Vigogo wanaisubiri Spurs au United nusu fainali

Muktasari:
- Leo usiku Manchester United itakuwa ugenini ikivaana na Totteham kutafuta timu ya nne itakayokwenda hatua ya nusu fainali.
London, England. Mshambuliaji wa Arsenal Gabriel Jesus, jana alifanya mambo makubwa baada ya kufunga mabao matatu, 'hat trick' na kuipeleka timu yake hatua ya nusu fainali ya Kombe la Carabao, huku Liverpool nayo ikiibuka na ushindi.
Arsenal ilipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Crystal Palace kwenye mchezo uliokuwa mgumu na wa kuvutia kwa pande zote mbili.
Jesus ambaye alikuwa hajafunga bao lolote kwenye Uwanja wa Emirates kwa mwaka 2024, alifunga hat trick yake kipindi cha pili cha mchezo huo, akianza kwa kusawazisha bao la mapema lililofungwa na Jean Phillipe Mateta katika dakika ya nne ya mchezo.
Staa huyo raia wa Brazil alifunga bao lake la kwanza katika dakika ya 54 kafunga la pili dakika ya 73 huku akikamilisha hat trick yake dakika ya 81 ya mchezo huo.
Hata hivyo, Palace waliipa Arsenal wakati mgumu baada ya kufunga bao la pili katika dakika ya 85 kupitia kwa Eddie Nketiah na kuifanya mechi hiyo kuwa ngumu dakika tano za mwisho.
Liverpool nayo ilifanikiwa kwenda hatua ya nusu fainali baada ya kuichapa Southampton mabao 2-1.
Liverpool ndiyo ilikuwa ya kwanza kujipatia bao kupitia kwa Darwin Nunez dakika ya 24, huku Harvey Eliott akiweka la pili dakika ya 31 ya mchezo huo, kabla wenyeji hawajarudisha bao moja katika dakika ya 59 kupitia kwa Cameron Archer kwenye mchezo ambao Liverpool waliumiliki kwa asilimia kubwa.
Timu nyingine ya tatu iliyofanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali ni Newcastle ambao waliichapa Brentford mabao 3-1, Sandro Tonali alifunga mabao mawili katika dakika ya tisa na 45, huku Fabian Schar akifunga la tatu dakika ya 69 ya mchezo huo.
Bretford ambayo ilionyesha kiwango cha chini kwenye mechi hii ilifunga bao la kufutia machozi dakika ya tisini ya mchezo likiwekwa kimiani na Yoane Wissa.
Leo usiku Manchester United itakuwa ugenini ikivaana na Totteham kutafuta timu ya nne itakayokwenda hatua ya nusu fainali.