Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ligi Kuu ngoma imeisha hivi

Muktasari:

  • Mchezo wa jana ndiyo ulikuwa wa mwisho kwa timu ya Kagera Sugar kucheza kwenye Ligi Kuu kwani katika msimu ujao timu hiyo itashiriki mashindano ya Championship kusaka upya tiketi ya kurudi katika Ligi Kuu.

Dar es Salaam. Klabu ya Simba imefanikiwa kuondoka na pointi tatu muhimu baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge huku Yanga ikiendeleza rekodi ya kufunga tano tano.

Yanga imefanikiwa kupata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Dodoma Jiji na kufanikiwa kufunga mabao kumi kwenye michezo miwili baada ya siku tatu nyuma kuichapa Tanzania Prisons mabao 5-0 kwenye mchezo mwingine wa Ligi Kuu.


Mechi ya Simba


Huu ulikuwa mchezo wa mwisho wa nyumbani kwa Wekundu wa Msimbazi, ambao sasa wanabaki na mechi moja ya kiporo dhidi ya watani wao wa jadi Yanga itakayokuwa ya kuamua hatima ya ubingwa msimu huu.

Katika mchezo wa leo, Simba ilipata ushindani mkubwa uwanjani licha ya Kagera Sugar kushindwa kusalia katika Ligi Kuu baada ya kushuka daraja. Kagera walianza kwa kasi katika dakika ya kwanza ambapo walifanikiwa kupata pigo la frikiki jirani na lango la Simba ambalo halikuzaa matunda. 

Bao pekee la Simba lilifungwa na mshambuliaji, Steven Mukwala katika dakika ya 16 akimaliza mpira wavuni baada ya mabeki wa Kagera Sugar kufanya uzembe. 

Katika mchezo huo, kocha wa Simba, Fadlu Davids aliwaanzisha nje baadhi ya nyota wake kama Kibu Denis, Elie Mpanzu, Shomari Kapombe, Yusuph Kagoma, Mohamed Hussein, Joshua Mutale na Leonel Ateba ikiwa ni njia mojawapa ya kuwapumzisha wachezaji wake kabla ya mchezo wa Dabi ya Kariakoo Jumatano ijayo ikiwa imefikisha pointi 78 moja nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 79. 

Yanga yapiga tano 

Ikiwa kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar, Yanga ilifanikiwa kuendeleza moto wake wa kufunga mabao mengi kwenye mchezo mmoja baada ya kuichapa Dodoma mabao 5-0.

Mchezo huu ulikuwa wa upande mmoja ambapo Yanga ilionekana kutawala na kufanikiwa kufunga mabao yake kupitia kwa wachezaji watano tofauti, bao la kwanza lilifungwa na Clatous Chama, Duke Abuya, Ibrahim Hamad Bacca, Maxi Nzengeli na bao moja na kujifunga.

Sasa Yanga inatakiwa kupata sare tu kwenye mchezo wa Dabi ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mabao, ikiwa imefunga mabao 81 na kuruhusu kumi tu, inafuatiwa na Simba kwa idadi ya mabao imefunga 69 na kuruhusu 11, hivyo kama Simba inataka kutwaa ubingwa msimu huu inatakiwa kuhakikisha inapata ushindi tu kwenye mchezo ujao.

Ahoua bado kinara ufungaji


Katika mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora wa Ligi kuu, mshambuliaji wa Simba, Jean Ahoua bado anaendelea kusalia nafasi ya kwanza akiwa na jumla ya mabao 16 mbele ya Leonel Ateba, Steven Mukwala, Clement Mzize (Yanga), na Prince Dube (Yanga) wote wakiwa na mabao 13.

Ahoua ambaye alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi kuu ya Ivory Coast msimu uliopita anapewa nafasi kubwa ya kuweza kutwaa tuzo hiyo tena kwa mara nyingine msimu huu baada ya kuhusika katika mabao 25 akiwa na Wekundu wa Msimbazi.

Camara amaliza kinara wa Clean Sheets 

Kipa wa Simba, Moussa Camara amethibitisha kuwa kinara wa 'Clean Sheet' msimu huu baada ya kutoruhu bao katika mchezo wa leo akifanya hivyo mara 19 mbele ya Djigui Diarra wa Yanga mwenye Clean Sheet 17, Patrick Munthari wa Mashujaa (12), Yona Amosi wa Pamba (11) na Mohamed Mustafa wa Azam (10).

Katika msimu uliopita wa 2023-2024 kipa wa Coastal Union, Ley Matampi ndiye aliyeibuka kipa bora wa Ligi kuu alipochomoza na jumla ya Clean Streets 15. Mara ya mwisho ilikuwa ni msimu wa 2020-2021 ambapo kipa wa Simba, Aishi Manula alitwaa tuzo hiyo.
Kagera Sugar ilivyomaliza mwendo.

Mchezo wa jana ndiyo ulikuwa wa mwisho kwa timu ya Kagera Sugar kucheza kwenye Ligi Kuu kwani katika msimu ujao timu hiyo itashiriki mashindano ya Championship kusaka upya tiketi ya kurudi katika Ligi Kuu.

Kagera Sugar iliungana na KenGold baada ya kushindwa kufikisha pointi za kusalia kwenye Ligi Kuu ikiwa imekusanya jumla ya pointi 23 katika michezo 30 iliyocheza huku KenGold ikikusanya pointi 16.

Playoff ni Prisons na Fountain 

Pamoja na kuonyesha upinzani kwenye michezo ya jana, Fountan na Prisons ndiyo zitacheza mechi za mtoano kutafuta timu moja itakayokwenda kuvaana na Stand United ili kupata timu moja itakayocheza Ligi Kuu msimu ujao.

Michezo ya leo, Prisons ilitoka nyuma na kulazimisha sare ya mabao 3-3 dhidi ya Singida na kufikisha pointi 31, huku Fountain ikilala mabao 3-2 dhidi ya Azam na kumaliza ligi na pointi 29 kwenye michezo 30.