Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba katika vita ya Ubingwa CAF

Muktasari:

  • Nahodha msaidizi wa Simba, Shomari Kapombe amesema kuwa wamejiandaa kufanya vizuri katika Uwanja wa New Amaan Complex leo.

Zanzibar. Ni dakika 90 za uamuzi zinazoweza kuleta furaha au majonzi kwa Tanzania ambazo ni za mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Simba na RS Berkane kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni.

Furaha kwa Watanzania ni kama Simba itafanikiwa kupata matokeo mazuri yatakayoihakikishia ubingwa wa mashindano hayo na hivyo kuuleta kwa mara ya kwanza ubingwa wa mashindano ya klabu Afrika katika ardhi ya Tanzania.

Kinyume na hapo, Tanzania kwa mara ya tatu itapata majonzi ya kushuhudia timu yake kushindwa kutwaa taji la mashindano ya klabu Afrika baada ya Simba kupoteza fainali ya mwaka 1993 ya Kombe la CAF ikifungwa mabao 2-0 na Stella Abdijan ya Ivory Coast na Yanga kuhukumiwa na kanuni ya bao la ugenini katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/2023.

Baada ya kupoteza mchezo wa kwanza ugenini Morocco, Mei 17, 2025 katika Uwanja wa Manispaa ya Berkane kwa mabao 2-0, Simba leo ili itwae ubingwa inapaswa kuifunga RS Berkane kwa ushindi wa tofauti ya mabao matatu au zaidi.

Kama Simba itapata ushindi wa mabao 2-0, mechi itaamriwa kwa mikwaju ya penalti lakini kinyume na hapo, wageni RS Berkane watatwaa taji hilo ambalo litakuwa la tatu kwao kwenye mashindano hayo yanayoshika nafasi ya pili kwa ukubwa na thamani katika ngazi ya klabu Afrika.

Kwa upande mwingine kama Simba itatwaa ubingwa huo, itakuwa ni faraja kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi kwani atakuwa amefanya kile ambacho baba yake Hayati Rais Ali Hassan Mwinyi hakukifanya mwaka 1993 ambacho ni kushuhudia Simba ikitwaa ubingwa huku yeye akiwa mgeni rasmi.


Inawezekana

Kama Simba itafanikiwa kuepuka au kupunguza makosa ya mchezaji mmojammoja hasa katika safu za kiungo na ulinzi, inaweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kupindua meza na kutwaa ubingwa leo.

Lakini pia wachezaji wake wa nafasi za ushambuliaji wanapaswa kuwa na umakini na utulivu wa hali ya juu katika kutumia nafasi ambazo zitapatikana kwenye mchezo huo ili waiwezeshe Simba kupata idadi kubwa ya mabao ambayo inayahitaji kwenye mechi hiyo.

Ikiwa nyota wa Simba watakuwa katika ubora na kupata matokeo mazuri leo haitokuwa jambo la kushangaza bali ni kama marudio tu ya walichokifanya kwenye hatua ya robo fainali dhidi ya Al Masry ya Misri.

Ikiwa ugenini Misri, Simba ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 na iliporudi nyumbani ikapata ushindi kama huo jambo lililofanya refa wa mchezo kuamua kupigwa mikwaju ya penalti ili kumsaka mshindi ambapo Simba ilisonga mbele kwa kushinda kwa mikwaju ya penalti 4-1.

Lakini kumbukumbu ya kile ambacho Simba walikifanya mwaka 1979 dhidi ya Mufulila Wanderers ya Zambia, kinaweza kuleta tumaini kwa mashabiki wake kwamba wanaweza kupata ushindi mnono nyumbani ambao utawafanya watwae ubingwa.

Mwaka 1979, Simba licha ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mufulila Wanderers, ilifanya maajabu ugenini huko Lusaka Zambia baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 ambao uliwafanya waingie raundi ya kwanza ya mashindano hayo.


Fainali ya nyota tano

Idadi ya maofisa walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kusimamia mchezo huo ni ishara tosha ya ukubwa na hadhi ya mechi hiyo.

CAF imeteua maofisa 16 kwa ajili ya kusimamia mchezo na orodha hiyo ndefu itaongozwa na refa wa mchezo Beida Dahane kutoka Mauritania ambaye atasaidiwa na marefa wasaidizi, Jerson Dos Santos kutoka Angola na Adou Desire N’goh kutoka Ivory Coast.

Waamuzi hao watatu watapata sapoti ya refa wa akiba wa mchezo, Abdel Aziz Bouh ambaye naye anatoka Mauriatania.

Kutakuwa na marefa watatu ambao watakuwa kwenye chumba cha teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR) ambao wataongozwa na Issa SY kutoka Senegal.

Marefa wasaidizi wa VAR ni Akhona Makalima wa Afrika Kusini na Arsenio Maringule kutoka Msumbiji.

Maofisa wengine ni Mohamed Yonis (Kamishina), Helly Zafinimanga (Mratibu Mkuu) na Djamel Halmoudi (Mtathmini Marefa), Ahmed Hussein na Clifford Ndimbo (Maofisa Habari), Amr Salman na Joe Sakaumba (Maofisa Usalama), Rasha Elghorour (Mratibu Msaidizi) na Gift Macha ndio Meneja wa Urushaji Matangazo uwanjani.


Ubingwa kuipa noti Simba

Kama Simba itafanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo itapata kitita cha Dola 2 milioni kutoka CAF na ikishindwa kufanya hivyo itapata Dola 1 milioni.

Habari za uhakika ambazo gazeti linazo ni kwamba uongozi wa Simba umetoa ahadi ya Sh1 bilioni kwa wachezaji wa timu hiyo ikiwa watatwaa ubingwa.

Kuna bonasi ya Sh30 milioni kwa kila bao ambalo Simba itafunga ikiwa itapata ushindi ambayo itatolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.


Fadlu, wachezaji washusha presha

Kocha wa Simba, Fadlu Davids amewaomba mashabiki wa Simba wajitokeze kwa wingi huku akiwaahidi matokeo mazuri leo.

"RS Berkane ni timu ya daraja la juu lakini bado hawajakutana na hasira ya Simba Sports Club ikiwa kwenye ubora na uwezo wake kamili. Mchezo wa kwanza kule Morocco tuliuchukulia kama somo kwetu na sasa tupo tayari kwa mchezo," alisema Davids.

Nahodha msaidizi wa Simba, Shomari Kapombe amesema kuwa wamejiandaa kufanya vizuri katika Uwanja wa New Amaan Complex leo.

"Kilichokuwa kinafanyika Benjamin Mkapa tunakileta hapa New Amaan Complex Zanzibar wala hilo halina shaka yoyote. Tupo hapa kucheza kwa hisia za watanzania wote na wanachama wote wa Simba," alisema Kapombe.