Yanga bado dakika 90 Algeria

Muktasari:

  • Alger ndio imetangulia kupata bao dakika ya 32 kupitia kwa Aimen Mahious lililodumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika kabla ya Fiston Mayele kusawazisha dakika ya 82 lakini Alger wakafunga bao la pili na la ushindi dakika ya 84 kupitia kwa  Islam Merili.

Yanga imepoteza mchezo wa kwanza wa fainali Kombe la Shirikisho Afrika, ikifungwa 2-1 nyumbani uwanja wa Benjamin Mkapa na USM Alger kutoka Algeria.

Alger ndio imetangulia kupata bao dakika ya 32 kupitia kwa Aimen Mahious lililodumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika kabla ya Fiston Mayele kusawazisha dakika ya 82 lakini Alger wakafunga bao la pili na la ushindi dakika ya 84 kupitia kwa  Islam Merili.

Matokeo hayo yameifanya Alger kuwa na faida ya uongozi katika mechi ya marudiano watakayokuwa nyumbani lakini  pia Yanga bado ina nafasi ya kufanya hivyo katika mchezo utakaopigwa Juni 3, mwaka huu.


Mchezo ulivyokuwa


Timu zote zilianza kwa kushambuliana huku kila klabu ikifanya shambulizi moja la hatari katika dakika 10, za kwanza lakini hayakuzaa mabao.

Katika kipindi cha kwanza, mashambulizi mengi ya Alger yamepitia upande wao wa kushoto hivyo hivyo kwa Yanga iliyokuwa ikimtumia zaidi Keneddy Musonda na muda mwingi Fiston Mayele naye alikua huko.

Bao la Aimen Mahious dakika ya 32 kwa kichwa, mpira uliotokana na faulo aliyoicheza Dickson Job kwa winga wa Alger na beki huyo kuoneshwa kadi ya njano ndilo liliwafanya Alger kwenda mapumziko wakiongoza.

Yanga katika dakika 45 za kwanza ilipiga mashuti sita lakini lililolenga lango likiwa moja tu na Alger wakipiga matano, mawili yakilenga lango na matatu kwenda nje.

Licha ya kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao moja lakini Yanga ndiyo imeongoza  kumiliki mpira kuliko wapinzani wake, Alger.

Kadi hiyo ya njano katika kipindi cha kwanza zilitoka mbili, moja ikienda kwa Job wa Yanga na nyingine kwa moja ya mastaa wa Alger.

Kipindi cha pili kimerejea kwa kasi na timu zote zikiendelea kufanya mashambulizi katika nyakati tofauti lakini hadi kufika dakika ya 60 hakuna upande uliokuwa umenufaika na mashambulizi hayo.

Yanga imefanya mabadiliko dakika ya 64 kwa kumtoa Stephane Aziz Ki ambaye hakuwa kwenye kiwango bora na nafasi yake kuchukuliwa  na Salum Abubakar ‘Sureboy’ aliyeingia kuchangamsha eneo la kiungo.

Alger imejibu mapigo ya mabadiliko hayo dakika ya 69 kwa kumtoa Aimen, mfungaji wa bao la kwanza na kuingia Abderrahman Meziane.

Baada ya hapo Yanga imefanya mabadiliko mengine matatu kwa mpigo wakiingia Benard Morrison, Djuma Shaban na Joyce Lomalisa kuchukua nafasi za Tuisila Kisinda, Job na Kibwana Shomari dakika ya 75.

Mayele ameiandikia Yanga  bao la kusawazisha  dakika ya 82 lakini halikudumu kwani Alger imeongeza bao la pili na la ushindi dakika ya 84 kupitia kwa Islam Merili.

Yanga bado inanafasi ya kutwaa kombe hilo kama itajipanga na kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano itakayopigwa nchini Algeria Juni 3 mwaka huu.

Katika mechi hiyo, Yanga itahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0, au zaidi ili kutwaa ubingwa na kama itashinda 2-1 basi bingwa atapatikana kwa mikwaju ya penalti.