Ancelotti aweka rekodi Madrid ikitwaa taji

Muktasari:
- Baada ya ushindi huo Carlo Ancelotti, amekuwa kocha mwenye mataji mengi zaidi katika historia ya Real Madrid akifikisha makombe 15, akiivunja rekodi ya Miguel Muñoz aliyekuwa na mataji 14.
Madrid, Hispania. Kocha wa Real Madrid Carlos Ancelotti ameiongoza timu hiyo kubeba Ubingwa wa FIFA Intercontinental, mashindano ambayo yanahusisha klabu ambazo zimefanya vizuri kwenye mabara yote sita ambapo ilishuhudiwa Madrid ikibeba taji hilo baada ya kuifunga Klabu ya Pachuca mabao 3-0 kwenye Uwanja wa lusail huko Qatar.
Baada ya ushindi huo Carlo Ancelotti, amekuwa kocha mwenye mataji mengi zaidi katika historia ya Real Madrid akifikisha makombe 15, akiivunja rekodi ya Miguel Muñoz aliyekuwa na mataji 14.

Mataji ya Ancelotti ni La Liga mara mbili (2022, 2024), Copa del Rey mara mbili (2014, 2023), Spanish Super Cup mara mbili (2022, 2024) UEFA Champions League mara tatu (2014, 2022, 2024).
Mengine ni UEFA Super Cup mara tatu (2014, 2022, 2024) Klabu Bingwa Dunia mara mbili (2014, 2022) na FIFA Intercontinental Cup mwaka 2024.
Hili ni taji la pili msimu huu wa 2024-2025, baada ya kutwaa UEFA Super Cup mwezi Agosti dhidi ya Atalanta.
Real Madrid inatarajiwa kucheza Supercopa de España Januari, huku wakiwa na nafasi nzuri ya kutetea mataji yao kama La Liga, UEFA Champions League na Copa del Rey.
Mabao ya Madrid yalifungwa na Kylian Mbappé dakika ya 37 baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Vinícius Júnior huku bao la pili likifungwa na Rodrygo dakika ya 53 akipewa pasi na Mbappé, wakati bao la tatu lilifungwa na Vinícius dakika ya 84 kwa mkwaju wa penalti baada ya Lucas Vazquez kuchezewa vibaya ndani ya eneo la hatari.
Kylian Mbappé ameweka rekodi ya kufunga mabao mawili kwenye mechi mbili za fainali akiwa na Madrid, ambapo alifanya hivyo Agosti 14, 2024 kwenye fainali ya UEFA Super Cup dhidi ya Atalanta.

Bao alilofunga dakika ya 37 linakuwa la nne kwa Mbappe kufunga kwenye Uwanja wa Lusail baada ya kufanya hivyo kwenye mchezo wa Kombe la Dunia alipofunga mabao matatu dhidi ya Argentina, Desemba 18, 2022.
Madrid imerejea Hispania leo asubuhi, ikijiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Sevilla utakaopigwa Desemba 22, 2024 kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu ambapo inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37 nyuma ya Barcelona ambayo inaongoza ligi ikiwa na pointi 38.