Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha atoa dira Simba

Muktasari:

Julio aliyetamba na kikosi hicho miaka ya 1980-1990 kabla ya kugeukia ukocha, alisema ifikie hatua viongozi ambao wamekaa kwa muda mrefu  katika  klabu hiyo wakae pembeni, ili kupisha wengine ambao watakuwa na mipango itakayoleta tija na maendeleo.

Simba imemaliza msimu wa nne mfululizo bila ubingwa wa Ligi Kuu Bara wala Kombe la Shirikisho (FA), jambo lililowakata stimu kuanzia viongozi, wachezaji, mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu hiyo, lakini kuna akili moja ameitoa kocha wa zamani wa klabu hiyo inayoweza kuwabeba.

Simba ilimaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga iliyotetea taji kama ilivyofanya katika Kombe la Shirikisho kwa kuifunga Singida Black Stars iliyowaong'oa Wekundu hao nusu fainali ya michuano hiyo, lakini ikilikosa taji la  Ngao ya Jamii ikifungwa pia nusu fainali na Yanga na katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 ilifungwa fainali na Mlandege.

Hata hivyo, kwa vile mambo yameonekana kuwavuruga Wanasimba, nyota na kocha wa zamani wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo 'Julio' amezungumza na Mwanaspoti na kusema imefika wakati klabu hiyo, ibadilishe mfumo wa kiuongozi na kuleta nguvu kazi ambayo italeta mapinduzi ya kunyakua mataji ya Ligi Kuu na michuano ya kimataifa inayoendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Julio aliyetamba na kikosi hicho miaka ya 1980-1990 kabla ya kugeukia ukocha, alisema ifikie hatua viongozi ambao wamekaa kwa muda mrefu  katika  klabu hiyo wakae pembeni, ili kupisha wengine ambao watakuwa na mipango itakayoleta tija na maendeleo.

"Kuna watu ambao wamezoeleka kwa muda mrefu kuwepo katika timu uungwana ni kukaa pembeni ili wengine wapate nafasi ya kusimamia mipango ya maendeleo ya Simba," alisema Julio ambaye amewahi kuzifundisha klabu mbalimbali hapa nchini baadhi ni Coastal Union, Singida Fountain Gate na KMC.

Jambo lingine alilolishauri Julio ni kuhakikisha jukumu la usajili linakabidhiwa kwa watu wanauojua mpira, vinginevyo itakuwa ngumu kupata wachezaji wa viwango vikubwa ambao watafikia malengo ya klabu.

"Haijawahi kutokea Simba ikafungwa na Yanga mara tano mfululizo, halafu viongozi wapo tu na wanaona ni jambo la kawaida kwa klabu kama Simba kupitia changamoto hiyo, sasa wakija wengine ambao wataona soka linataka kitu gani, Simba itakwenda kufanya maajabu makubwa Afrika," alisema Julio na kuongeza;

"Simba sio mali ya watu wachache ambayo wana uchoyo na kuona wanaweza wakaamua chochote na wakaacha maumivu ya watu yaendelee, kwa sasa soka lina mabadiliko ukisajili vizuri utaona matunda, mfano mzuri kipindi cha nyuma ambacho Simba ilikuwa imechukua ubingwa mara nne mfululizo kikosi chake kilikuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa."

Beki wa kati huyo wa zamani aliyetamba pia CDA na Taifa Stars, alisema uongozi mpya uende pia na kuleta majembe ya maana yenye viwango vya kuipigania timu uwanjani na sio wachezaji wanaokuwa na homa za vipindi ambao kwa sehemu kubwa wameikwamisha Simba msimu huu.

Hata hivyo, licha ya Simba kukosa ubingwa, lakini kwa msimu huu ilionekana kuwa moja ya timu zilizokuwa na ushindani mkubwa chini ya Kocha Fadlu Davids, ikiibana Yanga hadi siku ya Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Juni 25 na bingwa wa Ligi Kuu kujulikana siku hiyo kwa Yanga kushinda 2-0.

Simba imemaliza msimamo ikiwa na pointi 78, nne na ilizoiwezesha Yanga kubeba ubingwa ikivuna 82 kila moja ikicheza mechi 30, huku ikitoa Mfungaji Bora, Jean Charles Ahoua aliyefunga mabao 16.