Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu aahidi kujenga Kariakoo mpya Kiboriloni

Muktasari:

  • Ahadi hiyo ya kulijenga upya Soko la Kiboriloni kama kituo cha biashara cha kimataifa kama Kariakoo jijini Dar es Salaam, imepokewa kwa matumaini na baadhi ya wakazi wa Moshi, huku wito ukitolewa kwa wananchi kuwapigia kura viongozi wenye maono na uwezo wa kweli wa kuleta mabadiliko.

Moshi. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amewaahidi wakazi wa Moshi kuwa, endapo atachaguliwa kuwa Rais katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, atawajengea soko la kisasa la Kiboriloni lenye hadhi ya kimataifa.

Amesema soko hilo litalingana na Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa ubora na miundombinu, na litawezesha wafanyabiashara wa Moshi kufanya shughuli zao katika mazingira bora, salama na ya kisasa, hatua itakayochochea uchumi wa ndani na kuongeza ajira kwa vijana.

Kwa mujibu wa Mwalimu, ahadi hiyo imelenga kuboresha mazingira ya biashara na kuinua uchumi wa eneo hilo na kusimamia sera ya chama hicho ya kulinda mitaji ya wafanyabiashara wadogo ili wakue.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo, Septemba 6, 2025 katika eneo la soko hilo, Mwalimu ameleleza kusikitishwa kwake na hali duni ya soko hilo la kihistoria, ambalo hapo zamani lilihudumia wateja kutoka mataifa jirani kama Kenya na Uganda.

 "Najua heshima ya soko hili, tulikuwa tunakuja kununua nguo hapa kutoka sehemu mbalimbali. Leo hii soko limekufa, wageni hawaji tena. Naahidi kulijenga soko la kisasa litakalorudisha hadhi ya Kiboriloni na kuvutia wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi," amesema Mwalimu.

"Ahadi ninayowapa, kanichagueni najua historia ya soko hili watu walikuwa wanatoka Kenya na Uganda kuja kununua bidhaa siku wanakuja? Wakati nasoma tulikuwa tunakuja kununua nguo katika soko hili, leo soko limekufa hakuna wageni wanaokuja kununua bidhaa, najua heshima yake.

Kariakoo mpya kujengwa Kiboriloni

“Ahadi ninayowapa watu wa Kilimanjaro, watu wa Kiboriloni na watu mnaofanya biashara katika soko hili, tutakuja kujenga soko la kimataifa hapa, watu watatoka Uganda na Kenya kuja hapa kununua bidhaa kama ilivyokuwa zamani," amesema.


Wito kwa Wananchi

Mwalimu amewahimiza wakazi wa Moshi Mjini kuwachagua pia wawakilishi wa chama hicho kwenye Baraza la Madiwani na bungeni, ili kuhakikisha sera na ahadi za chama hicho zinatekelezwa kikamilifu.

 "Msidanganyike na baadhi ya viongozi wa chama tawala. Wakishachaguliwa huwa mabubu, hawasemei matatizo yenu. Wengine wanaingia bungeni kwa masilahi yao binafsi," amesema.

Amemtaja marehemu Philemon Ndesamburo kuwa alikuwa kiongozi aliyekuwa mfanyabiashara na sauti ya wananchi, akasema taifa linahitaji viongozi wa aina hiyo, waliowahi kuishi na kuelewa changamoto za wananchi na si wale wanaotoa ahadi za “danganya toto” zisizotekelezeka.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Moshi Mjini kupitia Chaumma, Patrick Assenga amesema jimbo hilo limekumbwa na changamoto nyingi, zikiwemo ubovu wa barabara za ndani na uchafu wa mazingira.

"Mji wa Moshi ulikuwa unaongoza kwa usafi, lakini sasa umedorora. Tunahitaji uongozi unaojali mazingira na maisha ya wananchi wa kawaida," amesema Assenga.

Ameahidi kupigania hoja hizo bungeni iwapo atachaguliwa, ikiwa ni pamoja na kuboresha usafi wa mji na miundombinu ya msingi.


Maoni ya wananchi

Alfred Oasso, mfanyabiashara wa ndizi katika soko la Kiboriloni, amesema uboreshaji wa soko utakuwa na tija kwao kwani utawavutia wateja wengi zaidi na kuongeza mapato.

"Msimu wa mvua ni wa mateso, tunafanya biashara kwenye matope. Tunaamini Mwalimu anaweza kuwa mkombozi wetu," amesema Oasso.

Mariam Mbwambo, mfanyabiashara mwingine, amesema sera ya kuboresha soko hilo imewagusa wafanyabiashara wadogo, kwani inaonyesha kuwa mgombea huyo anatambua changamoto zao za kila siku.