Simba yamaliza viporo kwa kishindo

Muktasari:
- Simba imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo huo wa nne mfululizo ndani ya siku 10.
Mechi za viporo ambazo zilikuwa mezani kwa Kocha Fadlu Davids limefungwa rasmi jana Jumapili kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam baada ya Simba SC kukamilisha mechi nne kwa mafanikio makubwa kwa kukusanya pointi zote 12.
Simba imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo huo wa nne mfululizo ndani ya siku 10.
Simba ilikuwa na mechi nyingi mkononi kutokana na kushiriki kwao katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hali ambayo iliwafanya kuchelewa kucheza mechi kadhaa za ligi huku mpinzani wao, Yanga, ikiendelea na ratiba ya kawaida ya ligi.
Ushindi huo umeifanya timu hiyo kufikisha pointi 69 baada ya mechi 26, ikibaki nyuma kwa alama moja tu dhidi ya Yanga ambayo nayo imecheza idadi sawa ya mechi.
KMC ilikuwa ya kwanza kufungua pazia la mabao katika dakika ya nane kupitia kwa Rashid Chambo ambaye alifunga kwa shuti kali nje ya boksi likiwa ni bao la 11 Simba inaruhusu msimu huu.
Hilo lilikuwa bao la tatu anaruhusu Camara katika mechi nne za viporo.
Kipa huyo ameruhusu mabao katika mechi tatu dhidi ya Pamba Jiji (5-1), Mashujaa (2-1) na jana dhidi ya KMC. Mechi pekee aliyotoka bila kuruhusu bao ilikuwa dhidi ya JKT Tanzania.
Simba ilijibu haraka bao hilo kwa kusawazisha dakika nane kupitia kwa Steven Mukwala, aliyeunganisha pasi ya Joshua Mutale ambaye alianza kwa mara ya tatu mfululizo kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.
Hilo lilikuwa bao la 10 kwa Mukwala msimu huu kwenye ligi, likimweka katika nafasi ya tatu kwenye orodha ya wafungaji bora wa Simba nyuma ya Charles Jean Ahoua mwenye mabao 15 na Leonel Ateba mwenye mabao 12.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na katika dakika ya 47, Mukwala aliipatia Simba bao la pili baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa KMC na kufunga kwa ustadi mkubwa akipata pia pasi kutoka kwa Mutale.
Simba ambayo inatarajiwa kuondoka keshokutwa kwenda Morocco kuvaana na RS Berkane imebakiza michezo minne kwenye ligi dhidi ya Singida Black Stars, Yanga SC, Kengold ambayo tayari imeshuka daraja na Kagera Sugar ambayo inahaha kuikwepa nafasi ya kushuka daraja.
Matarajio makubwa kwa sasa yapo kwenye mchezo wa dabi dhidi ya Yanga, mechi ambayo huenda ikaamua bingwa wa ligi msimu huu. Simba inahitaji ushindi katika mechi hiyo ili kukaa kileleni mwa msimamo.