Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

AAFP kuja na baraza dogo la mawaziri kubana matumizi

Muktasari:

  • Wadau wasema hatua hiyo ni ya lazima kwa kuondoa mzigo usio na tija kwa wananchi. Pia, chama hicho chaahidi kusimamia vyanzo vya mapato, kuboresha huduma za afya, kutoa bima bila malipo, kutoa ajira kwa madaktari, na kuhakikisha mwananchi ana kipato cha angalau Sh20,000 kwa siku.

Moshi. Chama cha Alliance for Africa Farmers Party (AAFP), kupitia ilani yake ya miaka mitano (2025-2030), kimekuja na ahadi ya kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali, ikiwamo kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri.

Suala la kubana matumizi ya Serikali limekuwa kilio cha muda mrefu kutoka kwa baadhi ya wabunge, wanaharakati, viongozi wa dini na wananchi, hoja hiyo ilitikisa pia wakati wa kukusanya maoni ya Katiba mpya 2013.

Kulingana na takwimu, Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa, Jullius Nyerere ndio iliyovunja rekodi kwa kuunda Baraza dogo la Mawaziri mwaka 1961 lililokuwa na mawaziri 11 pekee na nchi haijawahi kuvunja rekodi hiyo.

Serikali ya awamu ya pili chini ya Ali Hassan Mwinyi ilipoingia madarakani mwaka 1985, aliunda baraza lenye jumla ya mawaziri 31. Kulikuwa na mawaziri 23 na manaibu wanane, huku mrithi wake, Benjamin Mkapa mwaka 1995 alianza na mawaziri 27 na manaibu 10.

Mwaka 2005, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliingia na baraza lenye mawaziri 60, ambapo mawaziri kamili walikuwa 29 na manaibu 31, lakini alipofanya mabadiliko ya kwanza makubwa mwaka 2008, baraza lilishuka hadi 47.

Kwa upande wake, Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli alipotangaza baraza lake la kwanza la mawaziri mwaka 2015 lilikuwa na jumla ya wizara 18 ambapo manaibu waziri walikuwa 34, ingawa baadhi ya mawaziri waliteuliwa baadaye.

Lakini hoja ya wananchi katika matumizi makubwa ya Serikali hayaishii tu kulalamikia ukubwa wa baraza la mawaziri, bali pia matumizi makubwa hasa katika ununuzi na matumizi ya magari, hugharimu zaidi ya Sh500 bilioni kila mwaka.

Katika hotuba yake ya bajeti kwa mwaka 2022/2023, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali hutumia Sh558.4 bilioni kila mwaka kwa ajili ya kununua magari, mafuta, vipuri na matengenezo ya magari.

Mwigulu alisema Serikali ina magari 15,742, pikipiki 14,047 na mashine 373 na kupendekeza utaratibu wa kuyahudumia ubadilike na badala yake watendaji wenye sifa wakopeshwe magari ili gharama za matengenezo ziwe juu yao.


AAFP na kubana matumizi

Kutokana na kilio hicho cha wananchi cha kutaka Serikali ipunguze gharama za uendeshaji, chama cha AAFP, kupitia ilani yake ya 2025-2030, kimeahidi kufanya marekebisho ya muundo wa Serikali ikiiingia madarakani.

“Kwa kuwa muundo uliopo umekuwa na mlundikano wa madaraka na kusababisha matumizi makubwa ya rasilimali fedha ya kawaida kuliko ya maendeleo ya wananchi, hivyo AAFP kitaielekeza Serikali yake kufanya mambo mambo matatu.

"Mambo hayo ni kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri, kuondoa wakuu wa mikoa na makatibu tawala (RAS) nchi nzima na kuondoa wakuu wa wilaya na makatibu tawala na majukumu kuyapeleka kwa mameya wa wilaya," imeeleza sehemu ya ilani hiyo.


Walichokisema wadau

Mchambuzi wa masuala ya kisheria na kisiasa nchini, Dk Rwezaura Kaijage amesema hoja ya kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri ni jambo linalowezekana kwa sababu ni utashi wa Rais aliyepo madarakani, kwa kuwa si nafasi za kikatiba.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU), amesema nafasi za uwaziri hazitajwi kwa idadi kwenye Katiba, hivyo kufanya baraza liwe dogo inavyowezekana isipokuwa nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya zinahitaji mabadiliko ya Katiba.

“Unajua siasa zimetuathiri sana Watanzania. Kuna nafasi ambazo ni kwa mujibu wa Katiba na kwa mazingira tuliyonayo na ambayo tumepitia si rahisi kubadili Katiba haraka haraka, ili kufuta hivyo vyeo vya wakuu wa mikoa na wilaya.

“Lakini kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri hilo naunga mkono kuwa linawezekana ni utashi tu wa Rais. Ukiondoa local government (Serikali za Mitaa) hutaweza kutawala Serikali. Kuna njia nyingine za kubana matumizi,”amesisitiza.

Amani Ngowi, mkazi wa Dar es Salaam na Moshi, ameunga mkono ilani hiyo ya AAFP akisema ukubwa wa baraza la mawaziri halina tija na kuunga mkono kufutwa kwa nafasi za wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchi nzima.

“Wapo sahihi kabisa. Kwenye nchi yetu ukubwa wa baraza hauna tija yoyote wamewekwa mpaka manaibu ila ufanisi ni mdogo. Wakuu wa mikoa na wilaya ni vyeo vya kisiasa zaidi na kulinda watawala hizo nafasi zinatakiwa ziondolewe.”

“Ziondolewe kabisa kuanzia kwenye Katiba ila makatibu tawala wa mikoa na wilaya hao ni watendaji wanaweza kuwa watchdog (walinzi) wa kuangalia kati ya Serikali Kuu na Serikali za mitaa zinafanyaje kazi kwa ufanisi,”ameeleza Ngowi.

Juliana Alex, mama Lishe na mkazi wa Njoro katika Manispaa ya Moshi, ameunga mkono ilani ya AAFP akisema gharama za uendeshaji ni kubwa na mzigo mkubwa unabebwa na wananchi kupitia kodi ambazo zingine si rafiki.

“Mie naunga mkono, hizo nafasi kwa kweli zifutwe ni kuwabebesha mzigo wananchi usio na sababu. Kazi zao zifanywe na wakurugenzi wa halmashauri za majiji, manispaa na miji. Tunabebeshwa mzigo usio na tija,”amesema Juliana.

Mfanyabiashara masiriamali, Renalda Mboro, amesema ukubwa wa baraza la mawaziri na ukubwa wa gharama za kuendesha Serikali ni mambo yanayowabebesha wananchi hivyo ilani ya AAFP anaiunga mkono asilimia 100.


Vipaumbele vingine vya AAFP

Chama hicho kupitia ilani hiyo kimaehidi kuwa kwa kuwa huduma afya katika nchini Tanzania, limekuwa na changamoto nyingi kwa wananchi, hivyo kitaiagiza Serikali yake kuhakikisha inafanya mambo makubwa matatu muhimu.

Moja ni kusimamia vyema vyanzo vyote vya mapato ya nchi katika sekta zote kama vile za nishati, madini, maliasili, kodi, kilimo, biashara na nyinginezo ili kuwezesha kufanya maboresho ya miundombinu ya afya nchini Tanzania.

Mbali na hilo, pia itagharamia vifaa tiba na huduma za matibabu, kuwapatia wananchi wote bima ya afya bila malipo na kuhudumia wananchi wote na kwamba itatoa ajira kwa madaktari wote waliohitimu taaluma ya udaktari nchini.


Kukuza uchumi wa kujitegemea

AAFP inasema kutokana na uchumi wa Tanzania na mwananchi mmoja moja hauridhishi na ni tegemezi kwa mataifa makubwa ya kimagharibi na kiasia, itaelekeza Serikali kutumia na kusimamia kusimamia rasilimali zote za nchini.

Hii kwa mujibu wa chama hicho itasaidia Serikali kuwa ni vyanzo endelevu vya mapato katika kukuza uchumi wa kujitegemea.

Mbali hilo, itaagiza Serikali kusimamia na kuongeza vyanzo vingine vya mapato kulingana na mazingira ya fursa rafiki na kumwezesha mwananchi kuwa na kipato kisichopungua Sh20,000 kwa siku.