Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Marufuku kuguna, kushangilia watiania wakiwaomba kura

Wajumbe wa CCM, Kata ya Segerea, Wilaya ya Ilala wakiwa katika mkutano wa kuwasikiliza watiania wa Ubunge na Udiwami wa Jimbola Segerea.

Muktasari:

  • Watiania wa CCM wapo katika mchakato wa kutambulishwa na kuomba kura kwa wajumbe ngazi ya Kata ambapo upigaji kura unatarajiwa kufanyika Agosti 4, 2025.

Dar es Salaam. Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Segerea, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, Fatma Lomo, amewapiga marufuku wajumbe kuguna, kucheka au kushangilia wakati wa kuwasikiliza watia nia wakijinadi  kwao kuomba kuchaguliwa na chama  kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu unaofanyika Oktoba 2025.

Fatma ameyasema hayo leo Ijumaa Agosti 2, 2025 wakati wa kuwatembeza wagombea ubunge na udiwani wa Jimbo hilo katika Kata za Segerea na Liwiti, utaratibu ambao amesema utakuwepo kwa Kata zote mpaka shughuli hiyo itakapoisha.

"Ndugu wajumbe niwatahadharishe ni marufuku kuguna, kucheka au kushangilia pindi wagombea wanapokuja hapa mbele kujinadi na kwa atakayefanya hivyo hatutasita kumtoa nje," amesema msimamizi huyo.

Awali, watia nia hao Ubunge  wakijinadi  mbele ya wajumbe kwa nyakati tofauti  akiwemo Rajab Amir amesema endapo atachaguliwa  atakwenda kutengeneza miundombinu ya barabara kwa kuwa ni tatizo sugu katika Jimbo la Segerea.

Pia, Amir amesema anakwenda  kutengeneza mahusiano mazuri kuanzia ngazi ya shina ,tawi hadi Kata na kujenga nguvu ya pamoja ambayo itasaidia kuwaletea wananchi maendeleo.

"Nchi ina majimbo 272, hivyo Segerea inahitaji mtu makini wa kwenda kuwasemea bungeni na niwaahidi kazi hiyo mkinichagua mimi naiweza," amesema Amir.

Kwa upande wake, Aidani Kwezi  amesema hajaenda hapo kuzungumzia changamoto za barabara kwa sababu anazijua kwani alishawahi kuwa ndani ya Halmashauri isipokuwa anachohitaji wampe nafasi kuweza kwenda  kuzishughulikia.

Hata hivyo Kwezi amesema katika michakato ya uchaguzi anaelewa kuna mambo mengi kikubwa wawe makini kumchagua anayefaa.

"Najua uchaguzi ni gharama  na kwa kipindi hiki  huwa kunakuwepo na bakshishi lakini mnachopaswa kuangalia ni uwezo, utashi na mtu atakayekuja kulikomboa Jimbo la Segerea," amesema Kwezi.

Kwa upande wake Nyimadi Yange, amesema kipaumbele chake cha kwanza ni elimu kwa vijana ambapo kama atachaguliwa atakwenda kujenga chuo cha mafunzo ili kufanikisha hilo.

Pia, Yange amesema Katika Jimbo hilo anajua kuna changamoto ya upatikanaji wa maji na kubambikiwa bili, suala ambalo akifika bungeni atahakikisha analikomesha.

Katika Kata hizo walizopita watia nia, kilio kikubwa cha wajumbe kimeonekana kuwa ni ubovu wa  barabara na upatikanaji uhakika maji ya uhakika.