Yanga bado 90 ubingwa CAF

Muktasari:

  • Yanga imekubali kichapo cha pili katika Uwanja wa nyumbani katika Kombe la Shirikisho huku ikitizamia dakika 90 za ugenini kuamua hatma ya ubingwa wa kombe hilo.

Dar es Salaam. Licha ya Yanga kupoteza kwenye mchezo wa fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mabao 2-1 dhidi ya USM Alger bado wanadakika 90 nyingine za kupigania ubingwa.

Mabao ya USM Alger yalifungwa na A. Mahious dakika ya 32 na I. Merili dakika ya 84 huku la Yanga akifunga Fiston Mayele dakika ya 82.

Kwa matokeo hayo, Yanga anatakiwa kwenda Algeria akiwa na hesabu za kushinda mchezo wa marudiano ili kutwaa Kombe hilo kwa mara ya kwanza.


Hizi ni Dondoo za mchezo huo ambao ilishuhudiwa Yanga ikipoteza ikiwa nyumbani  kwa mara ya pili kwenye Kombe hilo la Shirikisho.

Dickson Job ndiye mchezaji pekee wa Yanga ambaye alionyeshwa kadi ya njano kwenye mchezo huo.

Katika mashuti 15 ambayo Yanga ilipiga langoni mwa USM Alger ni mashuti manne tu ambayo yalilenga lango.

USM Alger ilifanya madhambi mara 21 huku Yanga ikifanya mara 10.

Licha ya kupoteza Yanga ilikuwa na asilimia kubwa ya umiliki wa mpira huku ikipiga jumla ya pasi 449, USM Alger wakiwa na pasi 239.

Yanga ilipata kona tisa lakini hakuna hata moja ambayo ilizaa matunda huku USM Alger ilipata kona nne.

Hii ni mara ya pili kwa wapinzania wa Yanga, USM Alger kucheza fainali ya michuano hiyo ya Kimataifa.

Bao ambalo alifunga Mayele ni la saba msimu kwenye Kombe la Shirikisho huku akiongoza orodha ya wafumania nyavu wa michuano hiyo.