Vinicius JR ajifariji na tuzo ya Fifa

Muktasari:
- Idadi ya pointi 48 ambazo alipigiwa, zilitosha kumfanya Vinicius JR apate tuzo hiyo na kuwaacha kwenye mataa nyota wawili alioingia nao katika kinyang'anyiro cha mwisho, Rodri aliyepata pointi 43 na Bellingham ambaye alikusanya pointi 37.
Doha, Qatar. Mshambuliaji wa Real Madrid na Brazil, Vinicius JR amefichua kuwa amepitia katika nyakati ngumu hadi kufikia hatua ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia 2024 ya shirikisho la mpira wa miguu duniani (Fifa) juzi Jumanne.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo ambayo awamu iliyopita ilichukuliwa na Lionel Messi, Vinicius alisema kuwa ushindi wake una maana kubwa kwake na wote ambao wanamtazama kama kioo.
"Sijui hata nianzie wapi. Imeanzia mbali sana na ilionekana kama haiwezekani mimi kufika hapa. Nilikuwa mtoto mdogo ambaye alicheza mpira wa miguu akiwa hajavaa viatu katika mitaa ya Sao Goncalo iliyo na umasikini na uvunjaji wa sheria. Kuwepo hapa kuna maana kubwa sana kwangu.
"Ninafanya hili kwa ajili ya watoto wengi ambao wanaamini kwamba kila kitu hakiwezekani na wanahisi hawawezi kufika hapa," alisema Vinicius JR.
Idadi ya pointi 48 ambazo alipigiwa, zilitosha kumfanya Vinicius JR apate tuzo hiyo na kuwaacha kwenye mataa nyota wawili alioingia nao katika kinyang'anyiro cha mwisho, Rodri aliyepata pointi 43 na Bellingham ambaye alikusanya pointi 37.
Pointi hizo zilitokana na kura zilizopigwa na manahodha wa timu za taifa na wadau tofauti wa mpira wa miguu duniani.
Ushindi wa Vinicius JR ni kama umemfuta machozi nyota huyo baada ya kukosa tuzo maarufu ya Ballon d'Or ambayo Rodri aliibuka mshindi.
Katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika Doha, Qatar, kiungo wa timu ya wanawake ya Barcelona, Aitana Bonmati aliibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa kike wa Fifa 2024.
Carlo Ancelotti aliibuka mshindi wa tuzo ya kocha bora wa kiume na kocha bora wa kike alikuwa ni Emma Hayes na kipa wa Aston Villa, Emiliano Martinez aliibuka mshindi wa tuzo ya kipa bora, ikiwa ni mara ya pili kwake kufanya hivyo.
Alyssa Naeher alitangazwa mshindi wa tuzo ya kipa bora wa kike, Alejandro Garnacho alishinda tuzo ya goli bora la mwaka upande wa soka la wanaume huku katika soka la wanawake, mshindi wa tuzo ya goli bora la mwaka akiwa ni nyota wa Brazil, Marta.
Tuzo nyingine ilikuwa ni ya uungwana ambayo mshindi wake alikuwa ni Thiago Maia anayechezea Internaciol ya Brazil.