Karamagi: Tuache makundi CCM inataka ushindi
Muktasari:
CCM imezindua rasmi kampeni za uchaguzi jimbo la Missenyi mkoa Kagera, mgombea Ubunge jimbo hilo Frolente Kyombo anayetetea kiti chake akisisitiza kukamilisha miradi ya maendeleo iliyobaki kiporo huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera akisisitiza wanachama kuacha makundi.
Bukoba. Mgombea ubunge Jimbo la Missenyi Mkoa Kagera kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Frolente Kyombo ameahidi kukamilisha miradi ya maendeleo iliyosalia kipindi chake kilichopita.
Akizungumza Septemba 5, 2025 katika uzinduzi wa kampeni hizo Kyombo amewaeleza wananchi kuwa akipewa ridhaa ya kuwa mbunge kwa kipindi cha pili atahakikisha anasimamia miradi yote iliyobaki kiporo ya CCM inakamilika.
"Nasisitiza tahakikishe ile miradi yote iliyopo kwenye ilani ya CCM iliyokuwa inatekelezwa jimbo hili inakamilika kwa wakati chini ya uongozi wa mama yetu Samia Suluhu Hassan. Najua Missenyi kwenye sekta ya umeme, maji na barabara bado tunahitaji kukamilisha miradi yote," amesema.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, Karim Amri amewaomba wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanawafikia wananchi kwa kushiriki kampeni kwenye kata mbalimbali ili kutafuta kura za mgombea urais, wabunge na madiwani ili kukiwezesha chama hicho kupata ushindi wa asimilia 100.
"Dk Samia ameamua kujitoa kwa ajili ya Watanzania, tafuteni kura zake kila mahala ameleta maendeleo makubwa na miradi mikubwa Tanzania nzima sasa ni wakati wa kulipa deni," amesema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kagera, Nazir Karamagi amesisitiza kuvunja makundi ndani ya chama ambayo hayana sababu na kuendelea kitafuta kura za wagombea wote.
"Kwenye kura za maoni ndani ya chama mkoa Kagera hasa Missenyi kulikuwepo chokochoko nyingi na maneno mara huyu amenikanyaga mara amenichokoza, ila sasa tambua muda huo umeisha tusimame imara pamoja kutafuta ushindi kwenye urais, ubunge na udiwani," amesema.
Karamagi, amesisitiza kuwa ilani ya CCM imetekelezek,a hivyo ni wakati wa kumpatia nafasi tena Samia kuwa Rais maana kila unapopita nchi nzima kuna alama yake ya miradi.