Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi watanda Kisutu, waandishi wa habari wazuiwa

Muktasari:

  • Waandishi wa habari ni miongoni mwa watu waliozuiwa na Polisi kuingia au kusogea karibu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatilia kesi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu

Dar es Salaam. Ulinzi umeendelea kuimarishwa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuzunguka makutano yote yanayoingilia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambako kuna kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa leo, waandishi wa habari wamepigwa marufuku kusogea mahakamani hapo.

Katika eneo hilo la Mahakama, polisi waliovaa sare na wasio na sare wapo ndani ya magari wakifanya doria huku wakiwa wameshikilia silaha mbalimbali zikiwamo bunduki na virungu.

Polisi wakiwa ndani ya gari lao wakiwa katika majukumu yao ya kuimarisha ulizi katika maeneo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo Jumatatu Aprili 28, 2025.

Mahakamani hapa leo Jumatatu, Aprili 28, 2025 kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni inayomkabili Lissu itaendelea kunguruma, mawakili wa pande zote wanatarajiwa kuchuana kwa hoja, kuhusu kuendeshwa kwa njia ya mtandao.

Ulinzi huo ni sawa na uliokuwa Alhamisi ya Aprili 24, 2025 wakati kesi hiyo pamoja na ile ya uhaini zinazomkabili Lissu zilipoitwa kwa hatua mbalimbali.

Polisi walitanda maeneo ya Mahakama kuzuia wasohusika kuingia.

Kama ilivyokuwa siku hiyo waandishi wa habari kuzuiwa na hawakutakiwa kusogea karibu.

Wananchi wa kawaida hasa wale wanaohisiwa kuwa makada wa Chadema pia, wamezuiwa kuingia ndani ya Mahakama hiyo.

Magari ya maji ya washawasha yameegeshwa upande wa makutano ya Hoteli ya Serena pamoja na ulinzi huo bado kuna makada wa Chadema waliovaa nguo za kawaida wanazunguka kuangalia uwezekano wa kuingia.

Ugumu unaowasibu makada hao ni gari za Polisi zilizoegeshwa upande kushoto na kulia kulitazama geti kubwa la Mahakama hiyo, lakini si hivyo tu gari nyingine imegeshwa kutokea upande wa Hoteli wa Holiday Inn yote yakiwa na Polisi walioshika mitutu ya bunduki.

Makundi ya waandishi wa habari nao baada ya kuzuiwa kuingia na kutakiwa kukaa mbali na maeneo hayo, wamebaki kukaa makundi na wale wenye udhubutu wanajaribu kupiga picha kuona uwezekano wa kupata matukio yanayojiri.

Kesi hiyo ya Lissu inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, imepangwa leo kwa ajili ya Jamhuri (upande wa mashitaka) kujibu hoja za Lissu na mawakili wake kupinga kesi hiyo kuendeshwa kwa njia ya mtandao.

Lissu alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka yanayomkabili katika kesi hiyo pamoja na nyingine ya uhaini kwa mahakimu wawili tofauti, Aprili 10, 2025.

Upande wa mashitaka uliieleza Mahakama upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika, ukaomba Mahakama ipange tarehe kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

Katika hatua hiyo, mshitakiwa husomewa maelezo ya awali yanayohusiana na mashitaka kisha hatakiwa kubainisha taarifa zisizobishaniwa (anazokubaliana nazo) na zinazobishaniwa (asizokubaliana nazo), kabla Mahakama kuanza kupokea ushahidi.

Hivyo, Mahakama hiyo ilipanga kuendelea na hatua hiyo Aprili 24, 2025.

Hata hivyo, siku hiyo haikuendelea katika hatua hiyo baada ya Lissu kugomea utaratibu uliowekwa na Mahakama, kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya mtandao, huku Lissu akiwa mahabusu katika Gereza la Ukonga.


Mashitaka

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashitaka matatu ya kuchapisha mitandaoni taarifa za uongo, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.

Mashitaka hayo yote matatu ni ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube, akidaiwa kuyatenda Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaa, kwa nia ya kulaghai umma.

Katika shitaka la kwanza maneno aliyoyachapisha Lissu ni: "Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 wagombea wa Chadema walienguliwa kwa maelekezo ya Rais," wakati akijua maneno hayo ni ya uongo na yanapotosha umma.

Shitaka la pili anadaiwa siku hiyo alichapisha taarifa za uongo na za kupotosha umma kuwa: "Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi."

Polisi wakionekana kwa mbali wakiwa katika majukumu yao ya kuimarisha ulizi katika maeneo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo Jumatatu Aprili 28, 2025.

Katika shitaka la tatu anadaiwa siku hiyo hiyo alichapisha taarifa kuwa:

"Majaji ni Ma-CCM, hawawezi kutenda haki, wanapenda wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.

Katika mashitaka hayo alipoulizwa na hakimu iwapo ni kweli au si kweli, Lissu hakukana bali, alisema maneno hayo si kosa hivyo sio kweli.

Katika kesi hiyo Lissu aliachiwa kwa dhamana baada ya kutekeleza masharti ya dhamana.

Hata hivyo, alilazimika kupelekwa mahabusu kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine ya shitaka la uhaini, ambalo halina dhamana.