Prime
Simba yaanza na mashine 6

Muktasari:
- Simba ilikuwa na kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo kilichoongozwa na Mwenyekiti wake.
Mabosi wa klabu ya Simba katikati ya wiki walitana pamoja na kujadili mambo mbalimbali ya klabu hiyo ikiwamo kupitia ripoti ya kocha Fadlu Davids kwa ajili ya mipango ya kusuka kikosi kipya cha msimu ujao huku wakiafikiana na pendekezo la kocha huyo kuanza na mashine sita mpya.
Simba ilikuwa na kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo kilichoongozwa na Mwenyekiti wake, Mohammed 'MO' Dewji sambamba na viongozi wa zamani ambacho kilikuwa na kazi ya kujadili mambo muhimu ikiwamo tathmini ya msimu uliomalizika na ripoti ya kocha iliyohitaji usajili mzito.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zimelidokeza Mwananchi kuwa, ukiacha tathmini ya msimu uliopita, pia walijadili mipango na maandalizi kwa ajili ya msimu ujao ikiwamo pendekezo la Fadlu la kutaka mashine mpya zisizopungua sita ili kuisuka Simba mpya itakayotetemesha ndani na nje ya nchi.
"Simba imefanya kikao hicho ambacho kitakuwa na mabadiliko katika baadhi ya maeneo ya kiungozi na hata ya kikosi kwa ujumla," kilisema chenzo hicho kutoka ndani ya Simba na kuongeza;
"Kubwa hasa ni kuhusu mahitaji ya kocha ambayo aliyapendekeza kama atasalia ndani ya kikosi na ni uhakika kuwa tutakuwa naye tena na hivyo mahitaji yake lazima yatimizwe."
Kama ilivyoripitiwa jana ni kwamba, Fadlu pamoja na benchi lote la ufundi wamekubali kusaini mikataba mipya ya mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongezwa mwaka mwingine, baada ya kikao kizito kilichowahusisha viongozi wa juu wa klabu hiyo chini ya Mo Dewji.
Hatua hiyo imehitimisha sintofahamu iliyokuwapo juu ya hatma ya benchi la ufundi baada ya kushindwa kufikia mafanikio yaliyotarajiwa msimu uliopita, ambapo ilikuwa ni pamoja na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.
Mashine sita
Kwa mujibu wa chanzo hicho ni kwamba kocha Fadlu amependekeza baadhi ya wachezaji wa kikosi cha sasa kuongezewa nguvu kwa kuletewa mashine sita ikiwamo eneo analocheza Jean Charles Ahoua aliyemaliza kama kinara wa mabao wa timu hiyo akifunga mabao 16 na asisti tisa.
"Ripoti ya awali ya kocha Fadlu alihitaji Ahoua aongezewe nguvu zaidi, pia anataka beki wa kati mwenye uwezo wa kukaba kwa akili na nguvu, kiungo mkabaji mwenye ubora kama au kushinda kagoma," chanzo hicho kilifichua na kuongeza;
"Kiungo mshambuliaji namba 10, mwenye ubora kushinda Ahoua, Winga wa kulia mwenye makali kushinda Joshua Mutale na Mshambuliaji wa kati mwenye ujuzi wa kufunga kushinda Mukwala (Steven) na Ateba (Leonel)."
Sababu kubwa ya kutakiwa kwa mshambuliaji mwingine mkali ni kutokana na taarifa kwamba huenda Mukwala anaweza kuchomoka klabuni baada ya kupata ofa yenye maana inatoweza kuipa timu hiyo fedha za maana kutoka klabu moja ya Ukanda wa Afrika Kaskazini ambaye hata hivyo haijafahamika.
Hata hivyo, chenzo hicho hakijataja wachezaji waliopendekezwa moja kwa moja, lakini tarai mabosi wa klabu hiyo wameianza kazi ya kusaka beki mpya wa kati atakayetoka kati ya vikosi vya majeshi kama ilivyo kwa kipa atakayechukua nafasi iliyoachwa na Aisha Manula aliyerudi Azam FC.
Klabu hiyo iliyofika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa taji mbele ya RS Berkane ya Morocco, inatarajiwa kuanza kambi ya maandalizi ya msimu ujao wiki mbili zijazo mara baada ya kumalizia mapumziko mafupi waliyopeana baada ya kumalizika msimu uliopita bila ya kubeba taji.
Simba ilimaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu nyuma ya Yanga iliyotetea taji kwa msimu wa nne mfululizo, pia ilishindwa kwenda fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa kutolewa nusu fainali na Singida Black Stars, huku ikichemsha mapema katika Ngao ya Jamii na kutoenda kutetea taji la Ligi ya Muungano, mbali na kupasuka katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2025 mbele ya Mlandege.