Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ahadi ya ajira AAFP yavipiku vyama vyote

Muktasari:

  • Ahadi hii ya kuzalisha ajira milioni 15 si tu inavizidi baadhi ya vyama vya upinzani vinavyoshiriki katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025, imeipiku hadi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya ajira milioni 8.

Moshi. Kama ni ilani ya uchaguzi inayokuja na uzalishaji wa ajira nyingi basi ni ya Alliance for Africa Farmers Party (AAFP), Chama cha Wakulima, ambacho kupitia ilani yake ya miaka mitano (2025-2030), kimeahidi kuzalisha ajira milioni 15.

Ahadi hii si tu inavipiku vyama vya upinzani vinavyoshiriki katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025 na hata Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachotawala, ambachokilichoahidi ajira milioni 8.

Lakini kubwa zaidi ndani yake, ni ahadi yake ya kuanzisha ofisi ya mkandarasi wa ndani chini ya Jeshi la Maendeleo katika wilaya zote nchini, ambako vijana wote wanaomaliza kidato cha nne wanapata ajira katika ofisi hiyo.

Hii ni kwa vijana ambao watashindwa kuendelea na ngazi inayofuata ya kidato cha tano na sita na vyuo vya kati, lengo likiwa ni kuwapa maarifa na ujuzi.

Jeshi la Maendeleo, ni jeshi namba mbili ambalo AAFP imeahidi kulianzisha ikishika madaraka, baada ya kuligawanya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuunda jeshi namba moja mahsusi kwa ajili ya ulinzi wa nchi na jeshi namba mbili la maendeleo.

AAFP katika ilani yake, inasema kutokana na changamoto za ajira na kujiajiri kwa wananchi, itailekeza Serikali yake kuzalisha fursa ya ajira mpya milioni 15 – zisizo rasmi na ajira rasmi katika sekta mbalimbali ikiwamo sekta ya kilimo.

Ili kufikia ndoto hiyo, kitaweka masharti nafuu kwa wawekezaji wazawa na wa kigeni, kushrikiana na sekta binafsi na kuweka vijana wote waliomaliza vyuo vya kati na vyuo vikuu katika ajira rasmi na zisizo rasmi kwa ajili ya uzalishaji mali.


Elimu mkakati kwa vijana

Kupitia ilani yake hiyo, chama cha AAFP kitaiagiza Serikali kuweka utaratibu kisheria ili shule zote za sekondari kuanzia kidato cha kwanza na kuendelea mpaka vyuo vya kati, zibadilishwe na kuwa shule za ufundi na uzalishaji mali.

Vyuo vikuu pekee ndio vitaendelea na mfumo wake wa utoaji elimu lakini kitaagiza Serikali yake iweke utaratibu wa kugawa shule katika makundi kwa kuzingatia vipawa na ufundi wa fani mbalimbali kama itakavyoonekana inafaa.

Lengo lake ni kuwezesha wanafunzi kugawanywa katika mafunzo ya kujenga stadi na uzalishaji mali kadri itakavyowezekana.

Vyuo vikuu na vyuo vya kati vitasimamia kuzalisha wataalamu watakaopewa nafasi ya kuchochea mafunzo katika shule za sekondari na katika uboreshaji wa viwanda, mashambani na masuala yote ya sekta mbalimbali bunifu nchini kote.


Uzalishaji mashambani

Katika ilani hiyo, AAFP inakusudia kuanzisha mashamba makubwa ya mazao ya biashara kama vile pamba, korosho, kahawa, mpunga, mahindi na alizeti katika kila wilaya, ikizingatiwa kilimo kinaajiri karibu asilimia 80 ya Watanzania.

Pia, kitaimarisha sekta ya uvuvi kwa kuanzisha utaratibu kila wilaya yenye uvuvi kuhakikisha kunajengwa kiwanda au viwanda vidogo vya kusindika samaki.

Mbali na mikakati hiyo, AAFP inapanga kufufua viwanda vyote vya mazao ya mifugo, hasa vya ngozi, na kuanzisha viwanda vipya vidogo vidogo vya uchakataji ngozi wilaya zote zenye mifugo ili kuongeza ajira kwa vijana ambalo ni tatizo la muda mrefu.

Chama hicho kimeahidi pia kuanzisha mpango maalumu wa uagizaji wa mashine ndogondogo za usindikaji wa mazao na kuanzisha utaratibu kisheria wa masoko maalumu katika wilaya zote nchini ambayo yatakuwa chachu ya maendeleo.

Masoko hayo, AAFO inasema yatatumika kuuzia mazao yaliyoongezewa thamani na masoko hayo yatajulikana kama vituo vya biashara wilaya na kwa mpango huo maalumu katika wilaya zote, itahakikisha masoko yanazalisha ajira mpya 5,000.


Ukusanyaji wa kodi

Katika eneo hili la ukusanyaji wa kodi, Serikali ya AAFP itakuwa na kaulimbiu “kadiria kidogo kusanya zaidi” na ushuru rafiki kwa wafanyabiashara wa ngazi zote.

Ni kwa msingi huo, AAFP itaielekeza Serikali yake kuweka viwango rafiki vya kodi mbalimbali ili kuongeza hamasa kwa walipakodi inayowawezesha kulipa zaidi bila usumbufu kwa kwa hiyari na katika kutimiza lengo hilo itaweka viwango nafuu.

“Tutakikisha viwango vinakuwa nafuu na mifumo ya kodi inazingata hali ya unafuu kwa mwananchi a ili kuongeza ari ya kufurahia kulipa bila kusukumwa kwa kila mwananchi anaepaswa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu,” inasema.

“Tutaweka kodi ya mapato shirikishi ya muungano kwa Zanzibar na Tanzania bara kwa utaratibu unaoitaka kodi shirikishi ya muungano ikilipwa Zanzibar haipaswi tena kulipwa Tanzania bara na vilevile ikilipwa bara haipaswi kulipwa Zanzibar.”

Kadhalika, AAFP inasema ili Tanzania iweze kukua kiuchumi kwa upande wa muungano, kinakusudia kuimarisha Zanzibar kwa kuielekeza Serikali yake kuwa na kituo cha kibiashara kitaifa na kuwa na kituo cha utalii katika pwani ya Mashariki.


Ajira milioni 15 zinawezekana

Akizungumzia suala la ajira, mhadhiri mwandamizi katika Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam, Dk Riziki Nyello amesema kutengeneza ajira kwa mamilioni inawezekana endapo nchi itaongeza thamani ya bidhaa inazozalisha.

“Badala ya kupeleka nje bidhaa ghafi, ziongezewe thamani hapa nchini,” amesema.

Dk Nyello amesema mkakati mwingine ni kuongeza mnyororo wa thamani ambayo mwisho wa siku huongeza ajira na kutolea mfano bidhaa za nyuki inavyoweza kuzalisha asali, gundi na mishumaa (organic candle) na kuongeza ajira.

Mkakati mwingine ni matumizi ya teknolojia kwamba nayo inaajiri watu wengi sasa na kutolea mfano kuwa mtu ana parachichi Njombe kwamba anaweza kumuuzia mtu aliyepo Dar es Salaam na kuibua uchumi wa kidigitali.

Dk Nyello amesema hiyo inaenda kuzalisha watu wa kati (middlemen) ambao wao hawana bidhaa, lakini ana simu janja, anasimama kuuza bidhaa ya mtu mwingine na hao ni wengi wako kwenye mitandao wakiuza bidhaa ambazo sio zao.

Kwa upande wake, Emiliana Massawe ambaye ni mtaalamu wa uchumi, amesema vyama vinakuwa na mikakati na maneno mazuri katika ajira, lakini hakuna mifumo ya kupima kama kweli katika miaka mitano imezalisha ajira hizo milioni 15.

“Kutoa ahadi ni jambo moja na kutekeleza ni jambo lingine. Lakini tunapimaje ufanisi wa ajira wakati mitaani hali ni tofauti? Mimi nadhani tukiwekeza kwenye kilimo, zaidi ninaamini huko ndio kuna ajira ambazo unaweza kuzipima.

“Nimeona wanazungumzia kuweka mazingira mazuri ya kodi. Ni sawa, lakini mimi ukiniuliza naona tunakusanya vyanzo vilevile na kuwabebesha mzigo wananchi. Hivi Tanzania tunapata mapato kiasi gani kwenye uvuvu baharini?” amehoji.

Mwalimu Evarist Mbogo amesema tatizo kubwa la nchi yetu katika shule za umma ni utoaji wa elimu isiyo bora lakini pia inafundisha zaidi wanafunzi kuwa na fikra za kuajiriwa, wakati hata hao wanaofundishwa ufundi, hawawezeshwi kujiajiri.

Mathalan, amesema wanafunzi wanaweza kupewa elimu ya ujasiriamali au kilimo na Serikali inapaswa iwajengee mazingira ya kupata mitaji ya kujiajiri, ili baadaye nao waweze kuajiri wengine na kwa kufanya hivyo mnyororo wa uchumi unaongezeka.