Prime
Salmin Amour na harakati za muhula wa tatu
Aliyekiuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Salmin Amour
Februari 2000, anga la kisiasa Zanzibar lilijaa mawingu mazito ya sintofahamu baada ya kuibuka kwa mpango wa kubadili Katiba ya Zanzibar ili kumruhusu Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Salmin Amour, kugombea urais kwa muhula wa tatu.
Juhudi hizi, zilizokuwa na sura ya kificho na nyingine dhahiri, ziliendeshwa na baadhi ya viongozi wa SMZ kwa msaada wa makundi maalumu ya wafuasi wa Rais.
Kundi moja maarufu kisiwani Zanzibar likijiita “Ukija Usiulize”, ambalo pia lilitambulika kama wapiga debe wa Rais, liliibuka na kudai kuwa Wazanzibari bado wanamhitaji Dk Salmin, wakisisitiza kuwa ni wananchi wa Zanzibar pekee wenye mamlaka ya kumchagua au kumpinga kiongozi wao mkuu.
Mpango wa mabadiliko ya Katiba uliwasilishwa rasmi na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Idd Pandu Hassan, ambaye alipendekeza kifungu kipya kisomeke hivi: “Mtu yeyote ambaye ni Rais anaweza kuchaguliwa tena kushika kiti hicho.”
Katika taarifa yao ya fax, kundi la ‘Ukija Usiulize’ lilisisitiza kuwa Dk Salmin anazo sifa stahiki na uwezo wa kuliongoza taifa, wakionya kuwa mtu yeyote kutoka nje ya Zanzibar hastahili kuingilia nafasi ya urais wa visiwa hivyo.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Hassan Mussa Takrima, aliibuka na kueleza kuwa kikomo cha vipindi viwili vya urais kilitungwa wakati wa mfumo wa chama kimoja, ambapo jina moja tu lilikuwa likipitishwa kwa wananchi kupiga kura ya ‘ndiyo’ au ‘hapana’.
Katika enzi za vyama vingi, alisema Takrima, wananchi wana haki na fursa ya kuchagua kutoka miongoni mwa wagombea wengi—jambo ambalo kwa mtazamo wa serikali, lilifungua nafasi ya kuangalia upya ukomo wa mihula ya urais.
Katika kilele cha sherehe za miaka 23 ya CCM, Februari 5, 2000, Dk Salmin alijitokeza hadharani na kutetea hoja ya mabadiliko akisema kuwa “jinsi miaka inavyopita, ndivyo mabadiliko yanavyopaswa kutokea.”
Hata hivyo, hali haikuwa shwari ndani ya chama. Februari 13, Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar ilikutana kujadili hoja hiyo, lakini hadi usiku wa Februari 14 kuamkia Februari 15, kikao hicho kilishindwa kufikia muafaka kutokana na mabishano makali yaliyotamalaki miongoni mwa wajumbe.
Kufikia usiku wa Februari 14 kuamkia Februari 15, kikao hicho kilishindwa kufikia mwafaka na kikalazimika kuahirishwa usiku ili kiendelee tena kesho yake.
Kuahirishwa huko kulitokana na mabishano makali kati ya pande mbili zilizokuwa zinapingana kuhusu mabadiliko hayo. Kikao hicho kilikutana chini ya Waziri Kiongozi, Dk Mohamed Bilal, kabla Dk Salmin kukiongoza kwa siku mbili za Februari 14 na 15.
Mjadala mkali zaidi ulizuka baada ya baadhi ya wajumbe kuhoji sababu za hoja ya mabadiliko ya katiba kuwasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi.
Wajumbe hao walidai kuwa utaratibu huo ulikipa kikao hicho sura ya kiserikali badala ya kufuata mkondo wa chama ambapo waziri hapaswi kuwasilisha hoja kama hiyo.
Baadhi ya wajumbe walioalikwa katika kikao hicho ni pamoja na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano, Ali Hassan Mwinyi na Waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Nassoro Moyo.
Wengine ni aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Omari Ali Juma pamoja na mawaziri na naibu mawaziri wa Serikali ya Muungano wanaotoka Zanzibar ambao ni Ali Ameir Mohamed (Mambo ya Ndani), Seif Khatib (Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu), Dk Maua Daftari (Naibu Mawasiliano na Uchukuzi) na Absalaam Issa Khatib (Naibu Fedha).
Ziliibuka tena hoja nyingine za kuhusu uhalali wa badhi ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho ambao ilidaiwa kuwa kiutaratibu hawakupaswa kuhudhuria.
Baadhi ya wajumbe hao walijitetea na wengine wakatetewa. Miongoni mwa waliokumbwa na dhoruba hiyo ni Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi; Makamu wa Rais wa Muungan, Dk Omar Ali Juma na Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula.
Dhoruba hilo liliendelea tena kesho yake baada ya wazee wa CCM kutoka Pemba na vijiji kadhaa vya Unguja ambao si wajumbe wa kikao hicho kukataliwa kuingia kikaoni baada ya kufunga safari kuhudhuria.
Majadiliano yalilazimika kuingia siku ya pili baada ya wajumbe kukataa mabadiliko hayo yaliyoonekana kuwa yalishinikizwa na upande wa Dk Salmin.
Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, alijitetea kuwa alipaswa kuhudhuria kikao ili awe na fursa ya kuripoti vyema kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa iliyotoa kibali kwa kikao hicho kukaa.
Hadi wakati mjadala huo unaendelea, muswada wa mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ulikuwa unasubiriwa. Miongoni mwa ibara zilizotakiwa kubadilishwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 1995 ni pamoja na 30 (1) (b) inayosema "Mtu hatafaa kuchaguliwa kuwa Rais ikiwa amechaguliwa kushika maradaka hayo katika vipindi viwili mfululizo vilivyokwisha."
Ingawa Halmashauri Kuu ya CCM iliyokaa Dodoma mapema mwaka 2000 iliruhusu CCM Zanzibar wajadili suala la kubadili katiba baada ya kuibuka kikaoni, CCM Bara walionyesha wazi kuwa hawakuwa radhi Katiba kubadilishwa kwa maslahi ya mtu mmoja.
Tayari wabunge 52 wa CCM walikuwa wameshamwandikia barua Dk Salmin wakimtaka aachane na mipango hiyo. Hata hivyo barua hiyo ililaaniwa na wabunge wengine 28 wa CCM wa Zanzibar.
Ilipofika Februari 17 kikao hicho kilichokuwa na wajumbe 74 kiliamua kuurusha mpira kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya kushindwa kufikia mwafaka. Iliamuliwa kuwa huko nako hakutakuwa na mwafaka, basi suala hilo lingepelekwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Februari 18, ilijulikana kuwa matajiri watatu wa Zanzibar, kwa maslahi binafsi, ndio walishinikiza kufanyika kwa mabadiliko hayo ili Dk Salmin aendelee kukaa madarakani bila kikomo ili mradi tu anachaguliwa.
Aliyekuwa mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Harrison Mwakyembe (aliyewahi kuwa waziri), alisema kitendo cha Dk Salmin kuwa mwenyekiti wa kile kikao ni cha kuminya wigo wa demokrasia.
"Kumruhusu mtuhimiwa kuongoza jopo la majaji katika kesi yake mwenyewe...Sikuona sababu ya Dk Salmin kuwa mwenyekiti wa kikao kwa sababu ana maslahi katika hilo," alisema Dk Mwakyembe.
Siku moja baadaye, Februari 19, wabunge waliokuwa wakipinga mabadiliko ya Katiba Zanzibar walianza kusambaza wajumbe katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara kuwashawishi wajumbe wa NEC kukataa kuongeza kipindi kingine cha uongozi kwa Dk Salmin.
Miongoni mwa wabunge waliomwandikia barua Dk Salmin walikuwamo wajumbe kadhaa wa NEC pamoja na mjumbe mmoja wa Kamati Kuu ya CCM, Juma Ngasongwa, ambaye alikuwa mbunge wa Ulanga Magharibi. Barua yao ilisainiwa na aliyekuwa mbunge wa Mufindi, Joseph Mungai.
Wakati wabunge hao wakijiandaa kuhakikisha kuwa hoja hiyo haipiti, kulikuwa na habari kuwa SMZ pia ilikuwa imeandaa timu maalumu ya watu wa kuishawishi NEC kuhakikisha kuwa hoja hiyo inapita.
Kampeni za chini kwa chini zilianza kufanywa baada ya wajumbe wa Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar kukubaliana kutokukubaliana kuhusu suala hilo na kuamua kulipeleka mbele ya NEC.
Kikao hicho kililazimika kukaa kwa siku nne mfululizo katika ofisi za CCM Kisiwandui Zanzibar kutokana na malumbano makali yaliyojitokeza baina ya wajumbe waliokuwa wakipinga pendekezo hilo na waliokuwa wakiliunga mkono.
Ingawa kuna habari zilizosema wajumbe wengi wa kikao hicho walikubali Katiba ifanyiwe mabadiliko, wako waliopinga waziwazi kwa maelezo kuwa mabadiliko hayo yatakuwa ni kuirudisha nyuma Zanzibar katika nyanja za kidemokrasia.
Kutokana na msimamo huo na mvutano mkali uliokuwapo, iliamuliwa kuwa kikao cha NEC ndicho ambacho kingetoa uamuzi wa mwisho kuhusiana na mabadiliko hayo.