Antony, Garnacho wachongewa Man United

Muktasari:
- Antony ameichezea Real Betis idadi ya mechi 26 za mashindano tofauti katika msimu wa 2024/2025, akifunga mabao tisa na amepiga pasi za mwisho tano.
Meneja wa Manchester United, Ruben Amorim ameshauriwa kuhakikisha anaachana na mawinga Antony na Alejandro Garnacho kama anataka kutengeneza timu ya ushindani.
Ushauri huo umetolewa na Rene Meulensteen ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa meneja wa zamani wa Man United, Sir Alex Ferguson.
Meulensteen amesema Antony ni mchezaji mbinafsi wakati huo akimuelezea Garnacho kama mchezaji mbaya.
Msaidizi huyo wa Ferguson amesema kuwa hata Ajax ilivyomuuza Antony kwenda Manchester United 2022 kwa Uhamisho wa Pauni 80 milioni, ni kama iliuza mbuzi kwenye gunia na sasa mzigo unaitesa Man United.
Amesema kuwa ingekuwa yeye asingekubali kumrudisha Antony baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo wa mwaka mmoja katika kikosi cha Real Betis.
“Nisingemrudisha Antony kwa sababu nimemtazama vya kutosha na sio mtu sahihi kwa klabu na sio mzuri kiasi cha kutosha. Kiwango chake kinachochewa na haiba yake na sio nzuri kwa timu. Ni mbinafsi.
“Hauwezi kupata tena Pauni 80 milioni yako kutoka kwa Antony. Nadhani ilikuwa biashara ya kipuuzi wakati ule niliposikia imefanyika.
“Najua hilo pale niliposikia kuhusu dili hilo ndani ya Amsterdam. Inaonyesha kwamba wachezaji wanaocheza katika ligi ndogo kama Uholanzi ni wa tofauti kabisa. Wanacheza kwa staili tofauti na kasi ndogo,” amesema Meulensteen.
Meulensteen amesema kuwa wachezaji wanaotamba Uholanzi, ni rahisi kufanya vizuri wakiwa Hispania na sio England.
Meulensteen amshukia pia Alejandro Garnacho alisema kuwa naye anapaswa kuachwa kwa vile ana tabia mbaya.
‘Garnacho ni kama Antony. Ndio ni kijana mdogo lakini haiba yake, baadhi ya mambo sio mazuri na ni mbaya kwa klabu. Hili linaonekana katika kiwango chake na kukosa muendelezo wake,” amesema Meulensteen.
Licha ya kutoonyesha kiwango bora akiwa na Man United, Antony ameonyesha makali katika jezi za Real Betis aliyoichezea kwa mkopo kwa muda wa miezi sita.
Katika kipindi hicho amechezea idadi ya mechi 26, akifunga mabao tisa na kupiga pasi tano za mwisho.
Garnacho katika mechi 58 alizoichezea Man United msimu wa 2024/2025, amehusika na mabao 21 akifunga 11 na kupiga pasi za mwisho 10.