NLD inavyotafsiri Dira 2050 kwenye ilani yake ya uchaguzi
Muktasari:
Chama cha National League for Democracy (NLD) kimetoa ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2025. Ilani hiyo inatengeneza mfumo mbadala wa kifikra, kiuchumi na kijamii, unaotaka kuchochea mabadiliko ya kielimu, teknolojia, ajira na uchumi wa wananchi.
Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakitarajia kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025, vyama vya siasa vinaendelea kukimbizana katika maandalizi, ikiwemo kusimamisha wagombea na kuzindua ilani za uchaguzi.
Tofauti na miaka mingine, mwaka huu si ahadi tu zinapimwa, bali pia uwezo wa vyama kusoma alama za nyakati na kuandaa ilani zinazojibu maswali ya msingi ya jamii ili kushawishi wananchi wawapigie kura.
Tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipozindua Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 jijini Dodoma Julai 13, 2025, ambayo inalenga kulifanya Taifa kuwa la uchumi wa kati wa juu, shirikishi na jumuishi, swali limekuwa ni namna gani vyama vya siasa vitatafsiri maudhui ya dira hiyo kwenye ilani zao za uchaguzi.
Katika mkondo huo, Chama cha National League for Democracy (NLD) kimetoa ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2025 inayotengeneza mfumo mbadala wa kifikra, kiuchumi na kijamii ambao unalenga kuchochea mabadiliko ya kielimu, teknolojia, ajira na uchumi wa wananchi.
Ilani hiyo imeainisha vikwazo mbalimbali vinavyotakiwa kutatuliwa ili kuchochea maendeleo ya Taifa na ya mtu mmoja mmoja. Ukosefu wa ajira hasa kwa vijana wa vyuo vikuu na kati ni miongoni mwa mambo yaliyopewa nafasi kwenye ilani ya chama hicho.
Pia, chama hicho kimedhamiria kushughulikia elimu isiyoendana na soko la ajira na teknolojia ya kisasa, endapo kitapewa dhamana ya kuongoza Serikali.
Mambo mengine yanayomulikwa na chama hicho kwenye ilani yake ni kushughulikia changamoto za kilimo cha kujikimu kisicho na tija, upungufu wa huduma za maji safi na salama, rushwa sugu na ukwepaji kodi.
Pia, ilani hiyo imemulika mfumo wa kodi usio wa haki unaowakandamiza wajasiriamali wadogo, ubaguzi wa kijinsia na mimba za utotoni.
NLD kimeeleza pia kutambua na kuwezesha sekta binafsi ipasavyo, ili kutoa mchango wake katika maendeleo ya Taifa pamoja na kuimarisha usimamizi madhubuti wa rasilimali za madini.
Ilani hiyo imegusia maeneo kadhaa na kuweka mbinu madhubuti za usimamizi wake, mambo ambayo yana tafsiri pana inayoendana na mwelekeo wa Dira 2050.
Elimu bure, bora na ya kisasa
Kwa mujibu wa Dira 2050, Tanzania mpya itajengwa juu ya msingi wa watu wenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kujitegemea. Hapa ndipo NLD inaweka nguzo yake ya kwanza ya kimapinduzi: elimu huru na yenye vitendo.
Ilani hiyo inaahidi elimu bure hadi kidato cha sita na vyuo vya kati vya umma, lakini zaidi ya hilo, inarekebisha mitaala ili iandaliwe kulingana na mahitaji ya soko la ajira la leo na la kesho.
Masomo ya Tehama, ubunifu, maarifa ya fedha, stadi za maisha na lugha za kigeni yanaelezwa kuwa silaha ya ukombozi wa kizazi kipya. Kwenye jamii ambayo mitaala imekuwa kama mzigo wa nadharia za darasani.
NLD inataka elimu inayomfanya kijana ajitambue, ajiajiri na atoe mchango wake wa maarifa katika ujenzi wa Taifa.
“Kijiji Moja, Bidhaa Moja”
Katika nyakati ambapo uchumi wa dunia unapiga hatua kwa kasi huku Tanzania ikibakia kuwa tegemezi wa bidhaa za nje, NLD inaweka mezani falsafa ya uchumi wa ndani kwa jina la “Kijiji Moja, Bidhaa Moja”.
Katika kila kata, kiwanda kidogo kitazalisha bidhaa kulingana na rasilimali asilia, kuondoa pengo kati ya mzalishaji na soko.
Dira 2050 inataka uchumi shindani wa viwanda na NLD inaleta hoja yenye jibu: viwanda vya wananchi, kwa wananchi. Hapa ndipo sera ya viwanda haibaki kwenye makabrasha ya wizara, bali inafika katika mikono ya mzalishaji moja kwa moja.
Ajira si fadhila, ni haki
Katika Taifa ambalo vijana ndio zaidi ya nusu ya wakazi, ukosefu wa ajira umekuwa kama ukuta unaowatenga na ndoto zao. NLD kupitia mpango wa ‘Vijana kwa Kazi’, inasema wazi: “ajira si hisani, ni haki ya kizazi kinachozalisha.
Kupitia mafunzo ya vitendo ya miezi sita hadi 12 kwa wahitimu wote, vijana wataingia sokoni wakiwa wameiva sio kutangatanga na vyeti mikononi bila matumaini.”
Zaidi ya hayo, Ilani ya NLD inaeleza uanzishaji wa Mfuko wa Taifa wa Uwezeshaji wa Vijana ambao utatoa mikopo isiyo na riba na vituo vya mjasiriamali kwa kila halmashauri.
Kwa maneno mengine, chama hicho kinavunja mnyororo wa kutegemea ajira serikalini na kujenga kizazi kinachotengeneza ajira kwa wengine.
Utawala bora
Wakati Dira 2050 ikitoa msisitizo wa ujenzi wa taasisi thabiti na uwajibikaji wa kweli kwa watendaji, NLD inakuja na mapendekezo ya kuundwa kwa Tume Huru ya Kupambana na Rushwa isiyohusiana na uteuzi wa kisiasa.
Pia, inataka matumizi ya fedha za umma yawe wazi kwa wananchi kupitia mifumo ya kidigitali.
Haya si maneno mepesi, ni vita vya darasani dhidi ya tabaka la ufisadi. Huu ndio msingi wa utawala unaosimama upande wa wananchi, na si kwa ajili ya kulinda marupurupu ya wachache.
Huu ni msingi muhimu ulioainishwa katika Dira 2050 ambayo inasisitiza uwajibikaji, kukomesha rushwa na uzembe kwa watumishi wa umma.
Uchumi wa kijani
Katika zama za mabadiliko ya tabianchi, Dira 2050 inalenga kuijenga Tanzania kama taifa la kizalendo na kiikolojia linalotunza mazingira na utajiri wa asili kwa masilahi ya leo na ya kesho.
NLD inavuka mipaka ya ahadi za kawaida kwa kuona umuhimu wa kuwekeza kwenye nishati jadidifu, sola, upepo na bayogesi na kupiga marufuku ukataji wa misitu bila kibali.
Pia, chama hicho kinataka kila kijiji nchini kiwe na umeme salama kwa kutumia teknolojia mbadala.
Muhimu kufuata dira
Wataalamu wa masuala ya siasa na utawala bora nchini wamesema chama cha siasa kina wajibu wa kuhakikisha sera zake zinajengwa katika msingi unaoendana na Dira ya Taifa ili kikipata ridhaa ya kuongoza nchi kisiitoe jamii kwenye mwelekeo iliyojiwekea.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema ilani za vyama vya siasa zinapaswa kuibeba mikakati inayotekelezeka, hasa katika kutatua changamoto zinazolikabili Taifa ikiwemo changamoto ya ajira kwa vijana.
“Tatizo la ajira linaongelewa sana na kila mtu huku changamoto ikibaki kwenye mikakati, badala ya maneno matupu chama lazima kijue kinakuja na lipi jipya ambalo litatekelezeka na kuondoa tatizo hili,” amesema.
Ameongeza kuwa tatizo la ajira kwa vijana halihusiani na muundo wa mitaala ya elimu kama wengi wanavyofikiri, bali ni ukosefu wa fursa ambazo zinatakiwa kutengenezwa.
“Kikubwa katika suala la ajira ni fursa na si mitaala ya elimu, fursa zinazozalisha ajira zitengenezwe,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Profesa Mohammed Makame amesisitiza kuwa changamoto zilizopo si zote ni za kisiasa, bali zinagusa nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu.
Yeye anatoa wito kwa vyama vya siasa ikiwemo NLD kutumia fursa ya wadau wa maendeleo, ushirikishaji wataalamu na jamii nzima ili kila mmoja ahusike kwa nafasi yake katika kutatua changamoto ambazo zipo katika nafasi yake.
“Matatizo yanayoikabili nchi yetu si yote ni ya kisiasa, ni vema vyama vya siasa katika ilani zake, pamoja na mambo mengine, waone pia umuhimu wa kuweka namna ya uhusishaji wadau wa maendeleo, wataalamu, wachumi na jamii nzima ipewe nafasi,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Dk Richard Mbunda ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia amesisitiza chama cha siasa kinapaswa kuandaa ilani yake kwa kuzingatia mwelekeo wa Taifa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo.
“Dira ya Taifa ni mwelekeo wa nchi, hivyo ilani za vyama vya siasa zinapaswa kusukwa kuendana na mwelekeo huo, ili kufikia matamanio ya Taifa.
Chama kisipokuja na ilani inayoendana na Dira ya Taifa, kikipewa nafasi ya kuongoza Taifa halitafikia malengo yake,” amesisitiza mtaalamu huyo wa masuala ya siasa na utawala bora.