Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yafa kiume Amaan

Simba ikiwa kwenye aridhi ya Tanzania kwa mara ya pili imeshindwa kutwaa ubingwa wa Caf, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Berkane.

Huu ulikuwa mchezo wa pili wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar baada ya mchezo wa kwanza Berkane kushinda kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza nchini Morocco.

Hii ni fainali ya pili Simba inapoteza nyumbani, baada ya mwaka 1993 kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Stella Abdjan ya Ivory Coast kwenye Kombe la Caf baada ya suluhu ugenini.

Katika mchezo wa jana ambao Rais wa Mapinduzi wa Zanzibar, Hussein Mwinyi ndiye alikuwa mgeni rasmi, Simba ilianza mchezo kwa kasi ya hali ya juu na kuliandama lango la Berkane kwa nguvu kubwa ambapo ilifanikiwa kupata bao la katika dakika ya 17 kupitia kwa Joshua Mutale ambaye alifunga kwa ufundi akimalizia krosi iliyopigwa na Elia Mpanzu akaikosa Steven Mukwala ambapo mpira ulimkutana mfungaji.

Baada ya bao hilo, Simba ilionekana kuwa na kasi ya hali ya juu ya kutafuta bao la pili,  ambapo dakika chache baadaye, Shomary Kapombe alikosa nafasi ya wazi baada ya kushindwa kumalizia mpira wavuni kwa kichwa akiwa amebaki na lango na Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kadi nyekundu zawavuruga

Kipindi cha pili kilianza vibaya kwa Simba baada ya dakika tano tu baada ya mpira kuanzishwa, kiungo Yusuph Kagoma alitolewa uwanjani kwa kadi nyekundu baada ya kupewa kadi ya pili ya njano.

Pamoja na kadi hiyo, Simba ilionekana kupambana kuhakikisha kuwa wanapata bao la pili lakini mambo yakawa magumu kwao.

Kagoma alionyeshwa kadi hiyo baada ya kumfanyia madhambi, kiungo wa RS Berkane, Imad Riahi na kusababisha kikosi hicho kucheza pungufu na kukosa nguvu ya kuongeza mashambulizi kwa wapinzani wao.

 Pia kocha msaidizi wa Simba, Darian Wilken alionyeshwa kadi nyekundu baada ya mzozo akiwa katika benchi la ufundi, huku Fadlu Davids akionyeshwa ya njano kutokana na kutokubaliana na maamuzi yaliyokuwa yanaendelea kwa mwamuzi , Dahane Beida raia wa Mauritania ambaye aliwahi kukataa bao ambalo lilifungwa kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Stephane Aziz kwenye mchezo kati ya Yanga dhidi ya Mamelodi.

VAR yawanyima bao

Dakika ya 73, mashabiki wa Simba walinyanyuka kwenye viti wakiamiani kuwa timu yao imesawazisha bao lilowekwa kimiani na mshambuliaji Steven Mukwala, lakini baada ya mwamuzi kutazama kwenye VAR alionyesha mfungaji alikuwa ameotea na kulikataa bao hilo.

Dakika 90+3 Simba yaruhusu bao

Bao la kusawazisha lililofungwa na Soumaila Sidibe, lilizamisha kabisa matumaini ya kikosi hicho kutwaa ubingwa baada ya kufunga dakika za nyongeza wakati Simba wakionekana kushambulia kwa nguvu.

Nyota huyo aliyeingia dakika ya 78, akichukua nafasi ya Mamadou Camara, bao lake la kuchomoa lilikuwa mlima kwa Simba kwani ingewalazimu kushinda mabao 4-1.

Camara, Ngoma wataka kuzichapa

Katika hali isiyo ya kawaida, wachezaji wawili wa Simba SC, kipa namba moja Moussa Camara na kiungo mkabaji Fabrice Ngoma, walinaswa wakiwa kwenye mzozo mkali uliokaribia kugeuka ugomvi wa wazi, wakitaka kuzichapa mbele ya mashabiki kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Tukio hilo lilijiri muda mfupi kabla ya timu kwenda mapumziko, wakati Simba ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 dhidi ya RS Berkane katika mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Chanzo cha ugomvi huo kilianza baada ya Simba kuruhusu kona ya mwisho kuelekea mwisho wa kipindi cha kwanza, ambayo ilitokana na Camara kushindwa kumudu mpira wa juu, na kuufanya utoke nje.

Ngoma, ambaye alionekana kuchukizwa na tukio hilo, alimsogelea Camara kwa hasira, akimtuhumu kutokuwa makini.

Ndipo walipokutana uso kwa uso, wakaanza kurushiana maneno makali. Camara naye hakubaki nyuma, akijibu kwa hisia kali, hali iliyowafanya wachezaji hao kuanza kushikana mashati, kitendo kilichosababisha tafrani ndogo katikati ya uwanja.

Wachezaji wengine wa Simba, wakiongozwa na nahodha Mohamed Hussein 'Tshabalala' waliingilia kati kwa haraka kuwatuliza wawili hao, kabla ya mambo kuwa mabaya zaidi. Tukio hilo lilidumu kwa takriban sekunde 40.