Simba yajitwika mabomu kwa Berkane, Fadlu aweka kila kitu wazi

Muktasari:
- Simba inahitaji ushindi wa tofauti ya mabao matatu au zaidi kwenye mechi yake ya marudiano ya hatua ya fainali ili iweze kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Zanzibar. Simba imetamba kuwa maumivu iliyoyapata katika dakika 20 za mwanzo za mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika yanawapa ari ya kufanya vizuri dhidi ya RS Berkane ya Morocco kesho kwenye Uwanja wa New Amaan Complex katika mechi ya marudiano.
Mei 17, 2025 Simba ilijikuta ikiruhusu mabao mawiki ya haraka ndani ya dakika 20 za mwanzo ambayo yameipa kibarua kigumu cha kuhakikisha inapata ushindi wa kuanzia tofauti ya mabao matatu ili itwae ubingwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Zanzibar, Fadlu amesema: “Ndiyo, tulikuwa tumejiandaa kikamilifu kwa mechi ya kwanza. Tulikuwa tumepanga kila kitu kiufundi na kimkakati, lakini jambo kubwa zaidi lilikuwa kuwapa wachezaji uzoefu wa dakika zile 20 za mwanzo kwa sababu unaweza kuwa na mpango mzuri lakini hali halisi ya uwanja na mazingira ya fainali huwezi kuifundisha darasani. Lazima waishi nayo, wapitie, na wakue kupitia hilo.”
Katika mechi wa kwanza iliyochezwa Morocco, Simba ilikubali kichapo cha mabao 2-0. Hata hivyo, Fadlu anaamini kuwa kikosi chake sasa kiko tayari kwa pambano la marudiano, licha ya mchezo huo kuhamishiwa Zanzibar badala ya uwanja wao wa nyumbani wa Benjamin Mkapa.
“Tunajua Benjamin Mkapa ni faida kubwa kwetu. Ni uwanja wenye historia. Timu nyingi kubwa kama Al Ahly na Wydad zimekuja pale na kutoka bila pointi. Lakini hatutaficha, tunaumia kwamba mechi hii haipo pale,” alisema Fadlu.
“Lakini hata hivyo, hatutumii hilo kama kisingizio. Tumekuja hapa Zanzibar tukiwa na imani na fahari. Tunaamini Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla watasimama nyuma yetu.”
Fadlu alisema ana uhakika kuwa wakati basi la timu likifika uwanjani, wataona “mashabiki wao” wakilizunguka, wakipiga kelele na kushangilia kama ilivyo kawaida yao Simba, jambo analoamini litatoa msukumo kwa wachezaji wake kupambana hadi mwisho.
“Tunahitaji kuigeuza Zanzibar kuwa nyumbani kwetu. Tuifanye iwe kama Benjamin Mkapa. Hilo linawezekana kama Watanzania wataungana na kusimama pamoja nasi. Huu ni wakati wa umoja.”
Akizungumzia mechi ya kwanza, Fadlu alisema pamoja na Simba kufungwa, walijifunza mengi. “Nilipata kadi ya njano si kwa sababu ya hasira bali kuamsha wachezaji wangu. Walihitaji kujua kwamba hii ni vita, na licha ya mazingira magumu, wao ni timu nzuri na wanaweza kushindana.”
“Berkane walikuwa na mabao mawili, lakini kwa takwimu walikuwa na expected goals 1.18. Camara (Mussa) alifanya kazi kubwa sana. Aliokoa bao la wazi. Hilo lilitufanya tubaki mchezoni.”
Fadlu alisema kipindi cha pili walifanya mabadiliko ya kimkakati na mchezo ukawa wa kushindana zaidi. “Tulikuwa na nafasi nusu-nusu, wao pia. Lakini mwisho wa siku, wachezaji wangu walitoka uwanjani wakiwa na imani kuwa wanaweza kushindana. Tumejifunza, tumejipanga, na sasa tunasubiri mchezo wa marudiano kwa matumaini makubwa.”
Simba inahitaji ushindi wa mabao matatu bila nyavu zao kuguswa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza. Mechi hiyo ya marudiano inatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar, uwanja ambao Fadlu anautazama kama eneo jipya la kihistoria kwa Simba ikiwa watapindua meza.