Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbogwe yaahidiwa shule tano, wazazi wakipewa angalizo

Muktasari:

Utambulishio wa Jesca Magufuli, mgombea ubunge wa viti maalumu kundi la vijana (UVCCM), waibua shangwe.

Mbogwe. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiwaahidi wananchi wa Mbogwe, mkoani Geita ujenzi wa shule tano, kimewataka wazazi kuhakikisha watoto wote wanaopaswa kuwa shuleni wanapelekwa.

Vilevile, kimewaahidi wachimbaji wadogo wa madini kuwatengea maeneo maalumu ya uchimbaji yaliyofanyiwa utafiti wa kina ili kuwapunguzia adha.

Ahadi hizo zimetolewa leo Ijumaa, Septemba 5, 2025 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Masumbwe, wilayani Mbogwe na mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, alipomwombea kura mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani.

Dk Nchimbi amesema iwapo CCM itapewa tena ridhaa na Watanzania katika uchaguzi mkuu wa Jumatano Oktoba 29, 2025 itatekeleza kwa kasi Ilani ya uchaguzi mkuu 2025/2030.

Amesema miaka mitano ijayo wilayani Mbogwe, huduma za kijamii kama vile afya, miundombinu ya barabara, maji na elimu itaimarishwa, ikiwamo ujenzi wa vituo vipya viwili vya afya na zahanati tano.

"Shule za msingi mpya tano zitajengwa Mbogwe ila watoto wetu waende shule. Kuongeza shule bila watoto kwenda shule hapana. Ndugu zangu pelekeni watoto, shughuli za madini iwe baadaye. Mhakikishe watoto wanasoma," amesema.

Akizungumzia madini amesema: "Tunakwenda kutenga maeneo maalumu ya wachimbaji wadogo kwa sababu hawa wanakwenda kuwa wachimbaji wakubwa na ndio wanaichangia jamii, Taifa na chama chetu."

Amesema ilani ya uchaguzi ya CCM inaeleza watafanya utafiti ili wajue kuna madini ili wakipewa kunakuwa na uhakika wa asilimia 50.

Dk Nchimbi amesema watalindwa kwa kubadili sera na sheria ili madini ya kimkakati yachimbwe na wazawa.

"Ili kuwalinda Watanzania ni lazima kuzibadili sheria na sera kwamba, mwekezaji kutoka nje lazima ashirikiane na mzawa na hili tutalisimamia kwelikweli. Serikali ya CCM haitakubali tena. Tutaongeza thamani ya madini yetu. Tunataka kuwa na kituo kikubwa Afrika Mashariki," amesema.

Alichokisema Biteko

Katika mkutano huo, mgombea ubunge wa Bukombe, Dk Doto Biteko, ambaye ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, amesema watu wa Mbogwe kwa asili ni watulivu, wakikubaliana jambo wanafanya vizuri na Oktoba 29 wajitokeze kwa wingi kupiga kura.

Dk Biteko ambaye katika uchaguzi huo atapigiwa kura ya Ndiyo na Hapana kwa kuwa yuko pekee jimboni humo amesema: "Uchaguzi huu siyo wa majaribio. Unahusu maisha yetu, afya yetu, elimu yetu na maisha ya kila mmoja. Hatuna shaka na ushindi wa CCM.”


Umoja, amani

Katibu wa Oganizesheni wa CCM, Issa Gavu Ussi amesema chama hicho kimejiandaa.

"Tumejipanga kuipeleka nchi mbele kimaendeleo. Tunawaomba muendelee kutuunga mkono kwa kutunza umoja, amani na ushirikiano."

Gavu ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Geita amesema: "Tumekuja na ilani ambayo ni mkataba baina yetu sisi CCM na wananchi kwamba, mambo tuliyoyaanda yanakwenda kutekelezwa na yaliyomo kwenye ilani siyo porojo."

Amesema ilani hiyo inaonyesha jinsi gani CCM ilivyojipanga kuitumia vyema ardhi.

"Mkitupa ridhaa, tutahakikisha ardhi inatumika vyema kwa kupanga vizuri maeneo ya makazi, kilimo, wafugaji na uwekezaji,” amesema.

Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila amesema wamejiandaa kwa ajili ya uchaguzi, akihimiza kampeni za kistaarabu.

Amesema watahakikisha ushindi wa halali, wa kishindo na mweupe unapatikana.


Upepo wa Jesca Magufuli

Moja ya watu wanaoibua shangwe pindi wanapopewa fursa ya kuzungumza ni mgombea ubunge wa viti maalumu kundi la vijana (UVCCM), Jesca Magufuli.

Jesca, mtoto wa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli kila akiitwa pamoja na wagombea wengine wa ubunge wa eneo husika, ukawadia wasaa wa yeye kuzungumza shangwe huibuka.

Katika mikutano ya Dk Nchimbi mkoani Shinyanga na sasa Geita, Jesca amekuwa kivutio. Mara nyingine amekuwa wa mwisho kujitambulisha.

Anapojitambulisha: "Mimi ni Jesca John Magufuli." Shangwe huibuka kama ambavyo leo pia imetokea Mbogwe alikowaomba wananchi kuendelea kukiamini chama hicho na kukichagua kwa kura nyingi wakati wa uchaguzi Oktoba 29.

Baada ya kuzungumza, Dk Nchimbi amesema Samia amehakikisha ameendeleza miradi ambayo Dk Magufuli aliiacha na ameimaliza.

"Jesca anasimama kifua mbele kwa sababu kazi aliyoanzisha Rais Magufuli inakwenda mbele," amesema Dk Nchimbi.