vijana tukiambiwa tutulie sisi ni Taifa la kesho, sasa ni muda wa kumpata Rais kijana mwenzetu," amesema na kuongeza;
"Vijana tumesahaulika na tumeendelea kukabiliwa na changamoto nyingi, nipelekeni Ikulu msela mwenzenu ili tukapiganie masilahi yetu," amesema Mwalimu huku akishangiliwa na kundi kubwa la vijana waliokuwepo mkutanoni hapo.
Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chaumma, amesisitiza juu ya kuwekwa mkakati kamambe katika kujenga uchumi imara wa Mkoa wa Ruvuma kwa kutumia zao la korosho.
"Korosho ni zao lenye thamani kubwa duniani kote, hata ukifika ofisi kubwa utapewa korosho, ukipanda ndege utapewa korosho, hii inaonesha thamani kubwa ya zao hilo," amesema mtiania huyo.
Amesema ni jambo la kushangaza kuona mkoa maarufu kwa zao hilo ukiwa maskini huku zao lao linahitajika kila mahali kwa bei nzuri.
Katika mkutano huo, mgombea mwenza wa mtiania huyo, Devotha Minja amewaomba wakazi wa mkoa huo kumuunga mkono Mwalimu ashinde Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Devotha amesema amejiandaa vyema kuwa msaidizi bora wa rais wa nchi kupitia Chaumma ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
"Ndugu zangu, muungeni mkono Salum Mwalimu, mgombea kijana aende akapiganie maendeleo ya nchi yetu. Nimejiandaa vya kutosha kuwa msaidizi bora ili tuweze kuwaletea Watanzania maendeleo," amesisitiza.
Mwalimu, leo ameendelea na ziara yake iliyoanza jana Mkoani Lindi, akizungumza na Watanzania na kuwaomba wamdhamini kusudi atimize takwa la kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kugombea nafasi hiyo.
Katika ziara yake, mwanasiasa huyo kijana anaonekana kuvuta hisia za vijana akitumia lugha ya mtindo wa vijana (masela) jukwaani kunadi sera zake na kuomba udhamini.