Prime
Serikali ilivyojibu hoja za Lissu kupinga kesi yake kusikilizwa mtandaoni

Muktasari:
- Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imepanga Mei 6, 2025 kutoa uamuzi wa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu itasikilizwa kwa njia ya mtandao ama atafikishwa mahakamani.
Dar es Salaam. Serikali imejibu hoja za mawakili wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu, kupinga kesi inayomkabili ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Lissu alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka yanayomkabili katika kesi hiyo pamoja na kesi nyingine ya uhaini kwa mahakimu wawili tofauti, Aprili 10, 2025.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, alipanga usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo kufanyika Aprili 24, 2025.
Hata hivyo, kesi haikuweza kuendelea katika hatua hiyo baada ya Lissu kugomea utaratibu uliowekwa na Mahakama, kuisikiliza kwa njia ya mtandao huku Lissu akiwa mahabusu katika Gereza la Ukonga.
Jopo la mawakili wa Lissu walipinga kesi hiyo kuendeshwa kwa njia ya mtandano hasa katika hatua hiyo kwa madai kuwa ni kinyume na matakwa ya kifungu cha 192(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Upande wa mashitaka umejibu hoja hizo leo, Aprili 28, 2025 kupitia kwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mreme kwa niaba ya jopo la waendesha mashitaka wa kesi hiyo, na kuiomba Mahakama izitupilie mbali.
Wakili Mrema amedai mawakili wa upande wa utetezi wanachanganya kati ya mahakama ya wazi na mahakama kwa njia ya mtandao, akidai mahakama ya wazi inayotajwa katika kifungu hicho ni ile kuendeshwa kwa uwazi bila kificho.
Amedai shauri kusikilizwa kwa njia ya mtandao sio kuendeshwa kwa kificho bali ni namna tu usikilizwaji wake unafanyika kupitia mtandao.
“Cha msingi zaidi umma umeruhusiwa kushiriki kwenye shauri hili,” amesisitiza wakili Mrema.
Kuhusu kusainiwa kwa nyaraka amedai utaratibu wa namna ya mashauri ya kusikilizwa kwa njia ya mtandao umeainishwa wazi kwenye kanuni.
Alisisitiza kifungu hicho kinapaswa kusomwa pamoja na sheria nyingine, ikiwa ni pamoja na kanuni na kwamba shauri hilo, sio la kwanza kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Amedai maombi yao kesi hiyo kuahirishwa kwa siku 30 ili wapate nafasi ya kuzungumza na mteja wao ni kwa mujibu wa sheria ya CPA ambayo inatoa ukomo wa muda wa aihirisho kwa kesi ambayo mshtakiwa ana dhamana kuwa usizidi siku 30.
Hivyo amedai mawakili wa utetezi walishindwa kueleza ni sheria ipi imekiukwa kwa ombi hilo, huku akidai upande wa utetezi hawakubainisha kuwa ni muda gani wanaoona unafaa.
Kuhusu mkuu wa gereza kufika mahakamani kujieleza kwa kuwazuia mawakili kumuona na kuzungumza na mteja wao pamoja na ndugu wa Lissu, na polisi kuwazuia wananchi kuingia kusikiliza kesi hiyo, Mrema ameomba mahakama izipuuze kwa sababu:
“Kwanza, Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza hoja hizo kutokana na kwamba zina uhusiano na tuhuma zinazowatuhumu baadhi ya watumishi wa umma, kwamba wamekosea katika utendaji,” amesema.
Amefafanua mawakili wangeweza kwenda Mahakama Kuu kufungua shauri la Mapitio ya Mahakama kwa kutokuridhika na huduma au utendaji wa watumishi hao wa umma.
Hata hivyo, wakili Mrema amerejea Ibara ya 30 (1) ya Katiba ya Nchi, akisema kuwa hakuna haki bila wajibu na Jeshi la Magereza lina kanuni zinazoweka utaratibu wa kuwasiliana na mahabusu au wafungwa.
Amedai kuwa mshtakiwa (Lissu) alipaswa kuandika barua kuwatambulisha mawakili wake, lakini hakufanya hivyo.
Kuhusu hoja ya Lissu kuhamishwa kutoka Gereza la Keko kwenda Ukonga, wakili Mrema amesema hakuna sheria au amri ya mahakama iliyokiukwa kwani Magereza wenyewe ndio wanajua wapi pa kumuhifadhi mahabusu.
Amehitimisha kwa kuiomba Mahakama ipuuze hoja na maombi ya mawakili wa utetezi badala yake izingatie hoja zao na shauri hilo liahirishwe siku 30, ili kutoa fursa kwa mawakili wa utetezi kuonana na mteja wao na wajiandae kwa ajili hatua ya usikilizwaji wa awali.
Hata hivyo, Wakili Jebra Kambole (wa utetezi) na Jeremiah Mtobesya wamedai wanaamini mahakama ina uwezo wa kutoa hati ya kumuita mshtakiwa, kutoka gerezani na akapelekwa mahakamani kusikiliza kesi yake.
Wakili Mpale Mpoki amedai mteja wao (Lissu) kwa kutokufikishwa mahakamani hajatendewa haki, njia pekee ya kumtendea haki ni kumtoa mahabusu na kumpeleka mahakamani asikilize kesi yake.
Dk Rugemeleza Nshala amesisitiza kumekuwa na ukiukwaji wa wazi na wa kiwango cha kutisha wa kanuni za magereza dhidi ya mteja wao kwa kutokufikishwa mahakamani kusikiliza kesi yake.
Wakili Peter Kibatala amedai hoja za upande wa mashitaka hazina mashiko na ameiomba mahakama ipuuze, huku wakili Jeremia Mtobesya akisisitiza mahakama hiyo ina mamlaka ya kutoa uamuzi wa mshtakiwa kupelekwa mahakamani kusikiliza kesi yake.
Hakimu Mhini ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 6, 2025 atakapotoa uamuzi wake.