Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msajili atengua uteuzi wa wagombea urais ACT-Wazalendo, ADC

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetengua uteuzi wa wagombea wawili wa urais wa Tanzania, Luhaga Mpina wa ACT-Wazalendo na Wilson Elias wa ADC, kwa madai ya ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika mchakato wa uteuzi ndani ya vyama vyao.

Uamuzi huo umetolewa usiku wa jana Jumanne, Agosti 26, 2025 wakati leo Jumatano ni siku ya mwisho ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi kwa nafasi za Rais, Makamu wa Rais, wabunge na madiwani, kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni kesho, kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Agosti 26, 2025 usiku na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu ya Uraia, Abuu Kimario, imeelezwa wagombea hao wamekiuka masharti ya Kifungu cha 4(5)(a) na (b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 baada ya kubainika kuwa uteuzi wao haukufuata misingi ya sheria, katiba na kanuni za vyama vyao.

 “Mchakato wa uteuzi wa ndani ya vyama hivyo uligubikwa na utata na haukuzingatia sheria, jambo ambalo linahatarisha utawala wa sheria, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa,” amesema Kimario.

Ofisi ya Msajili imesema uamuzi huo umetolewa baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na pande husika na kubaini kasoro kubwa katika namna wagombea hao walivyochaguliwa ndani ya vyama vyao.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 6A(2) cha Sheria hiyo, vyama vya siasa vinapaswa kuendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Sheria ya Vyama vya Siasa, pamoja na Katiba na Kanuni za vyama husika.

Msajili amesisitiza uteuzi wa wagombea lazima uwe halali na wa kidemokrasia ili kulinda misingi ya kitaifa.

Kwa uwazi na haki, vyama vya ACT-Wazalendo na ADC vimekabidhiwa barua rasmi za uamuzi huo, pamoja na maelezo ya kina kuhusu hatua na mchakato uliotumika kushughulikia malalamiko yaliyowasilishwa na wanachama wao.

Wakati huohuo, Msajili amepongeza ushirikiano uliotolewa na vyama hivyo katika hatua zote za uchunguzi na uamuzi, huku akivihimiza vyama vingine vyote vyenye usajili kamili kuendelea kuheshimu sheria za nchi na kulinda misingi ya demokrasia, amani na mshikamano wa kitaifa hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.