Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vipande vitano Dabi ya Kariakoo

Muktasari:

  •  
  • Ukiweka kando hilo la Yanga, Simba nayo ina jambo lake katika mchezo huu inahitaji kufanya mbele ya mtani wake wa jadi.

JANA Jumapili, zimepigwa mechi nane za raundi ya 30 katika Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2024-2025 ambapo timu 14 zimefunga msimu rasmi, huku kikibaki kiporo kimoja kikizihusisha Yanga na Simba.

Kiporo hicho kimepangwa kuchezwa Juni 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo baada ya hapo, ni rasmi sasa itakuwa ligi imefikia tamati.

Wakati tukielekea kushuhudia mchezo huo utakaochezwa keshokutwa Jumatano, Dabi hiyo ya Kariakoo imegawanyika katika vipande vikuu vitano.

Kabla ya kufika huko, nikukumbushe tu kwamba katika michezo ya jana Jumapili, kulikuwa na mambo kadhaa yaliyokuwa yakisubiriwa ambayo ni idadi kamili ya timu zitakazocheza mechi za mtoano (play off) kuwania kubaki ligi kuu kwa msimu ujao baada ya KenGold na Kagera Sugar kushuka moja kwa moja.

Pia ile vita ya ufungaji bora imepamba moto ambapo hii itaamuliwa rasmi Juni 25 baada ya Dabi ya Kariakoo kuchezwa. Lakini pia ushindani wa kipa gani atamaliza na clean sheet nyingi baada ya Moussa Camara wa Simba kuongoza kwa muda mrefu, akifuatiwa na Djigui Diarra.

Camara katika mchezo wa jana ambao Simba ilicheza dhidi ya Kagera Sugar, kipa huyo alikuwa na clean sheet 18, alihitaji moja tu kujihakikishia umwamba kwani alimuacha Diarra aliyekuwa na 16 kabla ya Yanga kuvaana na Dodoma Jiji.

Mwisho kabisa, timu zilizomaliza msimu rasmi zilikuwa na vita yao ya nafasi kuanzia ile ya tatu hadi ya mwisho ambapo kuna bonasi kutoka kwa mdhamini mwenye haki za matangazo, Azam Media.

Kwa mujibu wa mkataba wa Azam Media mgao wa nafasi kuanzia msimu wa 2021-2024, timu inayoshika nafasi ya kwanza hadi ya mwisho haitoki patupu, kuna mgao wa fedha ambao haufanani, hivyo baada ya dakika tisini kukamilika kwa mechi za jana, kila kitu kimefahamika na kuacha vita ya wawili, Yanga na Simba.

Ipo hivi, bingwa wa ligi anapata bonasi ya Sh500 milioni, nafasi ya pili Sh250 milioni, nafasi ya tatu Sh225 milioni, nafasi ya nne Sh200 milioni, nafasi ya tano Sh65 milioni, nafasi ya sita Sh60 milioni, nafasi ya saba Sh55 milioni, nafasi ya nane Sh50 milioni, nafasi ya tisa Sh45 milioni, nafasi ya kumi Sh40 milioni, nafasi ya 11 Sh35 milioni, nafasi ya 12 Sh30 milioni, nafasi ya 13 Sh25 milioni, nafasi ya 14 Sh20 milioni, nafasi ya 15 na 16 Sh10 milioni.

Tukirudi kwenye mchezo wenyewe, hii itakuwa Dabi ya Kariakoo ya 114 katika Ligi Kuu ambapo msimu huu tumeshuhudia duru la kwanza Yanga ikishinda kwa bao 1-0.

Hadi kufikia mchezo huu kuchezwa, tumeshuhudia ukiahirishwa mara mbili. Awali ilikuwa Machi 8, 2025 ambapo Simba ilidai siku moja kabla ya mechi ilizuiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja utakaotumika, hivyo imenyimwa haki yao kikanuni, ikagoma kucheza hadi waliofanya tukio hilo wachukuliwe hatua. Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ikasikiliza hoja zao na kuahirisha mchezo huo.

Baada ya hapo, kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya wasimamizi wa ligi hiyo na Yanga ambapo mwisho wa siku TPLB ikatangaza mechi hiyo itachezwa Juni 15 mwaka huu. Yanga ikagomea.

Mgomo huo wa Yanga ulikuja na hoja nne ikiwemo kutaka baadhi ya viongozi waliopo kwenye mamlaka za soka kujiuzulu. Mazungumzo ya usuluhishi yaliyofanyika na baadhi ya viongozi kuondoka kwenye nafasi zao ikarahisisha mambo. Ndipo Juni 25 mwaka huu ikawa sasa tarehe rasmi ya mchezo huo kufanyika.

Sasa tukiwa tunasubiri kuona mchezo huo, hapa kuna vipande vitano vya Dabi ya Kariakoo.


UFUNGAJI BORA

Mechi za jana Jumapili kabla hazijachezwa, kinara wa mabao alikuwa Jean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga mabao 16. Chini yake kuna Lionel Ateba wa Simba, Clement Mzize na Prince Dube wanaocheza Yanga ambapo wachezaji wote hao watatu kila mmoja akifunga mabao 13 kabla ya jana.

Ukiachana na nyota hao, kabla ya jana orodha ya ufungaji kwa wanaofuatia ni Steven Mukwala wa Simba (12), Jonathan Sowah wa Singida Black Stars (12), Pacome Zouzoua wa Yanga (11) na Gibril Sillah wa Azam (11).

Ukiangalia katika vita hiyo ya ufungaji mbali na ushindani wa mchezaji mmojammoja, lakini pia inaingia utimu, kuna wachezaji watatu wa Simba sawa na Yanga, Singida Black Stars mmoja sawa na Azam.
Sasa basi kuelekea Dabi ya Kariakoo, mbali na timu kusaka matokeo mazuri, pia nyota wa Simba na Yanga watakuwa na vita yao ya kuwania ufungaji bora.


CLEAN SHEET


HAPA pia inawahusu makipa wawili, mmoja anacheza Yanga, Djigui Diarra na mwingine wa Simba, Moussa Camara.

Camara huu ni msimu wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara, kabla ya jana alikuwa na clean sheet 18, hitaji la clean sheet moja tu kwake ili kuwa mbabe akimuacha Diarra ambaye huu ni msimu wa nne.

Diarra katika misimu minne sasa, amebeba tuzo ya kipa bora mara mbili, huku msimu uliopita akipigwa bao na aliyekuwa kipa wa Coastal Union, Ley Matampi ambaye alimaliza kinara wa clean sheet akiwa nazo 15, huku yeye akikusanya 14.

Hadi sasa Diarra tayari amevunja rekodi yake ya msimu uliopita kwa kukusanya clean sheet nyingi, huku Camara pia akivunja ya jumla kutoka kwa Matampi.

UBINGWA

Hapa ndiyo kwenye utamu zaidi, Yanga inapambana kutetea ubingwa ilioubeba msimu huo ikitaka kushinda kwa mara ya nne mfululizo, Simba haipo kinyonge, inausaka ubingwa ambao mara ya mwisho iliubeba msimu wa 2020–2021 ambapo pia ilichukua mara nne mfululizo (2017–2018, 2018–2019, 2019-2020 na 2020–2021. Matokeo ya mchezo huu yataamua mbabe.

Ikumbukwe kuwa, Yanga ndiyo vinara wa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikifanya hivyo mara 30, inafuatia Simba iliyochukua mara 22.

YANGA KULIPA KISASI?

Utamu wa mchezo huu, kombe litakuwa uwanjani, raha iliyoje kuona unamfunga mtani wako kisha unasindikizia na kubeba ubingwa.
Hii kwa Yanga inawakumbusha ilivyotokea msimu wa 2011-2012 ambapo Simba ilikabidhiwa ubingwa wa ligi mbele yao kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hiyo ilikuwa Mei 6, 2012 ambapo Simba iliingia kucheza Dabi ya Kariakoo ikiwa na uhakika wa kuwa bingwa, hivyo ikaona ubingwa hautanoga bila ya kumfunga mtani, mabingwa hao wakashinda 5-0. Ilikuwa aibu kwa Yanga.

Sasa hii inaweza kuwa ni nafasi kwa Yanga kulipa kisasi kwa kuwafunga watani wao na kubeba ubingwa ikiwa ni baada ya kupita takribani miaka 13.

SIMBA KUMALIZA UTEJA?

Ukiweka kando hilo la Yanga, Simba nayo ina jambo lake katika mchezo huu inahitaji kufanya mbele ya mtani wake wa jadi.
Rekodi zinaonyesha Simba haijaifunga Yanga katika mechi nne mfululizo za ligi walizokutana wakongwe hao wa soka hapa nchini. Itakuwaje Juni 25?

Kocha Fadlu Davids wa Simba ana kazi ya kumaliza uteja uliopo ndani ya timu hiyo dhidi ya Yanga kwani mechi tatu mfululizo zilizopita za ligi timu hiyo imepoteza.

Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga kwenye ligi ilikuwa inafundishwa na Roberto Oliveira 'Robertinho' katika mchezo uliochezwa Aprili 16, 2023 ambapo matokeo yalikuwa Simba 2-0 Yanga. Wafungaji wakiwa Henock Inonga na Kibu Denis.

Baada ya hapo, Yanga imeifunga Simba mfululizo huku matokeo yakiwa; Simba 1-5 Yanga (Novemba 5, 2023), Yanga 2-1 Simba (Aprili 20, 2024) na Simba 0-1 Yanga (Oktoba 19, 2024).