Spurs, Newcastle zaingilia dili la Man United kwa Mbeumo

Muktasari:
- Hali inazidi kuwa ya mvutano zaidi kufuatia taarifa kuwa Spurs pia wanamtaka kocha wa Brentford, Thomas Frank.
Manchester United wanaendelea kusaka saini ya mshambuliaji wa Brentford, Bryan Mbeumo, huku wakikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mahasimu wao wa Ligi Kuu ya England, Tottenham na Newcastle United. Ingawa United tayari wamewasilisha ofa ya pauni milioni 55, Brentford wameikataa, wakisisitiza kwamba wanataka kiasi kikubwa ili kumuachia mshambuliaji huyo.
Kwa mujibu wa taarifa mpya kutoka Daily Mail na The Mirror, Manchester United wanajiandaa kuwasilisha ofa ya pili ambayo inaweza kufikia hadi pauni milioni 60 au zaidi.
Hii inakuja wakati ambao kocha Ruben Amorim amepewa nafasi ya kuendelea na mabadiliko ya kikosi baada ya msimu mbaya uliomalizika kwa kipigo kwenye fainali ya Europa League dhidi ya Spurs kilichowaondolea nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Lakini United hawako peke yao. Tottenham Hotspur, ambao wamepata mafanikio makubwa msimu huu kwa kutwaa taji lao la kwanza baada ya miaka 17, wameonesha nia ya kumchukua Mbeumo. Hali inazidi kuwa ya mvutano zaidi kufuatia taarifa kuwa Spurs pia wanamtaka kocha wa Brentford, Thomas Frank, ambaye ni mtu wa karibu sana na Mbeumo. Frank ndiye aliyemsajili nyota huyo kutoka Troyes kwa pauni milioni 5.8 mwaka 2019 na uhusiano wao wa karibu unaweza kuwa silaha ya Spurs kumnasa nyota huyo mbele ya United.
Kwa upande mwingine, Newcastle United nao wameingia kwenye vita hiyo. Klabu hiyo inayomilikiwa na wawekezaji kutoka Saudi Arabia imefanikiwa kufuzu Ligi ya Mabingwa baada ya kumaliza nafasi ya tano, jambo ambalo linaweza kuwa kivutio kikubwa kwa mchezaji yeyote. Hata hivyo, ripoti zinasema Mbeumo ameweka wazi kuwa angetamani zaidi kujiunga na Manchester United kuliko Newcastle, kutokana na jina kubwa la klabu na mshahara wa juu.

Mbeumo ameonesha kiwango bora tangu ajiunge na Brentford. Ameshafunga mabao 70 katika mechi 242 za mashindano yote, wakati amefunga mabao 42 katika mechi 136 za Premier League.
Manchester United, ambao walifunga mabao 44 tu katika EPL msimu uliopita idadi ya pili ya chini zaidi kwa timu zisizoshuka daraja wanamuona Mbeumo kama suluhisho.
Hata hivyo, Brentford hawana haraka ya kumuachia mshambuliaji huyo, hasa baada ya kumaliza nafasi tano juu ya Manchester United kwa tofauti ya pointi 14. Kocha wao Thomas Frank amesema:
“Ikiwa atauzwa, lazima iwe kwa kiasi kikubwa sana cha fedha. Hawezi kubadilishwa kirahisi. Na ningeshangaa kama vilabu vikubwa visingemtaka.”
Kwa sasa, mvutano wa saini ya Mbeumo umefikia hatua ya kusisimua, huku mashabiki wa United na Spurs wakingoja kwa hamu kuona ni nani atafaulu kupata huduma ya mmoja wa washambuliaji bora zaidi katika Ligi Kuu ya England kwa sasa.