Camara wa Berkane aipa saluti Simba

Muktasari:
- Mamadou Camara alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 ambao RS Berkane iliupata dhidi ya Simba katika mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho.
Zanzibar. Licha ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata katika fainali ya kwanza dhidi ya Simba SC huko Morocco, kiungo Mamadou Camara wa RS Berkane amesema kuwa hawatarajii mechi nyepesi katika mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Amaan.
Camara ambaye ni raia wa Senegal, amesema wanaiheshimu Simba kama timu kubwa barani Afrika lakini wamekuja Zanzibar wakiwa na dhamira moja kuhakikisha wananyakua taji la tatu la Kombe la Shirikisho Afrika.
“Hatujui kama itakuwa rahisi dhidi ya timu ya Simba ambayo ni timu nzuri sana. Tupo hapa tukitambua kile kinachotukabili. Tupo kwa ajili ya mechi ya furaha fainali ni muda wa historia,” amesema Camara.
Katika mechi ya kwanza iliyofanyika mjini Berkane, mabao ya Camara na Oussama Lamlaoui yaliipa Berkane ushindi wa 2-0, na kuwapa faida ya kuwa mbele.
Hata hivyo, Camara anaamini nafasi walizopoteza katika mechi hiyo ni jambo walilolifanyia kazi ili kuhakikisha hawapotezi ufanisi tena.
“Tulisema hatukufurahishwa sana kwa sababu tulikosa ufanisi. Tulipaswa kushinda zaidi. Lakini muhimu zaidi ni kwamba baada ya mechi ile, tumepata mafunzo mengi. Tumefanyia kazi hilo ili tusirudie makosa katika mechi ya kesho,” alisema.
Camara pia aliweka wazi kuwa kwa sasa hafikirii chochote kuhusu mustakabali wake wa baadaye kwa sababu ana mkataba na RS Berkane na anafurahia maisha ndani ya klabu hiyo.
“Kwa sasa nina mkataba na Berkane. Nina furaha, niko vizuri hapa. Kwa sasa siwezi kuzungumzia siku za baadaye, akili yangu yote ipo kwenye fainali hii ambayo ni muhimu sana kwetu. Baada ya hapo, tutaona,” aliongeza.
Camara, mmoja wa wachezaji waliokuwa kwenye kiwango bora msimu huu, anatarajiwa kuwa mchezaji muhimu katika kiungo cha Berkane.