Catherine Ruge: Nitaboresha kilimo, elimu na maisha ya Serengeti
Muktasari:
- Mgombea wa nafasi ya urais kupitia Chaumma, Salum Mwalimu amewaahidi vijana wanaoishi kando na hifadhi ya Taifa ya Serengeti neema ya ajira
Mara. Mgombea ubunge wa Serengeti kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Catherine Ruge amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi, atahakikisha anaboresha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia fedha za ndani ili kuhakikisha wananchi wanapata mavuno ya tija ili wajikwamua kiuchumi.
Katika upande wake, mgombea wa nafasi ya urais kupitia Chaumma, Salum Mwalimu amewaahidi vijana wanaoishi kando na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti neema ya ajira.
Akizungumza leo Septemba 9, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Mugumu, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Catherine amesema rasilimali ardhi yenye rutuba tayari ipo, hivyo miradi ya kilimo cha umwagiliaji inaweza kufanikishwa kwa vitendo.
“Watumishi wa halmashauri wajiandae kukesha kwenye miradi, siyo kushinda ofisini. Serengeti ni kipaumbele changu,” amesema Catherine huku akisisitiza ushiriki wa wananchi wote katika utawala bora.
Ameahidi pia kutoa elimu ya ufugaji wa kisasa kwa jamii ya wafugaji, pamoja na kuleta wataalamu wenye ujuzi kuwapa mafunzo na mbinu bora za ufugaji.
Katika hatua nyingine, Catherine amesema ataanzisha mfuko wa mikopo uitwao "Mshubati" kwa ajili ya vijana na watapatiwa mikopo yenye riba nafuu ili waweze kujiajiri kupitia biashara mbalimbali.
Kwa upande wa elimu, ameahidi kukarabati shule chakavu ili kuwapa wanafunzi mazingira bora ya kujifunza.
Katika hatua nyingin, amesema miradi ya miundombinu kama barabara za Mugumu-Bunda na Mugumu-Nata itaendelezwa ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kibiashara.
Pia, amesisitiza kuwa yeye ni mgombea sahihi kwa sababu anazijua changamoto za wananchi wa Serengeti na yuko tayari kuwa kipaza sauti chao bungeni.
“Licha ya kuwa karibu na Hifadhi ya Serengeti, wananchi wake ni maskini. Tunahitaji mtu wa kutupeleka kwenye utajiri wa rasilimali zetu,” ameongeza.
Akiwasilisha malalamiko ya wananchi wanaopoteza maisha kutokana na migogoro na wanyamapori, Catherine amesema anataka kwenda bungeni kutetea haki ya kuishi ya wananchi, akieleza kuwa wengi wamepoteza ndugu zao bila msaada wowote wa fidia.
Ahadi za Mwalimu
Mgombea urais kupitia Chaumma, Salim Mwalimu amesema umaskini wa wananchi wa Serengeti ni matokeo ya “mateso ya makusudi,” na kuahidi mabadiliko makubwa endapo atachaguliwa.
“Hifadhi si laana. Nitapiga marufuku ongezeko la maeneo ya hifadhi,” amesema Mwalimu.
Ameahidi kulipa fidia kwa wote waliopata ulemavu au kupoteza wapendwa wao kutokana na migogoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Serikali yake itaweka mkakati wa ajira kwa vijana wa maeneo ya jirani na hifadhi zote nchini.
“Ajira 200 zitakapotangazwa, asilimia kubwa itanufaisha wazawa wa Serengeti,” amesema.
Kwa jamii ya wafugaji, Mwalimu ameahidi kutengeneza sera ya maeneo ya malisho ya uhakika na kuunda tume ya kushughulikia migogoro ya ardhi ili kuhakikisha haki za wafugaji zinalindwa kwa mujibu wa sheria na mazingira.
“Haiwezekani kuzuia wafugaji kwenda kwenye malisho ya Mungu. Nitahakikisha matumizi ya ardhi yanawekewa utaratibu rafiki,” amesisitiza.