Liverpool kukamilisha usajili wa Wirtz

Muktasari:
- Imethibitishwa kuwa Wirtz amezikataa Bayern Munich na Manchester City jambo linalodhihirisha wazi dhamira yake ya kuvaa jezi ya majogoo wa Anfield msimu ujao.
Liverpool imepanga kutoa ofa ya mwisho kwa ajili ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz, baada ya klabu hiyo ya Ujerumani kugomea ofa ya pauni milioni 113 kutoka kwa vigogo hao wa Anfield. Kwa mujibu wa Daily Mail, Leverkusen wanasisitiza kwamba wako tayari kumuuza Wirtz kwa pauni milioni 118, kiwango kinachoelezwa kuwa kitafanikisha dili hilo.
Wirtz ambaye alikuwa sehemu ya mafanikio ya Leverkusen chini ya kocha Xabi Alonso, ikimaliza msimu wa 2023-2024 bila kupoteza mchezo wowote kwenye Bundesliga, tayari ameonyesha nia ya kujiunga na Liverpool. Imethibitishwa kuwa Wirtz amezikataa Bayern Munich na Manchester City jambo linalodhihirisha wazi dhamira yake ya kuvaa jezi ya Majogoo wa Anfield msimu ujao.
Ofa ya awali ya Liverpool ilikuwa pauni milioni100 kama ada ya awali, na pauni milioni 13 nyingine kama bonasi, lakini haikukidhi matarajio ya Leverkusen.
Hata hivyo, vyanzo vya ndani nchini Ujerumani vinasema kuwa majadiliano sasa yako katika hatua ya mwisho, ambapo pande zote mbili zinaelewana kuhusu masharti ya bonasi. Leverkusen wanataka bonasi zaidi kama njia ya kuongeza thamani ya dili hilo.
Kwa upande Liverpool wanaamini kwamba mchezaji huyo mwenye miaka 21 ni miongoni mwa vipaji bora zaidi Ulaya kwa sasa, na wanataka kumjumuisha haraka katika kikosi chao kinachojiandaa kwa msimu mpya wa Premier League.
Mbali na Wirtz, Liverpool pia wameweka jicho lao kwa beki wa kushoto wa Bournemouth, Milos Kerkez. Klabu ya Bournemouth imeweka bei ya pauni milioni 45, lakini mkurugenzi wa usajili wa Liverpool, Richard Hughes ambaye aliwahi kuwa Bournemouth, anatarajiwa kutumia ushawishi wake kupunguza bei hiyo katika siku chache zijazo.
Wakati huo huo, Liverpool pia wanajiandaa kusawazisha vitabu vyao vya kifedha baada ya kukamilisha usajili wa gharama kubwa. Mshambuliaji Federico Chiesa, ambaye alisajiliwa kutoka Juventus msimu uliopita, anafikiria kurudi Italia baada ya kucheza mechi chache Anfield.
Aidha, wachezaji kama Darwin Nunez, Harvey Elliott, na Kostas Tsimikas wako katika orodha ya wachezaji wanaoweza kuuzwa msimu huu, ingawa hakuna mazungumzo ya kina yaliyofanyika hadi sasa.